DODOMA,Tanzania
Pamoja na kubatilisha uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Kagera wa kuwafukuza madiwani wanane wa CCM katika Halimashauri ya Bukoba mjini kwa utovu wa nidhamu, leo Kamati Kuu ya CCM imeagiza serikali kumtuma Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu katika Halmashauri hiyo kupata ukweli halisi wa tuhuma za ufisadi anaodaiwa kufanya Meya wa Halmashauri hiyo, Anatory Amani.
|
Meya Anatory Amani |
Kamati Kuu imechukua hatua hiyo, baada ya kuwahoji Mwenyekiti na Katibu wa CCM mkoa wa Kagera, Mwenyekiti na Katibu wa CCM wilaya ya Bukoba mjini na Mbunge wa Bukoba mjini Hamisi Kagasheki na Meya wa Halmashauri hiyoi, mjini Dodima na kubaini kwamba moja ya mambo yanayodaiwa kuchangia sakata hilo hadi kufukuzwa madiwani hao, ni kuwepo kwa tuhuma za ufisadi dhidi ya Meya huyo katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza leo na mjini hapa, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye amesema, leo Kamati Kuu imetoa uamuzi wa kubatilisha hatua ya kufukuzwa kwa madiwani hao, baada ya kubaini kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera haikuzingatia Katiba ya CCM ya 1977 Toleo la 2012 Ibara ya 93 (15), ambayo inaelekeza kazi na majukumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa.
“Ibara hiyo inasema kumwachisha au kumfukuza uongozi, kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa, isipokuwa kwa suala la kumvua uanachama au uongozi Diwani lisifanyike hadi Kamati Kuu imearifiwa na kutoa maelekezo” alisema Nape.
Kufuatia hatua hiyo, CCM imewataka madiwani hao kuendelea na kazi zao na imewaonya viongozi wote wa chama mkoa, wilaya, Meya na mbunge kuhakikisha inarudisha hali ya utulivu na amani.
Nape alisema Kamati Kuu imewaonya madiwani wa CCM wa Manispaa ya Bukoba, Mbunge wa Bukoba Mjini na Meya kwa kusababisha kukosekana kwa utulivu, mshikamano na amani katika Manispaa na Chama.
“Wakati tuhuma za Meya zikichunguzwa, Kamati Kuu inawataka madiwani wa CCM kurejesha utulivu kwenye manispaa na Chama kwa ujumla ili kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwaletea maendeleo wananchi wa Bukoba,’’alisema.
Madiwani waliokuwa wamevuliwa na uanachama katika sakata hilo ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na Dauda Karumuna (Ijuganyondo).
Inadaiwa madiwani hao waliungana na wenzao wa wapinzani kupinga maamuzi mbalimbali yaliyofanya na Meya Tarimo, madiwani hao ni Dismas Rutagwelera (Rwamishenyi), Israel Mlaki (Kibeta), Winifrida Mkono (Viti Maalumu), Conchesta Rwamlaza ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu CHADEMA na Ibrahim Mabruk (Bilele), Felician Bigambo (Bakoba) na Rabia Badru (Viti Maalumu - CUF).
Maamuzi yaliyofanywa na Meya huyo, ambayo yamepingwa na madiwani kuwa ameiingiza manispaa katika ufisadi kwenye miradi kadhaa. Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh. bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu pamoja na kudaiwa kukopa sh. milioni 200 katika Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani.
Aidha, inadaiwa kuwa Meya huyo alitoa taarifa katika kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake, pamoja na kuwepo kwa mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh. milioni 297 zinazotiliwa shaka.
Pia, Meya ameshindwa kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi kiasi cha sh. milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Imetayarishwa na theNkoromo Blog.************************************TAARIFA RASMI YA CCMTAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa imejadili na kutolea maamuzi pamoja na mambo mengine suala la Madiwani wanane waliotangazwa kufukuzwa uanachama na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera.
Katika maamuzi yake, Kamati Kuu imebatilisha uamuzi uliofanywa na Halmashauri Kuu CCM ya Mkoa wa Kagera Agosti 13, 2013 wa kuwafukuza uanachama Madiwani hao. Hivyo Madiwani hao wanane ni wanachama halali wa CCM.
Kamati Kuu imetoa uamuzi huo, baada ya kubaini kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera haikuzingatia Katiba ya CCM ya 1977 Toleo la 2012 Ibara ya 93 (15). Ibara hiyo inasomeka kuwa moja ya kazi ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ni:-
“Kumwachisha au kumfukuza uongozi kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa, isipokuwa kwa suala la kumvua uanachama au uongozi Diwani lisifanyike hadi Kamati Kuu imearifiwa na kutoa maelekezo”.
Aidha, Kamati Kuu imewaonya Madiwani wa CCM wa Manispaa ya Bukoba, Mbunge wa Bukoba Mjini na Meya kwa kusababisha kukosekana kwa utulivu, mshikamano na amani katika Manispaa na Chama.
Kamati Kuu pia imeitaka Serikali kumwagiza mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali(CAG) kufanya ukaguzi maalum wa haraka wa mambo yanayolalamikiwa dhidi ya Meya ili ukweli ujulikane na matokeo ya uchunguzi huo yasilishwe kwenye baraza la madiwani ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoongoza Serikali za Mitaa.
Wakati tuhuma hizo dhidi ya Meya zikichunguzwa; Kamati Kuu inawataka Madiwani wa CCM kurejesha utulivu kwenye Manispaa na Chama kwa ujumla ili kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwaletea maendeleo wananchi wa Bukoba.
Imetolewa na:-
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CCM
ITIKADI NA UENEZI
27/08/2013
DODOMA,Tanzania Pamoja na kubatilisha uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Kagera wa kuwafukuza madiwani wanane wa CCM katika Halimasha...
[Read More]