Katibu wa CCM wilaya ya Makete Miraji Mtaturu (kushoto)akimuagiza diwani wa kata ya Bulongwa ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya fedha na mipango wilaya ya halmashauri ya Makete kupeleka maagizo ya kutolipwa kwa mkandarasi huyo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya makete Francis Chaula akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Luwumbu Makete
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya makete Francis Chaula akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Luwumbu Makete
Moja ya sehemu ya barabara ya Bulongwa - Luwumbu ambayo imewekwa kifusi ambacho si rafiki na mazingira ya kata hiyo.
Na Edwin Moshi, Makete
Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Makete kimeishukia serikali ya halmashauri ya wilaya hiyo kwa kumtaka mkandarasi anayekarabati maeneo korofi katika barabara ya Bulongwa-Luwumbu kurudia kuweka kifusi imara kwenye barabara hiyo na kutoa udongo waliouweka kwani hauna msaada kwenye barabara hiyo
Chama hicho kimekwenda mbali zaidi kwa kumtaka diwani wa kata hiyo kukataa kusaini hati ya kuidhinisha mkandarasi huyo alipwe fedha za kazi hiyo mpaka atakaporekebisha barabara hiyo kwa kuweka kifusi imara ambacho kitawaridhisha wananchi na watumiaji wa barabara hiyo
Kauli hiyo imetolewa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Usililo kata ya Luwumbu wilayani hapa na katibu wa CCM wilaya ya Makete Miraji Mtaturu, ambapo pamoja na mambo mengine wananchi wameoneshwa kukerwa na ukarabati wa barabara hiyo, ambapo kabla ya mkutano huo msafara wa viongozi hao ulishangazwa na uwekaji wa kifusi ambacho si rafiki wa mazingira ya kata hiyo
Kufuatia sakata hilo, chama hicho kupitia kwa Katibu Mtaturu walimuagiza diwani wa kata ya Bulongwa ambaye ni mjumbe wa kamati ya fedha na mipango ya halmashauri ya wilaya ya Makete ambayo inaidhinisha malipo ikiwemo ya wakandarasi, kupeleka taarifa wilayani kuwa mkandarasi huyo asilipwe fedha mpaka arekebishe barabara hiyo kwa kuweka kifusi kinachokubalika
"wananchi nawahakikishia mkandarasi huyo hatalipwa fedha, maana kifusi alichokiweka mvua ikinyesha tu maeneo yote yatakuwa na utelezi na hayatapitika, na huku kuna mazao na shughuli nyingi sasa hii kero hadi lini, sisi hatutaki matusi baadaye kutoka kwa watu, tunataka kazi hii ifanyike mara moja" alisema Mtaturu
Akihutubia wananchi mkutanoni hapo mwenyekiti wa CCM wilaya Makete Francis Chaula amewataka wananchi hao kutokubali kurudishwa nyuma kimaendeleo na kuzitumia rasilimali zilizopo katani hapo kwa maendeleo yao wote huku wakiwakemea na kukaa mbali na wale wanaokwamisha maendeleo yao
Amesema kutokana na kata hiyo kupewa mfereji wa umwagiliaji ambao hivi sasa una mgogoro na mtu aliyejitokeza na kudai eneo lililojengwa mfereji huo ni lake na kupeleka kesi hiyo mahakamani, wapambane hadi dakika ya mwisho kutetea mfereji huo na kwani chama hicho kipo nyuma yao kuhakikisha wanashinda katika kutetea mradi huo wenye manufaa kwa kata hiyo
Ziara hiyo ya viongozi wa CCM wilaya ya makete wakiongozwa na mwenyekiti Francis Chaula imefanyika katika vijiji vya Uganga, Luwumbu, Unenamwa na Usililo ambavyo vipo katika kata ya Luwumbu kwa lengo la kusikiliza kero na maoni ya wananchi hao.