Google PlusRSS FeedEmail

MAGUFULI AVUNA WANACHAMA WAPYA 376 CHATO

Mbunge wa Jimbo la Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli akipeana mikono na Wanachama wapya wa Chama cha Mapinduzi (CCM) walioamua kujiunga na chama hicho mara baada ya Mbunge huyo kufanya Mkutano mkubwa wa hadhara katika kijiji cha Nyabugela, kata ya Mganza katika Wilaya ya Chato leo.
Mbunge wa Jimbo la Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli kihutubia mamia ya wakazi wa kata ya Mganza katika Wilaya ya Chato leo.
Wananchi wa Kata ya Mganza wakimfurahia Mbunge wa Jimbo lao la Chato Mheshimiwa Dkt. John Magufuli wakati akiwahutubia na kuwasisitiza wafanye kazi kwa bidii ili waweze kujiletea Maendeleo.
Mbunge wa Jimbo la Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli akiwapokea wanachama wapya zaidi ya 100 walioamua kujiunga na Chama cha Mapinduzi CCM mara baada ya mbunge huyo kumaliza hotuba yake.
Wanachama wapya wa Chama cha Mapinduzi kata ya Mganza wakila kiapo mbele ya Mbunge wao Mheshimiwa Dkt.John Magufuli ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi baada ya kukabidhiwa kadi za uanachama hivi leo.

Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni mbunge wa Chato Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli amezidi kuongeza idadi ya wanachama wapya katika Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya mkutano wake wa siku moja kuzoa wanachama wapya 376.

Hali hiyo imekua pigo kubwa kwa vyama vingine vya siasa kwasababu katika muda mfupi wa mikutano ya Mbunge huyo idadi ya wanachama waliotoka katika vyama vya upinzani imezidi kuongezeka.
Katika mikutano hiyo iliyofanyika katika vijiji vya Nyisanzi, Kasenda na Muganza. Dkt. Magufuli alieleza jinsi alivyotekeleza ahadi mbalimbali zilizomo kwenye za Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika kutatua kero mbalimbali za wanachi.

“Mlinichagua kwa kura nyingi sana hapa na mimi lazima nionyeshe mfano katika kuwatumikia na naahidi vitu vyote nilivyoahidi nimetekeleza kwa sehemu kubwa kuanzia kwenye shule, huduma za afya, barabara, maji na umeme” alisema Dkt. Magufuli
Katika hatua nyingine Dkt. Magufuli aliwaasa vijana kufanya kazi kwa bidii na kuacha kudanganywa na wanasiasa uchwara.

“Nawaambia hakuna kitu cha bure, wala hakuna mtu atakayewaletea kitu chochote kama hamtajishughulisha, mfanye kazi muache maneno ya kukaa vijiweni” alisema Dkt Magufuli 
Akizungumza huku akishangiliwa na umati wa watu, Dkt. Magufuli aliwataka wakazi wa Muganza kufanya kazi kwa bidii na kutumia fursa za kiuchumi zinazoanza kufunguka katika kata hiyo.

“Hapa Muganza ndipo linajengwa lango kuu la watalii kuelekea hifadhi ya Taifa ya Rubondo, hivyo ni bora mkajianda mapema na fursa hii, mkikaa bila kufanya kazi fursa hizi zitawapita tu” alisema Dk. Magufuli
Aidha, Mbunge huyo wa Chato pia alisema watanzania wanatakiwa kudumisha Amani iliyopo isije kupotea kwani gharama yake ni kubwa.

Waziri Magufuli alitolea mfano wa nchi za Misri, Libya na Iraq jinsi zilivyokuwa na Amani hapo zamani lakini sasa hivi hali yake ni mbaya watu wanauana kila muda.

“Wakataeni wanasiasa wanaohubiri siasa chafu za kuvuruga Amani, na eti kudai hadi kieleweke vinginevyo damu itamwagika, akija mtu kama huyo mwambieni amwage damu yake kwanza, msimkubali kwani atawapoteza” alisisitiza Dkt. Magufuli.

Katika hatua nyingine Waziri Magufuli amewaahidi wakazi wa Muganza kuwa Serikali itamalizia kipande cha barabara kisichozidi kilomita tatu katika kata hiyo, kwani ni ahadi ya Mhe. Rais na tayari Wizara ya Ujenzi kwenye bajeti yake ya mwaka huu wa fedha 2014/15 imetenga kiasi cha sh. 50.mil kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mwanzo ya ujenzi wa barabara hiyo.

“Serikali ya CCM imeahidi na itatekeleza ahadi yake, tumejenga barabara kila kona ya nchi hatuwezi kushindwa kumalizia kipande hichi kidogo, alisema Dkt. Magufuli .

Pia katika mikutano hiyo waziri Magufuli alitoa michango mbalimbali katika shule na vituo vya afya.

This entry was posted in

Leave a Reply