Mkandarasi mkuu wa ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo Haraka, Strabag International GmbH imetangaza kufungwa kwa muda kipande cha makutano ya Kawawa na barabara ya Kinondoni kuanzia leo Julai 5 hadi kesho Julai 6 2014.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Yahya Mkumba, alisema kipande cha makutano ya Kawawa na barabara ya Kinondoni kitafungwa kuruhusu ujenzi unaoendelea kwenye eneo hilo la barabara hizo.
Akielezea zaidi alisema sehemu hiyo itafungwa kupisha ujenzi wa miundo mbinu ya mabasi yaendayo haraka.
“Tutafunga kipande hicho katika muendelezo wa ujenzi wa barabara ya mradi wa mabasi yaendayo haraka unaolenga kuboresha miundombinu hapa jijini,” alisema.
Alifafanua kuwa watumiaji wa barabara ya Kinondoni kuelekea Morocco na Magomeni wanashauriwa kutumia barabara ya Togo kupitia Karago kama njia mbadala na wale wanaotokea Morocco au Kawawa kuelekea Kinondoni Makaburini wanashauriwa kutumia barabara ya Mtama
“Tunaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaotokea,” alisema.
Mradi wa Mabasi yaendayo haraka unatarajiwa kuondoa adha ya foleni katika jiji hilo na kuleta ufanisi wa usafiri.