Google PlusRSS FeedEmail

UMOJA WA MATAIFA WAONGEZA VIWANGO VYA POSHO ZA WALINZI WA AMANI

Na  Mwandishi Maalum, NEW YORK
Baada ya  vuta ni kuvute  ya  muda mrefu na  majadiliano  makali   baina ya  nchi zinazotoa walinzi wa Amani ( TCC) na zile zinazochangia raslimali fedha,  hatimaye  siku ya alhamisi ( Julai 3).


Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,  lilipitisha nyongeza ya posho kwa walinzi  wa amani kutoka posho ya sasa ya dola  za kimarekani 1, 028  kwa mwezi hadi dola  za kimarekani 1,410   kwa mwezi.

Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa,  lilipitisha  nyongeza hiyo  baada ya  Kamati ya  Tano inayohusika na masuala ya Utawala na Bajeti kukamilisha majadiliano ambayo  yamedumu kwa miezi miwili na  wakati mwingine yaliendelea  usiku kucha ili kufikia makubaliano  ya  nyongeza hiyo ambayo  haijawahi kufanyiwa marekebisho kwa zaidi ya miaka 20.


Kwa  mujibu ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili yaani nchi zinazotoa walinzi wa Amani  ambao wengi wao wanatoka nchi za  Asia ya Kusini na Afrika na  wachangiaji wakubwa wa raslimali fedha wakiwamo  Japani ,   nyongeza hiyo ya  posho kwa walinzi wa Amani  itakuwa ikiongezeka kwa awamu   tatu.


Mgawanyo  huo itakuwa kama ifuatavyo, Julai mosi 2014  nyongeza ya posho itakuwa  dola za kimarekani 1,332.    Julai Mosi 2016 itaongezeka na kuwa dola za kimarekani  1,365 na awamu ya tatu  itaanza Julai Mosi 2017 ambapo posho itakuwa dola za kimarekani  1,410 kwa mwezi.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, litapitia   nyongeza hiyo ya posho baada ya miaka minne.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Uwakilishi wake wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa,  umeshiriki  kikamilifu katika mchakato mzima wa majadiliano  hayo ambayo hatimaye yaliwezesha kufikia muafaka wa nyongeza hiyo.


Nyongeza hiyo  posho ya dola za kimarekani  1,410 kwa mwezi ni tofauti na pendekezo  lililotolewa na   Jopo la wataalamu  waliopewa  jukumu ya kufanya  utafiti wa kisayansi    ili kupata  kiwango stahili cha nyongeza ya posho hasa kwa kuzingatia gharama kubwa  ambazo nchi zinazotoa wanajeshi  na vifaa zilikuwa  zikitumia katika maandalizi,  lakini pia  mazingira  magumu na hatarishi ambayo walinzi hao wa Amani wanakabiliana nayo.

Baada ya utafiti huo  Jopo hilo la Wataalamu lilikuja na pendekezo la nyongeza ya dola za kimarekani   1,762 kwa mwezi wa  kila  mlinzi wa Amani anayehudumu katika   ulinzi wa Amani katika Umoja wa Mataifa. Ingawa pendekezo hilo la  dola 1,762 liliungwa mkono na nchi zinazotoa wanajeshi wao, lakini  ilikuwa  gumu kukubaliwa na   nchi zinazotoa raslimali fedha licha ya kwamba kama ilivyokuwa kwa watoa walinzi wa Amani, nazo zililidhia kufanyika kwa utafiti huo wa kisayansi.


Pamoja na kupitisha nyongeza hiyo ya posho kwa walinzi wa Amani,  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa  pia limepitisha   Bajeti ya  Operesheni za Ulinzi wa Amani ambayo  imefikia dola za kimarekani 7 bilioni kwa mwaka.


Aidha  Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika  kikao chake cha Alhamisi pia kimepisha dola za  kimarekani 7.5 milioni  kwaajili ya mzunguko wa vifaa na zana za kijeshi. Kupitishwa kwa fedha hizo kumetokana na   pendekezo lililotolewa na Kikundi  Kazi  kuhusu  vifaa na zana za  kijeshi ambazo hutolewa na  nchi  zinazotoa walinzi wa Amani.  Dola hizo 7.5 milioni ni sehemu ya  bajeti  ya jumla ya  Operesheni za kulinda Amani  yaani dola za kimarekani  7 Bilioni.


Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya  nchi zinazoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya walinzi wa Amani   wanaohudumu katika  Operesheni za Kulinda Amani za Umoja wa Mataifa.

This entry was posted in

Leave a Reply