MWANZA, TANZANIA
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi Itikadi na Uenezi Ndugu Nape Nnauye amefafanua juu ya Mkakati uliopo sasa wa Chama Cha Mapinduzi wa kujihuisha. Nape ameyaeleza hayo leo asubuhi alipotembelea katika studio za Kituo Cha Televisheni cha Star Tv kilichopo Jijini hapa katika Kipindi cha Tuongee Asubuhi.
Nape alitoa Ufafanuzi kuwa kwa Taasisi ya Kisiasa kama Chama Cha Mapinduzi ambacho asili ya kuundwa kwake kimetokana na Chama Cha TAA na baadae kuwa na mabadiliko ya muundo na jina mpaka kufikia CCM ya sasa hatua za mabadiliko haya zinabeba tafsir ya kujihuisha na kukifanya Chama Kubaki na Nguvu yake na Uwezo wa kiutendaji na Utekelezaji wa ILANI yake kulingana na mazingira husika.
Pia Nape alieleza kuwa Utaratibu uliopo sasa wa Chama Kuzunguka na Mawaziri katika sehemu mbalimbali ambapo Chama Kinafanya mikutano ya hadhara na kusikiliza pamoja na kutatua kero mbalimbali na changamoto ambazo wananchi wanakutana nazo. Na kueleza kuwa Mkakati huu wa kuzunguka na Mawaziri unatokana na ukweli kuwa Chama Cha Mapinduzi ndicho chenye dhamana mbele ya wananchi ya kujibu na kujieleza juu ya utendaji wa Serikali.
Pamoja na hayo, Nape akawataka watu kuacha kutoa tafsir potofu na kuwataka watu waelezee uhalisia wa mapungufu yaliyopo kwenye Chama na Serikali bila kuongezea chumvi na kuyakuza kwa lengo la kutaka kuonesha wananchi kuwa Chama kimeshindwa kuisimamia Serikali yake. Akatoa mifano na takwimu mbalimbali na kuelezea ukweli juu ya kelele za uzushi kuwa CCM inaongozwa na watoto wa vigogo na kueleza kuwa kati ya wanachama zaidi ya 5000 waliojitokeza kuwania nafasi za uongozi ndani ya Chama ni wanachama ambao hawazidi 20 ndio wenye majina ya wanasiasa na miongoni mwao hao wapo waliokosa, kwa maana hawakuchaguliwa.
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi yupo Mwanza kwa ziara maalum Mkoani humo, ambapo amefuatana na wasaidizi wake na ziara hiyo itaisha hivi karibuni.