*YAWATAKA WATANZANIA HERI YA KRISMAS NA MWAKA MPYA
*YAWATAKA KUWA NA KIASI KATIKA SHAMRASHAMRA
* ASEMA USHINDI WA LEMA, NI ISHARA YA UTAWALA BORA WA SERIKALI YA CCM
NA BASHIR NKOROMO, CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema, baada ya kuutumia mwaka 2012 kupanga safu ya uongozi katika chaguzi za ngazi zote zilizomalizika hivi karibuni, mwaka ujao wa 2013 utakuwa wa kuchapa zaidi. Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) Mwigulu Nchemba (pichani) alisema, kazi itakayofanywa na CCM katika mwaka huo, ni pamoja na kukagua upya utekelezaji wa ilani ya CCM na kuhakikisha zile ambazo hazikamilika zinamalizwa.
"Mwaka huu wa 2012 unaomalizika tuliutumia zaidi kujipanga katika uchaguzi wa ngazi zote ili kupata safu nzuri itakayoisimamia serikali kutekeleza ilani ya CCM, sasa mwaka mpya wa 2013 utakuwa wa kazi zaidi za kusimamia serikali ili kuhakikisha mwaka 2015 mpiganaji wa CCM tutakayemteua kugombea urais anapita kiulaini", alisema Mwigulu.
Akizungumzia tukio la Mbunge wa Arusha Godless Lema kushinda rufani yake dhidi ya hukumu iliyomvua ubunge Aprili mwaka huu, Mwigulu alisema, ushindi huo ni ushahidi kwamba serikali ya CCM inaongoza kwa misingi ya utawala bora ambapo kila anayestahili haki anapata.
"Ushindi huu wa Lema, siyo kwamba anaakili sana au chama chake kina maarifa sana yaliyosababisha ushindi, ila ni kutokana na serikali ya CCM iliyopo madarakani kuheshimu na kujali haki na kwa kweli natumia fursa hii kuipongeza Serikali kwa kuthamini na kusimamia haki wakati wote.. Ninyi si mnajua katika nchi zisizo na utawala bora jinsi ambavyo mambo huwa kwenye kesi kama hizi. lakini hapa Tanzania ni tofauti kabisa", alisema, Mwigulu.
Aliwashangaa Chadema akisema, "Hawa ni watu wa aina yao, waliposhindwa katika kesi Arusha walisema Ikulu imeingilia na majaji hawajui kiingereza.. sasa leo wameshinda wanafurahi na kuona kwamba sasa majaji wanajua kiingereza na hawakuigusa Ikulu kwamba imeingilia, maana pale ilipotolewa hukumu umbali wake ni hatua chache na Ofisi ya Ikulu kuliko Arusha".
Mwigulu alitumia fursa hiyo kuwatakia heri Watanzania kwa sikukuu za Krismas na mwaka mpya na kuwataka kuzitumia sikukuu hizo kwa makini na kwa kiasi ili zisiwe chanzo cha matatizo kwao badala ya furaha.
"Chama Cha Mapinduzi kinawatakieni sikukuu njema za Krismas na mwaka mpya, lakini tunawaomba msherehekee kwa kiasi huku mkichunga usalama wenu na mali zetu", alisema Mwigulu.
kazi tu 2013!
Mungu aendelee kuwapa hekima Viongozi wa Tanzania Watuongoze kwa misingi ya utawala bora.
Kwa upande mwingine CCM iendelee kuongoza kwa kufuata misingi iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili. ili AMANI iendelee nchini.