*OFISI YAKE YA MKOA YATIWA KUFULI
*KISA DENI LA SH. 360,000 TU ZA PANGO!
DK, SLAA |
OFISI ya CHADEMA mkoa wa Mbeya, iliyopo eneo la Forest jijini hapa, imefungwa kutokana na Chama hicho kushindwa kulipa sh. 360,000 za deni la pango kwa muda mrefu sasa.
Imeelezwa kwamba mkataba wa awali wa CHADEMA, ulimalizika tangu mwezi Desemba mwaka jana, na jitihada za mmiliki wa chumba hicho, Eden Katininda, za kufuatilia malipo hadi sasa zimegonga mwamba.
Akizungumza leo Katininda amesema kabla ya kuchukua hatua za kufunga kufuli lake juu la lile la lilofungwa na CHADEMA, wiki mbili zilizopita alifanya jitihada kubwa za kudai deni lake bila mafanikio kutokana na uongozi kumpiga chenga.
Katininda alisema hata Katibu mkuu wa CHADEMA, Dk.Willbrod Slaa, alipofanya ziara yake mkoani Mbeya, hivi karibuni alikuwa tayari amefunga ofisi hiyo, na kuwa inaonyesha kiongozi huyo alipokelewa katika ofisi ya wilaya badala ya ile ya mkoa.
Kwa mujibu wa Katininda, aliwasiliana na Mwenyekiti wa chama hicho, mkoani hapa aliyemtaja kwa jina moja la Mwamboneke, wabunge David Silinde (Mbozi Magharibi) na yule wa viti maalum, Naomi Kaihula, lakini wote wamekuwa wanamzungusha.
Aliongeza alipomfuata mbunge Silinde na kumueleza kuhusu madai hayo, alimjibu asihofu kwani mara atakapofika Bungeni mjini Dodoma, atamtumia fedha hizo lakini kila akimpigia huwa hataki kupokea simu yake.
Alisema kwa upande wa mbunge viti maalumu wa CHADEMA, mkoani hapa Naomi, naye alimueleza kuhusu deni hilo, lakini alimjibu kuwa yeye hahusiki hivyo mmiliki (Katininda), awafuate aliowapangisha.
"Baada ya kuona napigwa chenga za mwili kiasi hiki, nilijaribu kuwasiliana na Dk.Slaa kwa simu yake ya mkononi, lakini naye hakupokea simu licha ya kujaribu mara kadhaa, ilikuwa inaita tu mpaka inakatika bila kupokelewa, hivyo ndipo nilipofikia uamuzi wa kufunga kufuli lingine juu ya lile la CHADEMA”, amesema Katininda.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wa chama hicho
Dk. Wiliborod Slaa wakiwa na tajiri Sabodo, mjini Dar es Salaam, hivi karibuni.