Google PlusRSS FeedEmail

DUNIA MZOBORA KUZIKWA MCHANA HUU MAKABURI YA KISUTU, DAR ES SALAAM

DUNIA MZOBORA
DAR ES SALAAM, Tanzania
MHARIRI Mwandamizi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Dunia Mzobora, ambaye amefariki dunia jana, anazikwa leo katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam

Habari zimesema Mzobora (49), ambaye alifariki dunia ghafla jana saa 12 asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa amepelekwa kwa matibabu zaidi, akitokea Hospitali ya Aga Khan pia ya Dar es Salaam, anazikwa leo saa 7 mchana katika makaburi hayo

Mussa, mdogo wa marehemu, alisema jana kuwa Mzobora alianza kujisikia vibaya juzi usiku  nyumbani kwake,Tabata Mawenzi na kupelekwa Aga Khan, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na ndipo alipopelekwa Muhimbili. Alifariki muda mfupi baadaye wakati madaktari wakiwa katika harakati za kuokoa maisha yake.

Mzobora, ambaye hadi anafariki dunia alikuwa Naibu Msanifu Mkuu wa Uhuru, alifanya kazi hadi kumalizika kwa gazeti la Uhuru toleo la jana, akikaimu nafasi ya msanifu mkuu, akiwa buheri wa afya.

Taarifa zilizopatikana jana kutoka kwa ndugu wa familia, zilisema maziko ya marehemu yatafanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mzobora, ambaye alizaliwa Aprili 6, 1964 Mwandiga mkoani Kigoma, alijiunga na Uhuru Publications Limited mwaka 1989, akiwa mwandishi wa habari mwanafunzi, baada ya kumaliza masomo ya ualimu ngazi ya cheti kutoka chuo cha Kasulu, mkoani Kigoma.
Kutokana na uwezo wake na kujituma kazini, mwaka uliofuata alithibitishwa kazini na kupandishwa cheo kuwa mwandishi kamili wa habari.

Mwaka 1992, alipandishwa cheo na kuwa msanifu kurasa wa Mzalendo na Burudani chini ya Msanifu Mkuu wa magazeti hayo kwa wakati huo, Hamisi Mkwinda, kabla ya kupandishwa na kuwa mwandishi wa habari daraja la pili mwaka 1994.

Mwaka 1995, alijiunga na kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa habari cha Nyegezi (sasa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine), Mwanza na kuhitimu stashahada ya juu ya uandishi wa habari mwaka 1998.

Baada ya kurejea kazini, alipandishwa vyeo ngazi mbalimbali kuanzia mwandishi mwandamizi daraja la pili na hadi kufariki dunia kwake, alikuwa Mhariri Daraja la Pili.

Miongoni mwa nyadhifa alizoshika ni pamoja na Kaimu Msanifu Mkuu wa Uhuru, Kaimu Mhariri wa Mzalendo na Kaimu Mhariri wa Makala.

Kutokana na kiu yake ya kupenda elimu, mwaka 2006, Mzobora alijiunga tena na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Mwanza kwa masomo ya shahada ya uzamili katika mawasiliano ya umma na uandishi wa habari. Marehemu ameacha mke na watoto.

Wakati huo huo; Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za pole Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, kufuatia kifo hicho.

“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha mmoja wa Waandishi wa habari shupavu na mchapakazi, Dunia Mzobora aliyekuwa akilitumikia Gazeti la Chama Cha Mapinduzi (CCM) la UHURU,” alisema Rais Kikwete.

Alisema alimfahamu Mzobora, enzi za uhai wake, kama Mwandishi wa Habari aliyejituma katika kazi zake za kuuhabarisha, kuuelimisha na kuuburudisha Umma kwa kutumia vyema kalamu yake.

Katika salam hizo, Rais Kikwete ametoa pole pia kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru na Waandishi wote wa habari nchini, kwa kumpoteza mwenzao waliyekuwa wakifanya naye kazi kila siku.

“Aidha, kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za rambirambi kwa familia ya marehemu Dunia Mzobora kwa kumpoteza baba, kiongozi na mhimili wa familia,” alisema Rais Kikwete.

Amewahakikishia wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba wa mpendwa wao, na anamuomba  Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu, Amina.

Amewataka wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira katika kipindi hiki kigumu wanachopitia baada ya kumpoteza mtu muhimu aliyekuwa kiungo cha familia yao, kwani yote ni mapenzi yake Mola.

This entry was posted in

One Response so far.

  1. Nashindwa cha kuandika, lakini naomba niseme kuwa nimezipokea taarifa za kifo cha DUNIA MZOBORA kwa mshangao mkubwa. Hakina kifo ni kitendawili kikubwa alichokiweka MWENYEZI MUNGU kwetu wanadamu. Nilimfahamu marehemu zaidi pale tulipofanya naye kazi ya kuandaa matini kwa ajili ya toleo maalumu la kumbukumbu ya miaka 14 ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu J.K.Nyerere lililotoka Oktoba 14, 2013

    Nakumbuka mambo mengi tuliyoongea naye. Nakumbuka mipango yange ya kulifanya gazeti la Uhuru kuzidi kupendwa na wasomaji. Nakumbuka jinsi alivyoamini katika kujituma katika utendaji wa kazi na hata kuamini kuwa maisha mazuri yanatokana na kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, na uaminifu.

    Alipotembelea Chuo Cha Mipango kwa ajili ya kukusanya matini ya makala ya toleo hili maalumu alinidokeza " ....haijapata kutokea, lakini safari hii itatokea. Tutatoa gazeti lenye kurasa zaidi ya 120....". Nakweli UHURU likatoka lenye kurasa 136. Ni tukio la kihistoria. Gazeti ambalo limesheheni mambo mengi: taarifa, habari, burudani, nk. Hii inaonesha namna marehemu alivyokuwa mwenye ari ya kuthubutu

    Nakumbuka nilipo mwingiza kwenye kumbi za mihadhara kwa ajili ya kupiga picha wanafunzi wakiwa wanasoma , aliwaasa wasome kwa bidii hadi wafikie ngazi ya shahada. Alisema..." hiyo astashahada mnayosoma iwe mwanzo tu wa kufika mbali. Hakikisheni mnasoma kwa bidii nakufaulu ilimpate sifa ya kusoma stashahada, na kisha shahada...". Aliwatia moyo, wakampigia makofi.... Hakika tasinia ya habari imepata pigo kubwa.

    Napenda kupitia blog hii kutuma salamu zangu za pole kwa mjane wa marehemu, watoto, na ndugu wote kwa msiba huu mzito . Aidha, nawapa pole wafanyakazi wote wa Uhuru Publications Ltd, na wadau wote wa habari hapa nchi kwa msiba huu wa ndugu yetu na jamaa yetu marehemu DUNIA MZOBORA. KIKUBWA TUJIFUNZE KUISHI BILA DUNIA, LAKINI SIKU ZOTE TUMUENZI KWA KUFANYA KAZI KWA BII, UBUNIFU, NIDHAMU, NA UTII BILA KUCHOKA....Sisi tulimpenda sana, lakini Mwenyezi Mungu alimpenda zaidi.... Amina....

    Godrick, Dodoma

Leave a Reply