Google PlusRSS FeedEmail

TFF YAJITOSA NA `PLAN INTERNATIONAL` KUTETEA HAKI ZA MTOTO WA KIKE



DSC_0837 
Rais wa TFF Bw. Jamal Malinzi akiwa na Dida Mushi Golikipa wa timu ya Taifa na Jorgen Holdasen Mkurgenzi mkazi wa Plani International hapa nchini wakiwa wameshika majarida mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF jijini Datr es salaam
...................................................................................
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
NDOA za utotoni zinawazuia mamilioni ya watoto wa kike nchini wasiweze kumaliza shule, kufikia ndoto zao katika maisha na kuwafanya waendelee kuteseka katika umasikini.
Kuna `mijibaba` inayoharibu watoto wa kike bila huruma na kama haitoshi inaamua kufunga ndoa za `kihuni` na watoto ambao ni taifa la kesho.
Serikali na mashiriki binafsi ya kutetea haki za watoto yanapambana dhidi ya tatizo hili, huku wazazi na watu wazima wakiwa sehemu ya tatizo.
Mpira wa miguu ni mchezo unaoongoza kuwa na mashabiki wengi nchini na dunia kote, hivyo mchezo huu unaweza kutumika kama njia ya kupambana na ndoa za utotoni.
Kwa kutambua mchango unaoweza kuletwa na mpira wa miguu, shirikisho la soka Tanzania, TFF limeingia ubia na shirika la kutetea haki za watoto la `Plan International` kwa ajili ya kutetea na kuhamasisha juu ya ulinzi wa haki za mtoto hapa nchini.
Mkataba wa ushirikiano umesainiwa leo katika ofisi za TFF makao makuu jijini Dar es salaam baina ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi na mkurugenzi wa `Plan International Tanzania`, Jorgen Haldorsen . Ushirikiano huo una lengo la kufanya kazi pamoja katika kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni.
Kwa mujibu wa Bw. Haldorsen, soka ndio mchezo unaongoza nchini na duniani kote kuwa na mashabiki wengi na kwamba joto la kombe la dunia linaloendelea kule Brazil na namna watanzania wanavyofuatilia kupitia luninga na wengine wakiwa Brazil ni ushahidi tosha.
“Tunatambua uwezo wa mchezo huu kuwajumuisha watu. Sasa tunataka tuwajumuishe watu sio tu kwa ajili ya furaha, pia kama njia ya kuleta mabadiliko juu ya usawa wa kijinsia kwa kutetea na kuhamasisha juu ya haki za mtoto wa kike”. Alisema Haldorsen.
Mkurugenzi huyo wa `Plan International Tanzania` alidokeza kuwa ushirikiano na TFF ni sehemu ya kampeni ya kimataifa inayoendeshwa na shirika hilo ulimwenguni inayoitwa `Because I Am A Girl`-BIAAG au kwa Kiswahili-KWA SABABU MIMI NI MSICHANA ambapo inalenga kuwatoa mamilioni ya wasichana kutoka katika umaskini kupitia uhamasishaji juu ya haki zao, elimu na stadi za maisha.
“Kwa kupita ubia huu tutakuwa na uwezo wa kuwafikia mamilioni ya Watanzania na tutawapa wasichana ujumbe kuwa KWA SABABI MIMI NI MSICHANA, lazima nipate fursa sawa na wavulana. KWA SABABU MIMI NI MSICHANA, lazima niwe na uwezo wa kufunga magoli kufikia ndoto zangu katika maisha”. Alieleza Bwa.Haldorsen.
Kwa upande wake, Rais wa TFF ambaye ni mjumbe wa kamati ya Huduma kwa jamii ya Shirikisho la mpira wa miguu Ulimwenguni, FIFA, alisema ubia huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za huduma kwa jamii ya TFF na wana furaha kushirikiana na Plan International kwa lengo hili muhimu.
“Ushirikiano huu ni muhimu sana kwetu kwani unakileta chombo kikubwa kabisa cha michezo hapa nchini pamoja na shirika la kutetea haki za watoto (plan International) hususani kwa ajili ya haki za mtoto wa kike. Tunategemea kutumia mtandao wetu nchi nzima kuelimisha juu ya usawa wa kijinsia na uhamasishaji wa haki za mtoto wa kike,” . Alisema Rais Malinzi.
KUHUSU PLAN INTERNATIONAL: Plan International ni shirika la kimaendeleo la misaada ya kibinadamu, linalomlenga mtoto lisilofungamana na mrengo wowote wa kidini, kisiasa au kiserikali.
Plan International ilianzishwa zaidi ya miaka 70 iliyopita na inaendesha shughuli zake katika nchi 70 duniani. Plan International imekuwa inafanyakazi hapa Tanzania tangu mwaka 1991 ikiwasaidia watoto na jamii kupata huduma za afya, elimu, maji, usafi na mazingira, kujikimu na ulinzi. Inaendesha miradi Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Geita, Pwani, Mwanza na Rukwa.
KAMPENI YA KWA SABABU MIMI NI MSICHANA –BIAAG: Kampeni ya Kwa Sababu Mimi ni Msichana-BIAAG (2012-2016) ni kampeni ya Plan ulimwenguni kote inayolenga kuelimisha na kutetea haki za mtoto wa kike na kuwatoa mamilioni ya wasichana kutoka kwenye lindi la umaskini kupitia elimu na utoaji wa stadi za maisha na kazi.
Kampeni hii inalenga kupambana na ubaguzi wa kijinsia na kuboresha maisha ya wasichana milioni 4 duniani na zaidi ya laki 3 hapa Tanzania kwa kuwawezesha kujiunga shuleni, kupata stadi za kiufundi na maisha, kujikimu, na kushiriki katika shughuli mbalimbali katika jamii na kulindwa, kwa kukabiliana na vikwazo dhidi ya maendeleo ya mtoto wa kike.

This entry was posted in

Leave a Reply