Google PlusRSS FeedEmail

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AAGANA NA BALOZI WA KENYA NCHINI TANZANIA, IKULU DAR LEO

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Kenya nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mutiso Mutinda, wakati Balozi huyo alipofika Ofisini kwa Makamu Ikulu jijini Dar es Salaam  Agosti 20, 2013 kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini. Picha na OMR
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Kenya nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mutiso Mutinda, wakati Balozi huyo alipofika Ofisini kwa Makamu Ikulu jijini Dar es Salaam  Agosti 20, 2013 kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini. Kushoto ni Kaimu Balozi wa Kenya, Peter Sang. Picha na OMR
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipokea Kitabu cha Kamusi ya Kiswahili, kutoka kwa balozi wa Kenya nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mutiso Mutinda, wakati Balozi huyo alipofika Ofisini kwa Makamu Ikulu jijini Dar es Salaam  Agosti 20, 2013 kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini. Kushoto ni Kaimu Balozi wa Kenya, Peter Sang. Kitabu hicho kimetungwa na Balozi huyo. Picha na OMR
 

MAKAMU WA RAIS AAGANA NA BALOZI WA KENYA NCHINI TANZANIA
JUMANNE 20, 2013
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal leo ameagana rasmi na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mheshimiwa Balozi Mutiso Mutinda. Shughuli hiyo ya kuagana imefanyika ofisini kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo Balozi Mutiso amemueleza Mheshimiwa Makamu wa Rais kuwa, amefurahi kufikia kikomo cha utumishi wake kama Balozi nchini Tanzania na kwamba siku zote alizokuwa akifanya kazi hapa nchini ziliambatana na furaha kufuatia kuishi katika nchi yenye amani tele na watu wakarimu na wanaoheshimu utu wa watu.

Balozi Mutiso alisema katika kipindi chake hapa Tanzania uhusiano baina ya Kenya na Tanzania umeimarika zaidi na kwamba pale Kenya ilipohitaji msaada wa aina yoyote Tanzania imekuwa rafiki na jirani mwema. “Nashukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais kwa kunipa fursa ya kuja kuagana nawe. Kwa kweli umekuwa kiongozi wa karibu nami na kwamba katika kipindi ambacho nimekuwa Tanzania mengi yamefanyika ambayo yanaashiria kuimarika kwa uhusiano baina ya nchi zetu. Ni wazi kuwa mengi yataendelea kufanyika hata katika kipindi ambachio nitakuwa nje ya hapa,” alisema.

Balozi Mutiso ambaye pia katika kazi nyingine alizofanya amefanikiwa kuandika Kamusi ya Diplomasia, alimkabidhi Kamusi hiyo ambayo imechapishwa na TUKI na kisha kufafanua kuwa, Kamusi hiyo itakuwa chagizo la kuongeza ari ya uzungumzaji wa lugha ya Kiswahili katika nchi za Afrika Mashariki. Kwa upande wake Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal mara baada ya kupiokea Kamusi hiyo alimtaja Balozi Mutiso kama Balozi mfano wa kuigwa kutokana na kutumia nafasi yake vema kuimarisha mahusiano baina ya Kenya na Tanzania.

Mheshimiwa Makamu wa Rais alieleza kuwa, katika kipindi Balozi Mutiso akiwa nchini Kenya imefanikiwa kutanua uwekezaji katika Tanzania na kwamba uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi hizi mbili umeimarika zaidi jambo analotarajia kuwa litazidi kuendelea hata wakati ambapo Balozi Mutiso atakuwa katika majukuimu mengine.
“Nakupongeza kwa kazi nzuri uliyofanya na nakutakia mafanikio zaidi katika majukumu mapya utakayopangiwa,” alisema 
Mheshimiwa Makamu wa Rais huku akimuahidi Balozi Mutiso kuwa kazi nzuri aliyoifanya atahakikisha kuwa inaendelea hasa 
katika eneo la utunzaji mazingira.
 
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais

Ikulu, Dar es Salaam
 

This entry was posted in

Leave a Reply