*Yataka usichukue muda mrefu
* Yataka ubaini pia mazingira ya kuuawa mwandishi huyo.
* Yatoa pole kwa wafiwa, Wanahabari na Watanzania.
CCM imevitaka vyombo na tume zilizoundwa kuhusiana na kifo cha mwandishi wa habari Daudi Mwangosi, vichunguze kwa umakini na weledi mkubwa ili kubaini kila kitu ikiwemo chanzo cha vurugu zilizotokea na mazingira yaliyosabaisha kipigo hadi kufa mwandishi huyo.
Aidha imetaka uchunguzi usichukue muda mrefu ili ukweli kuhusiana na kadhia hiyo ujulikane mapema na hatua zichukuliwe kwa kila atakayebainika kuwa sababu au chanzo cha vurugu na kifo cha mwandishi huyo.
Aidha imesema imepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za kifo hicho na kujeruhiwa kwa askari watatu wa Polisi wakati wa vurugu hizo na kimetoa pole kwa wafiwa, wanahabari wote nchini na wote walioguswa na msiba huo kwa namna moja au nyingine.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye katika taarifa ya CCM kwa vyombo vya habari, leo kuhusiana na sakata la vurugu hadi kifo cha mwandishi huyo, juzi mkoani Iringa.
"Itakumbukwa tarehe Septemba 2, 2012 katika operesheni za CHADEMA mkoani Iringa kulitokea vurugu zilizosababisha kuuawa kwa mwandishi wa habari mzoefu, Daudi Mwangosi na kujeruhiwa vibaya kwa polisi watatu wa kikosi cha kutuliza ghasia. Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za kifo hicho na kujeruhiwa kwa askari hao", Nape alisema katika taarifa hiyo, na kuongeza:
"CCM inachukua nafasi hii kutoa pole kwa wafiwa, wanahabari nchini na wote walioguswa na msiba huu kwa namna moja au nyingine na tunatoa mwito kwa vyombo na tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza swala hili, vichunguze kwa umakini na weledi mkubwa ili kubaini yote - ikiwemo chanzo cha vurugu zilizotokea na mazingira ya kifo cha ndugu yetu".
Alisema CCM inasikitishwa na mfululizo wa matukio ya watu kupoteza maisha au kujeruhiwa katika mikutano na operesheni mbalimbali zinazoendeshwa na CHADEMA nchini hasa zile zilizofanyika kwa kukaidi amri halali za vyombo vya ulinzi na usalama.
Alikumbusha baadhi ya matukio hayo kuwa ni pamoja na lile la kuuawa kwa kada wa CCM Mkoani Singida, kuuawa kwa Ally Hassan mjini Morogoro na la juzi la kuuawa kwa Mwangosi Mjini Iringa, kujeruhiwa kwa askari polisi Iringa na matukio mengine mengi ambayo yametokea wakati CHADEMA wakiendesha operesheni zao mbalimbali nchini.
"Matukio haya si mazuri kutokea kwenye shughuli za Chama cha siasa. Kwakweli ni aibu, inayohitaji uwajibikaji,hata kama ni wa kisiasa. Inapotokea shughuli za chama chako zinasababisha kupotea kwa maisha ya watu kila unapozifanya na bado usitake kuwajibika, inahitaji roho ngumu na ujasiri wa aina yake" alisema
Nape katika taarifa hiyo na kuongeza;
"Inakuwa mbaya zaidi pale vifo hivi vinaposababishwa na Chama hicho kutotii amri halali zilizotolewa kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi inayovipa pia uhalali vyama vya siasa kuwepo na kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria".
"Laiti Chama hicho kingesubiri siku chache zilizobakia kabla ya Sensa kuisha kabla ya kuendelea na mikutano yake ni dhahiri mauaji haya yasingetokea. Lakini kauli za kukebehi na uamuzi wa kukaidi amri ya Jeshi la Polisi na kusema "tupo tayari kwa lolote" ni ishara kwamba Chama hiki kiliandaa na kujiandaa na fujo
zilizotokea", alisema Nape.
CCM imetoa mwito kwa vyama vya siasa na wanasiasa kwa ujumla kujenga utamaduni wa kuheshimu utawala wa sheria na kusema kwamba amani na utulivu vilivyopo nchini ni kazi nzuri iliyojengwa kwa muda mrefu na waasisi wa taifa la Tanzania kwa kujenga utamaduni wa kuzingatia utawala wa sheria.