Google PlusRSS FeedEmail

MCT YAWAPELEKA WABUNGE INDIA

Wabunge saba wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii ya Bunge la Jamhuri ya Muungano pamoja na
Wajumbe wawili wa Baraza la Wawakilishi mmoja kutoka Kamati ya Mifugo, utalii, uwezeshaji na  Habari na mwingine kutoka Kamati ya katiba na Sheria wanaenda India Septemba 23 kwa siara ya siku tano.
Katibu Mtendaji wa  Baraza la Habari Tanzania (MCT) , Kajubi Mukajanga amesema  Baraza limeandaa ziara hiyo kwa lengo la kuwapa fursa Wabunge na Wawakilishi kupata ufahamu wa nchi  inayoendelea yenye sheria ya Haki ya Kupata Habari.
Akizungumza katika mkutano  wa waandishi wa habari katika ofisi za MCT, Mukajanga  alisema ziara hiyo  imo katika mpango kazi  wa mwaka huu wa Baraza la Habari kupeleka kundi la Wabunge  na Wawakilishi katika nchi moja inayoendelea ambayo ina sheria ya Haki ya Kupata Habari.
Sababu ya kuchagua nchi inayoendelea ni kuhakikisha kuwa Wabunge na Wawakilishi wanapata uzoefu katika nchi yenye mazingira na hali inayofanana na nchi yetu, amesema.
Mukajanga amesema kwamba uzoefu wa Baraza la Habari kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano hivi katika mchakato wa kupata sheria ya Haki ya Kupata Habari umeonyesha kuwa kuna wasiwasi kuhusu sheria  hiyo kwamba inaweza kuleta vurugu ama fujo.
Baraza la Habari, alisema Mukajanga,  linataka wabunge ambao ni  watunga sheria, waende wakajifunze, wakaulize  maswali na waelewe umuhimu wa kuwa sheria hiyo.
Aliongeza kuwa ziara hii ya mafunzo kwa Wabunge na Wawakilishi imeandaliwa na MCT kwa  mtazamo kwamba “kuona ni kuamini”.
Msafara huo wa wabunge na wawakilishi utaongozwa na  Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Mheshimiwa Juma Nkamia.
Wabunge wengine katika msafara huo ni:  Rebecca Michael Mngodo, Ramadhani Haji Saleh, Hussein Mussa Mzee, Assumpter Nshunju Mshama, Moza Abeid Saidy na Said Mtanda . Wawakilishi ni  Ali Mzee Ali na Ismail Jussa Ladhu.
Akizungumza katika  mkutano huo, kiongozi wa msafara huo, Nkamia aliipongeza  MCT kwa kuona umuhimu wa kuwaandalia wabunge ziara hiyo ya mafunzo nchini India.
Alisema watatumia watakayojifunza katika  ziara hiyo kufanikisha upatikanaji wa sheria ya haki ya kupata habari nchini.
Wabunge wote waliomo kwenye msafara huo walieleza kwenye mkutano huo kuwa  bila shaka watanufaika na safari hiyo ya mafunzo na watatumia uzoefu watakaoupata kufanikisha kupitishwa sheria  ya haki ya kupata habari.
Wabunge na Wawakilishi hao watafuatana na maofisa watatu wa Baraza la Habari ambapo wawili  John Nguya na Ziada Kilobo wanatoka Dar es Salaam na mmoja, Shifaa Hassan anatoka  Zanzibar.
Miongoni mwa  sehemu watakazotembelea  Wabunge na Wawakilishi ni pamoja na  Ubalozi wa Tanzania mjini New Delhi, Ofisi ya Tume Kuu ya Habari, Ofisi ya Tume ya Habari ya Jimbo,  Kituo Kikuu cha Habari cha Umma, Idara ya Utumishi na Mafunzo na Ofisi ya Taifa ya  Kampeni ya  Haki ya Kupata Habari.
Akijibu  swali kuhusu kwanini wanahabari hawakujumuishwa kwenye msafara huo,  Mukajanga alisema kuwa Baraza  litawaandalia ziara kama hiyo wanahaabari mwakani.
Alifafanua baadaye kuwa  ziara hiyo inaweza kuwa India ama Afrika Kusini.

This entry was posted in

Leave a Reply