*Ukweli wake umewapa matumaini mapya
Nape akihutubia wananchi wa Nyamongo, wilayani Tarime |
Matatizo yaliyokuwa yakiwakabili wananchi waishio katika eneo linalouzunguka mgodi wa Barrick North Mara katika wilaya ya Tarime mkoani Mara, yamepata tiba baada ya kikao cha siku nzima kilichofanywa juzi na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye katika kijiji cha Nyamongo wilayani humo.
Nape alifanya kikao hicho lengo haa likiwa ni kuwasilikiliza wananchi wenye matatizo mbalimbali wilayani humo, kutimiza ahadi iliyotolewa na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, Septemba mwaka huu baada ya kubaini uwepo wa matatizo makubwa yanayowakabili wananchi wa eneo hilo.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkuu wa wilaya ya Tarime, John Henjewele, Wakuu mbalimbali wa Idara katika Halmashauri ya Wilaya hiyo, viongozi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo na wawakilishi wa wananchi.
Wakiwasilisha maelezo na ushahidi juu ya matatizo hayo walisema Mfuko wa elimu kwa ajili ya kusomesha wanafunzi wa sekondari na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu umevurugwa na kwamba kuna haja ya kuwekwa utaratibu mpya wa kuwawezesha wanafunzi hao kulipiwa ada za shule kama ilivyokuwa awali.
Mkazi mmoja wa Nyamongo Daud Makone, akizungumza kwa niaba ya wenzake, alituhumu watendaji wa serikali ngazi ya wilaya hiyo kuwa wamekuwa wakichangia kuvuruga mahusiano mazuri yaliyokuwepo kati ya wananchi na uongozi wa mgodi huo ukiwemo utaratibu uliokuwa ukitumika kulipa ada za wanafunzi waliokuwa wakisomeshwa kwa fedha toka katika mgodi huo.
“Miaka yote tumekuwa tukihamishwa bila kutokea vurugu wala watu kutishwa, tena tunapokea fidia na kuondoka …sasa tangu kuundwa kwa kikosikazi imekuwa kero kubwa, hatua ambayo imefanya kuwepo uhasama mkubwa kati ya jamii na uongozi wa mgodi, kila siku. Tunajiuliza hivi Nyamongo si Tanzania? alihoji Makone.
Naye Mwenyekiti wa kitongoji cha Nyabichune, Kagesa Nyakuranga, alieleza kusitikitishwa kwake na kitendo cha mgodi huo kutoa taarifa za alizosema ni za uongo serikalini kuhusu miradi inayotekelezwa katika vijiji vya eneo hilo, taarifa ambazo alidai zimejenga chuki na kutoaminiana kwa pande hizo.
“Mgodi umekuwa ukileta viongozi wa kitaifa na kuwapa taarifa za uongo kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo wakati wakijua si kweli wanachokisema. Kwa mfano wameomba kuhamisha shule zetu za msingi za Matare na Nyangoto, kupisha shughuli za mgodi na kukubali kutujengea mpya, sasa leo wanadanganya viongozi wa kitaifa eti wametujengea shule mpya wakati wamefidia shule zetu” alisema kiongozi huyo.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Nape Nnauye, alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) haitakubali kamwe kuendelea kwa uhasama katika eneo hilo huku wananchi wakikosa haki zao kutokana na tamaa za baadhi ya viongozi.
“Nimesema nakwenda kukutana na TAMISEMI ili watume watu wao kuja kuchunguza, tukibaini yeyote aliyehusika tutamchulia hatua kali zikiwemo za kisheria bila kujali yeye ni nani. Hatuwezi kuendelea kwa uonevu huu”, alisema Nape.
Wakati hatua hizo zikichukuliwa, aliwagiza viongozi wa vijiji waanze mapema iwezekanavyo mchakato wa kuanzisha upya mfuko huo na baada ya ngazi hiyo kukamilisha kazi hiyo ipelekwe kwenye baraza la madiwani kwa ajili ya kupata baraka zake ili mfuko huo uweze kuanza mara moja katika eneo hilo.
Nape aliongeza kuwa CCM haiwezi kupinga uwekezaji, bali uwekezaji huo unapaswa kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini, lakini uwekezaji huo utoe haki kwa pande zote ili kuweza kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima.
Kuhusu kikosikazi kilichoundwa na serikali kwa ajili ya kushughulikia migogoro katika eneo hilo la Nyamongo, ambacho kimelalamikiwa na wananchi kwa kushindwa kutenda haki kwa wananchi, Nape aliwaahidi wananchi hao kulifikisha suala hilo kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kuona namna bora ya kuundwa kwa kikosi kazi kitakachokuwa na tija kwa pande zote.
Akizungumzia maji yanayodaiwa kuwa na sumu ambayo yanadaiwa kumwagwa kutoka mgodini kwenda katika vyanzo vya maji na mto Mara, Nape ambaye awali alijionea hali hiyo alisema ingawa si mtalaam wa maji lakini ukweli umeonesha kuwa maji hayo si salama pia ni hatari kwa matumizi ya binadamu.
Nape (aliyeshika shavu) akiwasilikiza kwa makini wananchi wa Nyamongo wakati wakitoa malalamiko yao.