CCM TAWI LA UINGEREZA WAADHIMISHA MIAKA 50 YA MUUNGANO
Apr 25, 2014
CHAMA CHA MAPINDUZI - TAWI LA UINGEREZA – UNITED KINGDOM
Website: ccmuk.org, Blog: ccmuk.org/blog, Facebook page: chama cha mapinduzi uingereza, twitter: CCMUK 1, Contacts Phone +44 74 04 863333, +44 7545 213515. E-mail – itikadi-uenezi@ccmuk.org
Uongozi na Wanachama wote wa Chama cha Mapinduzi Tawi la Uingereza (UNITED KINGDOM) pamoja Watanzania wanaoishi nchini Uingereza kwa pamoja wanajumuika na Watanzania wote katika Kuadhimisha kilele cha sherehe za miaka hamsini (50) ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitazofanyika Tarehe 26 Aprili, 2014 katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, na pia kuwaombea shamrashamra za amani na Utulivu katika Mkesha wa Miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utakaofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja Tanzania Bara na Viwanja vya Maisara, Zanzibar kuanzia saa 4:00 usiku wa tarehe 25 April 2014.
Vile vile Mwenyekiti wa CCM UK anayemaliza muda wake Ndugu Maina A Owino anapenda kutoa shukrani za kipekee kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. JAKAYA KIKWETE kwa kuonyesha weledi mkubwa katika kuulinda na kuutetea Muungano wetu wenye manufaa makubwa kwa Watanzania toka pande zote mbili.
Chama cha Mapinduzi Uingereza, Viongozi, wanachama wote na watanzania kwa ujumla hapa UK wanasisitiza Kanuni za Msingi za Muungano wa mwaka 1964 zinaonyesha dhahiri chimbuko la Muungano , pamoja na mambo mengine linajumuisha uhusiano wa karibu wa muda mrefu kati ya watu wa Tanganyika na Zanzibar, uhusiano wa kisiasa uliotokana na harakati za kupigania uhuru zinazofanana na imani ya pamoja ya Uhuru wa Afrika yote. Ni Muungano pekee unaodumu Leo hii kwenye Bara la Afrika kwa kuwezekana kuunganga kwa mataifa mawili huru yanayojitawala. Tukio hili limeonyesha kwamba kuwa na dhamira ya dhati na kuwa na ari na moyo kwa watu wa Afrika na viongozi wao, inawezekana kuwa na umoja wa Afrika. Imedhihirika kuwa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ndiyo umoja pekee ambao bado unaendelea kudumu na kuwa ni wa kipekee sana na wenye kuleta hamasa ya nchi mbali mbali duniani kote kutaka kujifunza kutoka katika Muungano wetu.
Kitendo cha Waasisi wetu kukubaliana na kubadilishana Kanuni zenye misingi ya Muungano ndiyo nguzo kuu ambayo Taifa letu linapasa kuilinda na kujivunia pamoja na changamoto mbalimbali zinazotukabili, kuchanganya udongo wa Tanganyika na ule wa kutoka Zanzibar inaonyesha ni kiasi undugu wetu ulivyo wa karibu na wenye mahusiano ya damu moja ya KITANZANIA.
Katika kipindi hiki cha mchakato wa Katiba Watanzania tusikubali kugawika kutokana na propaganda za kisiasa na watu wachache zenye kujenga chuki miongoni mwetu katika pande hizi mbili za Muungano.
Muungano ni wa kwetu na wala siyo wa wanasiasa au makundi machache yenye dhamira na malengo yao binafsi; hivyo tunawaomba Watanzania wenzetu tujikite katika kutoa michango na mawazo yenye mashiko yatakayoboresha zaidi Muungano wetu wenye manufaa mengi miongoni mwetu toka pande zote mbili.
TUDUMISHE MUUNGANO WETU WA KIPEKEE DUNIANI
MUNGU IBARIKI JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Imetolewa na Abraham Sangiwa – Idara ya Itikadi, Siasa na Uenezi
CHAMA CHA MAPINDUZI TAWI LA UINGEREZA – UNITED KINGDOM
Tarehe 24/04/2014.