Google PlusRSS FeedEmail

CHADEMA: KIKWETE NI JEMBE KATIKA MAENDELEO

*KIKWETE NAYE AWATAKA VIONGOZI WASITUMIE WANANCHI KAMA CHAMBO KUTIMIZA TAMAA ZAO ZA KISIASA.

KARATU, Tanzania
CHADEMA wamemshukuru Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kwa kusaidia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Wilaya ya Karatu katika Mkoa wa Arusha.

Chama hicho kimempongeza Rais Kikwete kwa kusambaza maendeleo kwa Watanzania wote bila kujali msimamo wao wa kisiasa na hata katika maeneo yanayounga mkono upinzani.

Shukurani na pongezi hizo zimetolewa mchana wa leo, Jumanne, Aprili 22, 2014 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Lazaro Titus Massey wakati wa sherehe za uzinduzi wa jengo la Halmashauri hiyo mjini Karatu. Halmashauri hiyo inaongozwa na CHADEMA.

“Ni lazima tutoe shukurani nyingi kwako Mheshimiwa Rais kwa sababu bila wewe kuwa Rais wa Tanzania sisi Karatu tusingepata jengo hili. Pamoja na kwamba Halmashauri yetu ni CHADEMA bado umeamua kuchangia sana maendeleo ya Wilaya yetu kwa kuchangia kiasi kikubwa ujenzi wa jengo hili. Sisi hata robo ya fedha za ujenzi huu hatukuweza kuzitoa,” amesema Mheshimiwa Massey huko akishangiliwa na wananchi.

Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Karatu limegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.412 na kati ya hizo, Serikali imetoa shilingi bilioni 1.394 na Halmashauri imechangia shilingi milioni 18 tu.

Akizungumza baada ya kumsikiliza Mheshimiwa Massey, Rais Kikwete amesema kuwa ni sera ya Serikali yake kusambaza maendeleo kwa Watanzania wote bila kujali misimamo yao ya kisiasa wala kuongozwa na hisia nyingine mbali na ukweli kuwa kila Mtanzania anataka na anayo haki ya kupata maendeleo.

“Sisi hatuna wasiwasi, wananchi wa Karatu wamechagua CHADEMA lakini chama hiki hakina Serikali. Wananchi wamechagua chama bila Serikali. Halmashauri mnayo lakini Serikali tunayo sisi. Katika kusambaza maendeleo, sisi hatuwezi kubagua. Hiyo ndiyo demokrasia na Serikali yetu inaheshimu sana demokrasia na misingi ya utawala bora,” amesema Rais Kikwete.

Wakizungumza baadaye kwenye mkutano wa hadhara wabunge wote wawili wa CHADEMA, waheshimiwa Cecilia Paleso na Israel Nanse wamerudia tena kumpogeza Rais Kikwete kwa kusambaza maendeleo katika maeneo yote ya Tanzania yakiwemo yaliyoko chini ya wapinzani.

“Chini ya uongozi wako, maendeleo yamesambazwa na sisi Karatu tumenufaika sana.  Ni matumaini yetu kuwa chini yako, tutaendelea kunufaika na sera zako sahihi,”amesema Mheshimiwa Paleso.

Naye Mheshimiwa Nanse amesema: “Mheshimiwa Rais sisi kwetu hapa hatuna ugomvi kati ya vyama vya siasa. Siye CHADEMA tunajua kuwa CCM ni chama tawala Tanzania na CHADEMA ni chama kiongozi hapa kwetu Karatu. Ni uhusiano huu uliowezesha Karatu kuendelea kupata maendeleo.”

“Tunakushukuru na kukupongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuifungua nchi yetu kwa barabara kila mahali. Aidha, sisi wana-Karatu tunakushukuru sana kwa mradi wa maji ambao umeuzindua leo”. Tunakushukuru sana.

Rais Kikwete alikuwa katika ziara ya siku moja wilayani Karatu, Mkoa wa Arusha na kesho atafanya ziara ya Wilaya ya Mwanga katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Wakati huohuo, Rais Kikwete amewataka viongozi nchini kuacha kuwatumia wananchi kama chambo cha kufanikisha malengo yao ya kisiasa na kusababisha migororo na uvunjifu wa amani.

Rais amewataka wananchi wa Wilaya ya Karatu wasiige mfano wa Arusha ambako fujo zinazoongozwa na baadhi ya viongozi zimezorotesha sana uchumi wa mji huo kwa sababu usalama ni kigezo kikuu cha maendeleo ya uchumi.

Akizungumza wakati anazindua Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha, mjini Karatu asubuhi ya leo, Jumanne, Aprili 22, 2014, Rais Kikwete amesema:
“Usalama ni jambo muhimu sana na kwa maana hiyo, nawaombeni msiige kabisa mfano wa Arusha, sote tunajua kimetokea nini kule kwa sababu ya fujo za kisiasa ambazo zinachochewa na viongozi na hasa Mbunge wa Arusha mjini Bwana Lema,”.

“Mbunge anayo nafasi kubwa kujenga hoja zake ndani ya Bunge na ndani ya mikutano ya halmashauri. Lakini kwa mbunge kuwachochea wananchi na kuwachukua na kuwatembeza barabarani ambako wanakumbana na virugu vya polisi siyo uongozi wa busara hata kidogo.” Alisema Rais Kikwete.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Lazaro Titus Massey amewaambia wananchi kuwa moja ya mwelekeo mkuu wa CHADEMA wilayani Karatu ni kushirikiana na Serikali na polisi katika kudumisha amani.

"Tunawakaribisha Arusha waje kujifunza kwetu namna ya kudumisha amani. Tunamkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Bwana John Mongella kuja kujifunza namna ya kurejesha na kudumisha amani mjini humo", alisema

This entry was posted in

Leave a Reply