Google PlusRSS FeedEmail

SHIVJI: SIFUATI MATAKWA YA WANASIASA

  • Awashangaa  Lissu, Jussa kujilinganisha naye
  • Wasomi wawaita wanasiasa wapiga kelele
DAR ES SALAAM, Tanzania
MWANAZUONI mashuhuri nchini, Profesa Issa Shivji (pichani), amesema hafanyi uchambuzi kwa ajili ya matakwa ya wanasiasa na kwamba, alichokizungumza kuhusu muundo wa serikali mbili ndio msimamo wake kwa siku nyingi.

Amesema hawezi kujibizana na wanasiasa kwa kuwa kuna wengine walikuwa hawajazaliwa kipindi akifanya utafiti na uchambuzi hasa katika suala zima la Muungano.


Shivji alisema hayo jana katika mahojiano na UHURU, ambapo alisema yeye ni msomi na mwanazuoni na amekuwa akifanya tafiti na chambuzi zake nyingi zipo kwa ajili ya jamii na si wanasiasa wanaopiga kelele.
“Nisingependa kuwajibu, lakini sifanyi tafiti au chambuzi kwa ajili ya wanasiasa. Nimeandika mambo mengi juu ya Muungano kwa zaidi ya miaka 40 na nina hakika wengine walikuwa bado hawajazaliwa, nawataka wasome vizuri na watambue msimamo wangu ni upi,’’ alisema Profesa Shivji.
Alisema alichokisema kuhusiana na hotuba yake, kimetokana na maandishi aliyoyatoa kama utafiti na uchambuzi wake, toka mwaka 1983 na amekuwa akiufanya kwa ajili ya jamii na si wanasiasa.

Hivyo, alisema asingependa kuzungumza zaidi kuhusiana na suala hilo na kuwataka wale wote wanaotoa kauli dhidi yake, waende kusoma maandiko yake juu ya Muungano na watapata msimamo wake.


Kauli ya Shivji imetokana na  taarifa iliyotolewa juzi na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wakimwemo Tundu Lissu na Ismail Jussa mjini Dodoma kuwa, Profesa Shivji anatumia jina lake kuwapotosha watanzania.
Viongozi hao, walizungumza huku wakiwa wameshika moja ya kitabu chake ambapo walidai Profesa Shivji amezungumza hivyo kwa madai amenunuliwa na serikali katika kuipigia chapuo serikali mbili na si tatu.


Kauli ya UKAWA ilitokana na hotuba aliyoitoa Profesa Shivji katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam katika kongamano la vijana, ambapo alisema taarifa ya mwisho ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba inaweza ikawa na hatari.


Alisema hilo linatokana na kuamsha na kushawishi hisia za Utanganyika, na, pili, kufanya watu wa Tanzania  Bara wawachukie wenzao wa Zanzibar. Kwa hivyo, inahatarisha muungano badala ya kuuimarisha.
“Muungano wowote hauwezi kudumu, au kudumu kwa amani, kama hauna mizizi katika watu na hisia zao na sisemi kwamba muundo wa serikali au dola mbili tulionao hauna matatizo, unayo. Lakini tusiangalie muungano kwa jicho la idadi ya serikali. Tuuangalie kwa mtazamo wa demokrasia. Na tukifanya hivyo tunaweza kubuni muundo ambao utakidhi mahitaji yetu bila kuhatarisha uhai wa muungano,’’ alisema Profesa Shivji katika kongamano hilo.
WASOMI WAWAPONDA UKAWA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alisema kamwe hawezi kuingia katika malumbano ya UKAWA na Profesa Shivji kwa kuwa ni watu tofauti na wenye upeo tofauti wa mambo.
“Profesa Shivji ni msomi na mwanazuoni, wale ni wanasiasa, kuna tofauti kubwa hapa, ningependa niwaombe UKAWA wasome zaidi alichokisema profesa na wakitafakari kisomi na si kiushabiki au kisiasa,’’ alisema.
Naye, Dk. Benson Bana alisema amepata bahati ya kusoma vitabu vingi vya Profesa Shivji na yupo sahihi na kinachofanyika sasa ni uanaharakati kutoka kwa kikundi cha UKAWA na si kujibu hoja kwa umakini.
“Profesa Shivji yupo sahihi na ameangalia maslahi ya watanzania. UKAWA wanapaswa kutambua hisia za Utanganyika na Uzanzibar hazitotusaidia na zitaua Muungano. Tunaweza kuuvunja, lakini wananchi watambue wanasiasa nao ni wanafiki,’’ alisema.
Dk. Bana alisema mtu anapopata wasaa wa kutafakari zaidi juu ya serikali tatu, ataona kuna hatari kubwa inayokuja mbeleni kama ikipita na kinachofanyika ni uharaka wa kutaka mabadiliko hasa ya muundo wa Muungano na si kutafuta suluhisho la tatizo.
“UKAWA watulie na wasome vyema maandishi ya Shivji, wataelewa wanachofanya wanakurupuka, ingawa naamini ni siasa za uanaharakati. Mtu mwenye busara anawaangalia na waendelee kumshambulia wanavyotaka, lakini ningependa wasome maandishi yake ndipo wazungumze,’’ alisema.

This entry was posted in

Leave a Reply