Hakim Nyangoha akipataiwa matibabu hospitalini |
HAKIMU wa mahakama ya mwanzo katika manispaa ya Shinyanga Satto Nyangoha amejeruhiwa kwa kuchomwa kisu na mlalamikaji wa kesi ya wizi wa baskeli Emmanuel Izengo (28) mkazi wa Tambukareli.
Tukio hilo limetokea jana saa 8:00 mchana katika mahakama hiyo baada ya hakimu huyo kutoa hukumu hiyo ambayo ilikuwa imefunguliwa tarehe 1/8/2013, mlalamikaji akiwa ni Izengo ambaye ni aliibiwa baiskeli aina ya Neria yenye thamani ya Sh. 150,000.
Hakimu Nyangoha alitoa hukumu hiyo, iliyofunguliwa 1/8/201, huku mshitakiwa wa wizi huo wa basikeli, Daniel Makelezia mkazi wa Lubaga akiwa hayupo mahakamani kutokana na kuingia mitini tangu alipopewa dhamana Agosti 23, 2013.
Hata hivyo baada ya kuendelea kesi hiyo mshtakiwa na mdhamini wake hawakuhudhulia mahakamani hapo mara mbili huku mlalamikaji akiendelea kuhudhulia.
Kufuatia hali hiyo hakimu Nyangoha aliamua kutoa hukumu ya kifungo cha miaka miwili jela, adhabu ambapo mshitakiwa atatakiwa kuanza kuitumia mara atakapopatikana.
Imeelezwa kwamba baada ya hakimu Nyangoha kutoa hukumu hiyo mlalamikaji alitoa shukrani kwa kuwapa mikono watu waliokuwemo mahakamani kisha akatoka nje.
Habari zinasema, baada ya dakika 15, mlalamikaji Zengo, alirudi mahakamani na kwenda kwa hakimu akidai kwenda kumpelekea stakabadhi ya manunuzi ya beiskeli ili kumuonyesha thamani halisi.
"Alipoingia ndani ndipo kelele zikaanza kusikika kutoka kwa mshauri wa Baraza katika mahakama hiyo, Mary Wamba akisema njooni jamani hakimu amevamiwa, anapigwa” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.
Inaelezwa kwamba watu walipofika katika ofisi ya mahaka hiyo walikuta hakimu akivuja damu nyingi huku mlalamikaji huyo ambaye sasa amekuwa mtuhumiwa, akiendelea kumshambulia kwa kumchoma kisu hadi kumjeruhi kwenye shavu la kushoto. Source GAZETI LA UHURU