*Awataka kutoa michango ya maendeleo kwa jamii inayowazunguka
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amewataka wawekezaji nchi kujenga tabia ya kutoa michango ya maendeleo kwenye maeneo ambayo wamewekeza na si kutoa michango ili kumfurahisha Rais au Waziri Mkuu.
Kinana alitoa kauli hiyo jana katika Kijiji cha Mwendakulima katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara yake ambayo itakuwa kwa Mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara ambapo akiwa eneo hilo alizungumzia umuhimu wa wawezaji kujitahidi kufanya maendeleo kwa wananchi ambao wamewekeza kwenye maeneo yao.
“Wawekezaji wapo tayari kutoa hadi sh.milioni 200 wakiwa Dar es Salaam, Mwanza au Arusha, lakini ushauri wangu kwao, ni vema wakachangia kwenye maeneo ambayo wamewekeza kwani hiyo itasaidia kuondoa malalamiko lakini pia itakuwa ni jambo jema wananchi kunufaika kutokana na uwekezaji huo.
Alisisitiza kuwa anatambua umuhimu wa wawekezaji kuchangia maendeleo lakini inapendeza zaidi inapofika mahali wananchi wakawa na maendeleo kutokana na wawekezaji.
Kinana alifafanua hayo zaidi wakati akizindua kituo cha afya kwenye kijiji hicho ambacho kimejengwa na kampuni ya madini ya Buzwagyi ambapo alisema kampuni hiyo imeanza na eneo la afya lakini mwaka mwingine wanaweza kujenga miundombinu ya barabara na mwaka unaofuata kufanya jambo lingine la maendeleo.
Wakati huo huo Katibu Mkuu huyo , alisema kuwa Watanzania wanatakiwa kushiriki kikamilifu kwenye mchakato wa Katiba mpya na kwamba msimamo wa chama chake ni Serikali mbili lakini wapo tayari kwa uamuzi ambao utafanywa na wananchi kwa kuamua aina ya katiba ambayo wanahitaji.
Pia alisema wananchi wafahamu kuwa licha ya umuhimu wa kuwa na Katiba mpya lakini hiyo haitakuwa mbadala wa kuwa na mabadiliko ya maisha baada ya kupatikana kwake ambapo alitoa mifano ya nchi kadhaa Afrika na Asia ambazo zilipata katiba mpya lakini hali ya uchumi kwa watu wake imebaki kuwa ile ile.
Akifafanua kuhusu msimamo wa CCM wa kutaka muundo wa Serikali mbili, Kinana alisema hakuna sababu ya kuwa na Serikali ya tatu kwani kuwanayo ni kuongeza mizigo kwa Mtanzania kwani ni gharama kuindesha kwake lakini pia haitakuwa na kazi.
Pia Kinana akiwa Kahama alizindua Saccos ya Mkombozi katika eneo la Isaka ambapo alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kubuni miradi ya maendeleo lakini pia kwa vijana kujiendeleza kielimu hasa kusoma masomo ya ufundi yakiwamo ya ujenzi, ufundi mchundo na aina nyingine nyingine ya taaluma ya ufundi ambayo itawawezesha kupaa kipato.
Katika kuhakikisha hilo la masomo ya ufundi linafanikiwa,Kinana aliweza kutoa ahadi ya kusomesha vijana 10 wa eneo la Kahama na kwamba kama gharama itakuwa nafuu ataongeza idadi ya vijana ikiwa ni sehemu ya kufanikisha malengo ya vijana.
Wakati huo huo akiwa katika Uwanja wa CDT Kinana aliwataka Watanzania kuwa makini na wapinzani kwani nia yao si kuwaisaidia Watanzania bali n kutafuta maslahi yao na ndio maana wapo tayari kufanya lolote kufanikisha kile wanachokitaka.
Katibu Mkuu wa CCM Taifa Abdulrahman Kinana akikata utepe kuashiria kukamilika kwa awamu ya kwanza ya jengo la kituo cha afya cha kijiji cha Mwendakulima ambalo limedhaminiwa na Mgodi wa Buzwagi.