Google PlusRSS FeedEmail

DK BILAL AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UHURU WA UGANDA

NA MWANDISHI WETU, UGANDA

Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika kuadhimisha sikukuu ya miaka 50 ya uhuru wa Uganda.  Taarifa iliyotlolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais, leo imesema.

Uganda ilipata uhuru wake Oktoba 09, mwaka 1962 na jana Jumanne 09 Oktoba, 2012 iliadhimisha miaka 50 ya uhuru huo katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Mapinduzi wa Kololo na kuhudhuriwa na Mwenyeji wa Sherehe hizo Rais Yoweri Kaguta Museveni. 

Sherehe hizo za aina yake zilipambwa na vikosi mbalimbali vya kijeshi vilivyopita mbele ya Amiri Jeshi Mkuu Rais Museveni na kutoa heshima zao za utii kwa kiongozi huyo, sambamba na vikundi mbalimbali vya burudani ambavyo vilitumbuiza wakati wote wa sherehe, huku wananchi mbalimbali wa Uganda ambao hawakupata nafasi ya kufika katika uwanja wa Kololo wakitazama tukio hilo la kihistoria kupitia televisheni mbalimbali. Sambamba na hilo pia vyombo mbalimbali vya kiusalama nchini hapa, vilikuwa vikitumia kila aina ya taarifa sambamba na kuzunguka eneo la maadhimisho wakati wote ili kuhakikisha kuwa sherehe hizi zinafanyika na kumalizika kwa usalama kama ambavyo imetokea. 

Pamoja na Makamu wa Rais Dkt. Bilal pia kulikuwa na viongozi wafuatao: Rais Mwai Kibaki wa Kenya, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Pierre Nkurunzinza wa Burundi, Rais Salva Kiir wa Sudan ya Kusini, Rais Seretse Ian Khama wa Botswana, Rais wa Afrika ya Kati, Rais Ahmad Muhamad wa Somalia, Rais Mursi Mohamed wa Misri, Rais Boni Yayi wa Benin, Rais Mugabe wa Zimbabwe, Rais Joseph Kabila wa Congo (DRC), Makamu wa Rais wa Sudan, Makamu wa Rais Alhaji Namadi Tsambo wa Nigeria, Mtukufu Agha Khan, Prince Edward na wengine wengi. 

Sherehe hizi ziliongozwa kwa lugha tatu kwanza Kiswahili ambacho kilitumika kutoa amri kwa vikosi vya majeshi na hii inadhihirisha wazi kuwa lugha hii imejikita zaidi miongoni kwa wanajeshi hapa Uganda, lugha ya Kiganda na Kiingereza. Vyombo vya habari mbalimbali vya hapa vimeelezea kuwa tukio hili la kuadhimisha miaka 50 ya uhuru, ni moja ya matukio makubwa kabisa ambayo yametokea Uganda na ambayo yameonesha kuwa taifa hili lina kila sababu ya kuunganisha nguvu zake na kubakia taifa moja tofauti na sasa ambapo kuna hali kadhaa za kusigana miongoni mwa wananchi hali inayofanya kukosekana kwa utulivu wa moja kwa moja.

Tofauti na ilivyozoeleka ambapo Amiri Jeshi Mkuu Rais Yoweri Museveni huzoea kukagua vikosi vya majeshi kwa kutembea, safari hii alifanya hivyo akiwa ndani ya gari maalum kwa ajili ya shughuli hiyo, huku watangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Taifa (UBC) wakielezea kuwa hali hiyo ni kuonesha namna Uganda ilivyoendelea. Baada ya zoezi hilo la ukaguzi kama ilivyo ada ilifuata zoezi la vikosi kutoa heshima na na utii na kisha Rais Museveni akapata wasaa wa kuhutubia wananchi sambamba na wageni waliofika katika hafla hii kubwa. Katika hotuba yake aliwakumbusha wananchi kuhusu Uganda ilipotoka na dira yake katika miaka mingine ijayo. Pia aliwasisitiza wananchi wa Uganda kutambua fursa mbalimbali zilizopo hasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na akaelezea nia ya Uganda kuzidi kudumisha ushirikiano na nchi jirani sambamba na nchi rafiki wa Uganda. 

Msafara wa Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Tanzania sambamba na kuwepo kwa Mama Zakhia Bilal pia uliambatana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa SMZ, Ali Juma Shamhuna, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Omar Juma Mahadhi, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Rashid Ali Abdalla sambamba na viongozi na maafisa wengine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ofisi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais. Katika taarifa yake kuhusu sherehe hizi, Mheshimiwa Makamu wa Rais alielezea kufurahishwa kwake na nanma sherehe hizo zilivyofanyika huku akifafanua kuwa, Watanzania wanayo nafasi kubwa ya kuinua uchumi wao kama nguvu itaongezeka katika kuboresha uhusiano kati ya Tanzania na Uganda hasa katika sekta za elimu na biashara. Pia alifafanua kuwa, Tanzania inaipongeza Uganda kwa kufanikiwa kutimiza miaka 50 ya uhuru na akaitaka Uganda kuhakikisha inadumisha amani, inatokomeza matabaka na pia inahakikisha kuwa vita kati nchi hii vinatokomezwa ili nchi nzima ya Uganda ibakie moja hali itakayosaidia kufanya Jumuiya ya Afrika Mashariki kubakia moja na yenye amani na utulivu. 

Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na ujumbe wake unarejea leo jijini Dar es Salaam, tayari kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais na viongozi waliomabatana naye kuendelea na shughuli nyingine za ujenzi wa Taifa la Tanzania.

This entry was posted in

Leave a Reply