Google PlusRSS FeedEmail

UCHAGUZI MKUU CCM NOV.11


Katibu wa NEC,Itikadi na Uenezi ,Nape Nnauye akiongea na waandishi wa habari,ofisi ndogo za CCM Lumumba,Dar es salaam.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

                        MKUTANO MKUU WA CCM 2012

Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika tarehe 13/10/2012 pamoja na mambo mengine kilipanga ratiba ya Mkutano Mkuu wa Taifa iwe kama ifuatavyo:-

1.           Mkutano Mkuu wa Nane wa Kawaida wa CCM utafanyika tarehe 10 – 12 Novemba, 2012 .  Kwa kawaida Mikutano Mikuu ya CCM imekuwa ikifanyika kwa siku mbili.  Lakini safari hii CCM imeamua mkutano huo uwe wa siku tatu ili kutoa fursa kwa Wajumbe kujadili kwa kina taarifa muhimu zitakazowasilishwa.

2.           Mkutano huo utafanyikia KIZOTA – Dodomamahali ulipofanyika Mkutano Mkuu uliopita mwaka 2010.

3.           Shughuli muhimu zitakazofanywa wakati wa Mkutano huo zitakuwa:-

(1)                Kufanya marekebisho ya Katiba ya CCM ya 1977 toleo la 2010 kwa kuzingatia mapendekezo ya Halmashauri Kuu ya Taifa yatakayowasilishwa kwenye Mkutano huo.

(2)                Kupokea na kujadili taarifa mbalimbali zikihusu:-

(i)                  Taarifa ya Kazi za Chama kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2007-2012 itakayowasilishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.

(ii)                 Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

4.           Shughuli za Uchaguzi ambazo zitahusu Uchaguzi wa:-

(i)                  Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Viti Kumi vya Bara na kumi vya Zanzibar.
(ii)                 Mwenyekiti wa CCM.
(iii)                Makamu wawili wa Mwenyekiti mmoja kutoka Bara na mwingine kutoka Zanzibar.

Shughuli za Mkutano Mkuu zitatanguliwa na kuweka Jiwe la Msingi la Majengo ya Ukumbi wa Mikutano na Makao Makuu ya CCM eneo la Medelii katika Manispaa ya Dodoma.  Shughuli hii itafanywa na Mwenyekiti wa CCM Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete.

MAANDALIZI YA MKUTANO

Shughuli za Maandalizi ya Mkutano zinaendelea vizuri.  Shughuli hizi ni pamoja na uchapaji wa Nyaraka mbalimbali; usafiri wa Wajumbe, Maandalizi ya Ukumbi na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya kufanikisha Mkutano huo.

VURUGU ZILIZOTOKEA MBAGALA

Chama cha Mapinduzi kimesikitishwa na matukio yaliyotokea Mbagala, jijini Dar es Salaam, tarehe 11 Oktoba 2012. Chama Cha Mapinduzi kinalaani kitendo cha kukojolewa kwa kitabu kitakatifu cha dini ya Kiislam, yaani Kuran. Vilevile, Chama cha Mapinduzi kinalaani vitendo vya vurugu na kuvamiwa na kuchomwa moto makanisa.

Vitendo vyote hivi havifanani na mila na desturi za Watanzania. Kitendo cha kukojolea kitabu kitakatifu cha Waislamu hakikubaliki. Na kitendo cha kuvamia na kuchoma moto nyumba za ibada za Wakristo na kufanya vurugu pia hakikubaliki. Tanzania ni nchi inayofahamika na kusifika kwa amani na utulivu na kwa umoja na mshikamano wa watu wake wa kabila, rangi na dini zote. Chama Cha Mapinduzi kinawasihi wananchi wawe na subira na uvumilivu yanapotokea matukio kama haya na waviachie vyombo vya dola vifanye kazi yake.

Ni imani ya CCM kwamba vyombo vya dola vitachukua hatua stahiki kwa wote waliohusika na matukio haya. Pia, tunatumaini kwamba hali ya amani na utulivu itarejea Mbagala kamakawaida.

UTEUZI WA MAJINA YA WAGOMBEA NAFASI MBALIMBALI
MKOANI KILIMANJARO

Kamati Kuu pia imefanya uteuzi wa mwisho wa majina ya Wanachama wa CCM walioomba nafasi za Uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi katika nafasi za Uenyekiti wa CCM Wilaya na Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nafasi ya Wilaya za Siha na Moshi Vijijini.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM; uteuzi wa mwisho wa nafasi hizi hufanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa, lakini Kikao cha tarehe 25/9/2012 kilichofanyika Mjini Dodoma hakikufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi hizi katika Wilaya za Siha na Moshi Vijijini. Hivyo, Kikao hicho kilikasimu madaraka yake ya uteuzi kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

Nafasi za Uongozi zinazogombewa na majina ya walioteuliwa ni kama ifuatavyo:-

(1)    Nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini

Waliojitokeza kugombea nafasi hii ni 13.  Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-

        (a)    Ndugu Shayo Isack EDWARD
        (b)    Ndugu Masenga John GABRIEL
        (c)    Ndugu Shao C. GEOFREY
        (d)    Ndugu Mallya Mathew MARTIN

(2)    Nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Siha

Waliojitokeza kugombea nafasi hii ni wanne (4).  Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-

        (a)    Ndugu Tawida Nahato BASSO
        (b)    Ndugu Simon Lekshon MOLLEL
        (c)    Ndugu Happiness Mathias MUNUO
        (d)    Ndugu Oscar Jeremiah TEMI

(3)    Nafasi ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Wilaya ya Siha

Waliojitokeza kugombea nafasi hii ni saba (7).  Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-

        (a)    Ndugu Meijo Loloinyo LAIZER
        (b)    Ndugu Joha Shabani  MTAWAZO
        (c)    Ndugu Happiness Mathias MUNUO
        (d)    Ndugu Cosmas Sebastian MUSHI

Imetolewa na:
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
14/10/2012

This entry was posted in

Leave a Reply