Google PlusRSS FeedEmail

NHC YAVUTIA WAWEKEZAJI MAONYESHO YA NYUMBA DUBAI, KAMPUNI KUBWA ZAVUTIWA KUWEKEZA KWENYE SEKTA YA MAKAZI TANZANIA

Dubai, United Arab Emirates
Katika kile kinachoonekana ni hatua kubwa katika kuelekea kutengeneza fursa kwenye sekta ya uendelezaji wa makazi, Shirika la Nyumba la Taifa limeweka historia kwenye soko la kimataifa na kufanikiwa kwa mara ya kwanza kufanya kongamano la uwekezaji hapa Dubai ambalo limefanikiwa kufikia lengo lake la kuonyesha fursa zilizopo kwenye sekta ya ujenzi kwa makampuni makubwa ya ujenzi yaliyopo Mashariki ya Kati na kwingineko.

Tukio hili la kipekee na kihistoria kwa Tanzania lilizinduliwa na Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal na lilihudhuriwa na kampuni kubwa za ujenzi Dubai kama Damac, Nahkeel, Jumeirah na Emaar, ambazo zimehusika na ujenzi wa majengo makubwa na maarufu Dubai kama Burj Khalifa, Hoteli za Jumeira na Dubai Mall.

 Kampuni zingine zilizohudhuria kutoka ukanda wa Ghuba kama Qatar na Bahrain pamoja na nchi nyingine kama Korea, Sweden na Romania zimeonyesha kuwepo kwa nia ya kampuni kubwa kuwekeza kwenye sekta ya makazi Tanzania.

Malengo ya Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa;
Kongamano la Wawekezaji Wa Sekta ya Makazi Tanzania ni sehemu ya lengo kuu la Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Mchechu, ambaye kwa sasa analiongoza shirika hilo kubwa Afrika Mashariki.

Kipindi cha Msechu kwenye uongozi kimeonyesha mabadiliko na ubunifu mkubwa kwenye uendelezaji wa sekta ya makazi nchini. Mchechu anasema lengo kuu la kongamano hili ni hatua kubwa kuelekea mkakati wa kuionyesha dunia kuwa Tanzania ni sehemu pekee likija swala la uwekezaji na urudishaji wa faida kwenye sekta ya makazi.

 ‘Tanzania inatoa fursa ya pekee linapokuja swala la uwekezaji kwenye sekta ya makazi barani Afrika na hii ni kutokana na uwazi pamoja na utulivu wa kisiasa na amani inayopatikana nchini, uchumi unaokua pamoja na ushirikiano mkubwa unaotolewa na serikali’ anasema Mchechu.

 ‘Tukio hili la kihistoria ni sehemu tu ya mpango kamili wa kuifahamisha dunia kuhusu fursa za uwekezaji kwenye sekta ya makazi zinazopatikana nchini’ alisema Mchechu. Mchechu anaamini kuwa huu ni muda mwafaka kwa wawekezaji kuitazama Tanzania na Afrika kwa ujumla.

 ‘Zamani ilikuwa ni hatari kwa wawekezaji kuwekeza Afrika na Tanzania, lakini kwa uchumi wa leo, ni hatari kutokuwekeza Tanzania’ alisema Mchechu.

Kati ya miradi iliyoonyeshwa kwa wawekezaji ni pamoja na miradi mitatu ambayo itaendelezwa kwa kwa kipindi cha miaka 5. Hii inajumuisha miradi miwili ya kuendeleza Arusha inayoitwa Safari City na USA River ambayo kwa pamoja itakuwa na jumla ya nyumba 8000, pamoja na mradi mwingine wa kuendeleza makazi Dar es Salaam utakaofahamika kama Salama Creek Satellite City ambao utakuwa na jumla ya nyumba 9,500.

Miradi hii yote iko tayari kwa maana ya kuwa vibali vyote vya mradi vimepatikana na kinachotakiwa ni kuwekeza tu, na ndio maana kongamano hili lilikuwa muhimu kwa ajili ya kupata uwekezaji unaotakiwa.

  Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa, Nehemia Mchechu akizungumza wakati wa kongamano hilo la nyumba mjini Dubai.
    Makamu wa Rais, Dk. Bilal akizungumza
 Wageni waalikwa katika kongamano.

This entry was posted in

Leave a Reply