Google PlusRSS FeedEmail

CCM ARUSHA WAKAMILISHA UCHAGUZI KWA ASILIMIA 90

ARUSHA, TANZANIA
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Arusha kimesema, kimefanikiwa kukamilisha uchaguzi wake wa Chama na Jumuiya katika ngazi za mashina,matawi na kata kwa asilimia 90 kwa mkoa mzima.

Katibu wa siasa na uenezi wa mkoa huo, Loota Sanare alisema hayo leo alipokua akizungumza na vyombo vya habari ili kuelezea mafanikio yaliyopatikana katika uchaguzi huo ambao umeonyesha kuungwa mkono na vijana walio wengi.

Alisema asilimia 10 za matawi,mashina na kata ambazo hazijafanya uchaguzi wake zimetokana na malalamiko mbalimbali ya wanachama waliogombea kwa madai tofauti yakiwemo ya kuchezewa rafu kwa majina yao kukatwa.

Alisema hata hivyo chama kimeshaagiza nafasi hizo kujazwa mara moja kwa kufanyiwa marekebisho ya makosa mbalimbali yaliyojitokeza katika uchaguzi huo ili kuwezesha kupatikana kwa viongozi halali kupitia chaguzi hizo.

Sanare alisema katika chaguzi za ngazi za wilaya na mikoa nafasi zinazowaniwa ni uenyekiti,wajumbe wa halmashauri kuu ya wilaya,mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa,mwenezi na mchumi wa wilaya,wajumbe wa mkutano mkuu taifa na wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa.

Alisema zoezi la uchukuaji wa fomu za kuwania nafasi hizo limeanza leo Agosti 22 na litakamilika Agosti 29 ambapo aliwataka wanachama wote wa CCM wenye sifa za kuwania nafasi hizo kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi hizo.

Aidha Sanare alizungumzia kinyang’anyiro cha chaguzi ndogo mbili za udiwani katika kata ya Daraja mbili jijini Arusha na Bang’ata wilayani Arumeru ambapo tayari zoezi la kupatikana kwa wagombea ndani ya chama limeshaanza.

Akizungumzia kata ya Daraja mbili Sanare alisema mgombea ameshapatikana Philipo Mushi kupitia vikao mbalimbali vya chama ambapo wagombea walijitokeza watatu kuchukua fomu lakini ni mmoja tu ndiye aliyerejesha hali ambayo inampa nafasi ya moja kwa moja kuwa mgombea kwakua wenzake wote wanamuunga mkono.

Kuhusu kata ya Bang’ata alisema mchakato uko ndani ya vikao kwaajili ya kujadiliwa kwa majina matatu yaliyopo ili kupatikana jina moja kupitia kamati ya siasa ya wilaya inayokutana kesho ili kupitisha jina hilo.

Alitaja majina matatu yanayojadiliwa kuwa ni Ezekiel Mollel,David Mollel na Olais Mfele ambapo mgombea atajulikana kupitia kikao hicho cha kamati ya siasa ya wilaya inayokutana kesho.

This entry was posted in

Leave a Reply