NA PIUS NTIGA
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi-CCM Tanzania Bara Mzee PHILP MANGULA, amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Bara Mzee JOHN MALECELA na kushauriana kuwa Chama kisiendelee kuwafumbia Macho wanachama wanaokiuka taratibu za Chama.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ofisi Ndogo Lumumba yamelenga kuzungumzia umuhimu wa Chama kuendelea kusimamia ipasavyo kanuni za Chama hasa katika kupata viongozi kupitia chaguzi mbalimbali za Chama.
Katika mazungumzo hayo Mzee MANGULA amesisitiza kuwa viongozi wote waliochaguliwa kwa kutoa rushwa siku zao zinahesabika ndani ya Chama kwani Kamati Ndogo iliyoundwa kufuatilia suala hilo itaanza kuwaita kwa ajili ya mahojiano kila mmoja kwa wakati wowote kuanzia sasa.
Mzee MANGULA amesema Kamati hiyo ambayo ipo chini yake tayari imepokea malalamiko mengi kutoka kwa wanachama wanaowashutumu wagombea kuchaguliwa kwa kutoa rushwa katika chaguzi mbalimbali za Chama zilizofanyika mwaka jana.
Kwa upande wake Mzee MALECELA amempongeza Mzee MANGULA kutokana na kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara huku akimtaka kusimamia pasipo woga kurudisha nidhamu ya Chama kwa kuendelea kuwachukulia hatua kali viongozi waliochaguliwa kwa njia ya kutoa rushwa ndani ya Chama.