AMINA MAKILAGI |
NA MWANDISHI WETU
UMOJA wa Wanawake wa Tanzania (UWT) umelezea kusikitishwa kwake na matukio ya watu kupoteza maisha na kujeruhiwa yaliyotokea mapema wiki hii, likiwemo la kuporomoka jengo la ghorofa 16, jijini Dar es Salaam, na kusababisha vifo vya watu 36 na kujeruhiwa wengine kadhaa.
Tukio lingine lingine ni lililotokea juzi, Aprili mosi, ambako watu zaidi ya watu 20 wameelezwa kupoteza maisha baada ya kuangukiwa na kifusi katika machimbo ya Moramu, eneo la Chekereni mkoani Arusha.
Katika taarifa iliyotolewa na Makao Makuu ya UWT jijini Dar es Salaam, leo, Aprili 3, 2013, Katibu Mkuu wa Jumuia hiyo, Amina Makilagi amesema, UWT pia inalaani matukio ya kuchinjwa kwa wanawake yanayoendelea kutokea Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara ambapo taarifa zilizopo Mwanamke mmoja amechinjwa kinyama kwa kutenganishwa kichwa na kiwiliwili chake na watu wasiojulikana.
" UWT imesikitishwa na vitendo vya kinyama vinavyofanywa na baadhi ya watu wasio na moyo wa kibinadamu kwa kuwakata vichwa wanawake na kuondoka navyo kwa malengo yao binafsi hivyo kusababisha wanawake kuishi katika maisha ya wasiwasi katika nchi yao", alisema Amina katika taarifa hiyo.
Alisema, UWT inaungana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Jakaya Kikwete kwa kutoa maelekezo mazito kwa mamlaka husika kuchukua hatua kali kwa wahusika wa matukio yote.
Hata hivyo UWT imeomba hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya majanga hayo, ikiwemo kuporomoka kwa ghorofa, watu kuangukiwa na kifusi kwenye machimbo na watu kukatwa vichwa, ziwe hatua endelevu kuhakikisha matukio hayo hayatokei tena kirahisi.
"UWT pamoja na kutambua hatua za awali zilizochukuliwa hadi sasa katika matukio hayo, inaiomba Serikali kuhakikisha hatua inazochukua sasa ziwe ni endelevu ili kuhakikisha matukio kama haya ambayo kwa sehemu kubwa yanatokana na uzembe hayatokei tena", alisema Makilagi katika taarifa hiyo na kuongeza;-
"UWT inaungana na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Kikwete kwa kutoa maelekezo mazito kwa mamlaka husika kuchukua hatua kali kwa wahusika wa matukio yote".
Amina aliwaombea ndugu jamaa na marafiki wa marehemu kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya wapendwa wao ambao wameacha pengo katika familia zao na Taifa kwa ujumla na kuwaombea wapone haraka waliojeruhiwa.