Google PlusRSS FeedEmail

CCM: MGOMBEA BINAFSI KUWA PIGO KWA VYAMA VYA UPINZANI

Nape Nnauye

 Chama Cha Mapinduzi  kama mdau miongoni mwa wenye haki kisheria kutoa maoni kuhusu mabadiliko ya Katiba, leo kimetangaza msimamo wake kuhusu mambo ambayo  kinaona kwamba yanafaa kuwemo kwenye mdajala wa  katiba mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (CCM), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema mapendekezo ya CCM yapo katika sehemu mbili.

Nape alisema moja ya mambo ambayo haihofii kujadiliwa ni uwepo wa mgombea binafsi, akisema ikiwa hilo litapita katika katiba mpya, itakuwa pigo zaidi kwa wapinzani kuliko CCM.

 “Sisi CCM hatuhofii hili la mgombea binafsi, kwanza likikubalika wapinzani ndio watakaoumia.. Unadhani kama kungekuwa na mgombea binafsi nani angehamia upinzani?” Nape alisema na kuhoji .
Ifuatayo ni Taarifa Kamili kuhusu tamko hilo la CCM;
:

Kwakuwa sheria inayosimamia mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini imevipa uhuru vyama vya siasa kushiriki kwenye mchakato wa Mabadiliko hayo ya Katiba. Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi wakiongozwa na  Mwenyekiti wake, Mhe. Dk Jakaya Mrisho Kikwete, Mei 13, 2012, walifanya semina kuhusu Mwongozo wa CCM katika kushiriki katika mjadala wa Katiba Mpya.

Katika semina hiyo, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa walijadili maeneo ya Misingi Mikuu ya Taifa ambayo yanatakiwa kubaki ndani ya Katiba mpya; na Mambo ambayo hayagusi Misingi Mikuu ya Taifa lakini ni muhimu kwa nchi, mambo ambayo yako wazi kwa mjadala mpana.

Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ilijadili na kukubaliana kuwa wanachama na wananchi kwa ujumla wahakikishe kuwa Misingi Mikuu ya Taifa letu inabaki katika Katiba Mpya itayoandikwa. Misingi mikuu iliyojadiliwa na kukubalika ibaki au iingie katika Katiba Mpya ni pamoja na:

1. Kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
2. Muundo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuwa wa Serikali mbili;  Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
3. Kuendelea kuwapo kwa mihimili mitatu ya Dola (Serikali, Bunge na Mahakama).
4. Kuendelea kuwapo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
5. Kuendelea kuwapo kwa Umoja wa Kitaifa, Amani, Utulivu, Usawa na Haki.
6. Kufanyika kwa uchaguzi wa mara kwa mara katika vipindi maalumu na kuzingatia haki ya kupiga kura kwa kila mtu mwenye sifa zinazohitajika kwa mujibu wa sheria.
7. Kuendeleza uhifadhi na ukuzaji wa Haki za Binadamu na kuheshimu usawa mbele ya sheria.
8. Kuendeleza sera ya dola kutokuwa na dini rasmi, bali inaruhusu kila mtu awe na uhuru wa kufuata dini anayoitaka mwenyewe.
9. Kuendeleza sera ya serikali kuwa ndiye mmiliki wa raslimali kuu za nchi, hususan Ardhi.
10. Kuendeleza sera ya kuwapo kwa usimamizi madhubuti wa maadili ya viongozi. Kwa kuupa nguvu za kikatiba.
11. Kuimarisha madaraka ya umma.
12. Kuhamasisha Sera ya msingi ya kujitegemea.
13. Kusimamia Usawa wa jinsia na haki za wanawake, watoto na makundi mengine maalumu katika jamii.
14. Kusimamia Hifadhi ya mazingira.
15. Na kuendelea kuwapo kwa Rais mtendaji.

Mambo mengine mengine yaliyobaki, ambayo yanahusu masuala ya uendeshaji wa serikali, wananchi wapewe fursa ya kuchangia  maoni yao kwa kadri kila mmoja anavyoona inafaa kwa kuzingatia maslahi ya Taifa letu.

Mambo hayo ambayo yapo wazi kwa mjadala mpana ni pamoja na haya yafuatayo;-

1. Mambo yanayosababisha kuwapo kwa kero za Muungano zilizopo hususani Orodha ya mambo ya Muungano.
2. Utaratibu wa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
3. Madaraka ya Rais.
4. Taratibu za uteuzi wa Mawaziri/ Waziri mkuu.
5. Utaratibu wa Uteuzi wa Tume huru ya uchaguzi.
6. Swala la mgombea binafsi katika uchaguzi wa dola.
7. Kuhusu muundo wa bunge/ baraza la wawakilishi na aina ya wabunge/ wawakilishi.
8. Kuhoji mahakamani matokeo ya Uchaguzi wa Rais.
9. Uwepo wa baraza la pili la kutunga sheria.
10. Ukomo wa Idadi ya Wabunge.
11. Mfumo wa mahakama.
12. Nafasi ya Rais wa Zanzibar katika Uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
NAPE NNAUYE
Katibu wa NEC
Itikadi na Uenezi.

This entry was posted in

4 Responses so far.

  1. idadi ya watendaji kwa ngazi za mikoa, wilaya na kata ni nyingi mno na wote wanafanya kazi zinazokaribiana sana, kuwepo na mchakato mkali wa kuwachagua watu hawa kama wakuu wa mikoa na wilaya umuhimu wao ni nini hasa? na uchaguzi wa wakurugenzi upitie vigezo vya elimu ya mtu na uwezo wake kuhusu mambo ya ukurugenzi si kila mtu mtu hii ni pamoja na watendaji wote wa wizara kama makatibu na wakuu wa vitengo

  2. tusiogope mabadiliko,ilimladi tu hayavunji amani kubwa tuliyo nayo kwa miaka mingi,kwani binadamu hawezi kuzuia mabadiliko,hilo la mgombea binafsi niwazo zuri tu lifanyiwe kazi kwenye katiba mpya.

  3. Kusema ukweli kuhusu hili suala la mfumo wa serikali, siiungi mkono CCM kabisa. Hivi kwa nini mnashindwa kukubali kwamba miongoni mwa kero kubwa za Muungano ni muundo huu wa serikali mbili? Mi nawashauri mrudi mezani na kulijadili suala hili kwa umakini tena. Katika kipindi hiki ni vyema kukawepo serikali tatu zikijumuisha Tanganyika, Zanzibar na Muungano. Wawepo maraisi wa kila pande kwa ajili ya mambo yasiyo ya muungano na raisi wa Muungano awe ni kwa mambo yote ya Muungano na uwakilishi wa nchi katika majukwaa ya kimataifa. Yeye ndiye awe kiongozi mkuu wa nchi.

  4. Hamadi says:

    Kuongezea BusinessAfrica aliyoyasema: urudufu wa watendaji ni moja ya vyanzo vya urasimu na, kwa kiasi fulani, rushwa.

Leave a Reply