Google PlusRSS FeedEmail

TAMKO LA NEC KUHUSU KUKOMESHA TATIZO LA RUSHWA KWENYE UCHAGUZI NDANI YA CHAMA

 Kikao cha NEC baada ya kujadili kwa kina changamoto zinazokikabili Chama Cha Mapinduzi wakati wa uchaguzi wa ndani ya Chama kimebaini tishio la  tatizo la rushwa. Hivyo  NEC imesisitiza kusimamia kwa ukamilifu ahadi ya Mwanachama wa CCM  inayosema;
“Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa”,

Na pia kusimamia kwa nguvu zaidi Kanuni za Chama za Uchaguzi Na.33(2) inayosema:-
"Ni mwiko kwa kiongozi mgombea au mwana-CCM kutoa au kupokea rushwa. Kwa ajili hiyo, Kiongozi, mgombea yeyote wakati wa uchaguzi akithibitika kuwa ametumia rushwa katika jitihada zake za kuwania nafasi anayoiomba hatateuliwa kugombea nafasi hiyo.

Hali kadhalika, mgombea yeyote atakayethibitika kuwa ameshinda uchaguzi kwa njia ya kutoa rushwa, atanyang’anywa ushindi alioupata, na pia atazuiwa asigombee tena katika uchaguzi mwingine wowote kwa muda utakaoamuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa; au atapewa adhabu kubwa zaidi ya hiyo kama itakavyoonekana inafaa."
Hivyo basi NEC imetoa maagizo yafuatayo:-

(a)      Kuanzia sasa ni marufuku kwa mgombea wa ngazi yoyote kuzunguka matawini, kwenye kata, wilayani na mikoani kukutana na Wajumbe wa mkutano utakaomchagua kwa kisingizio cha kuwasalimu Wajumbe,kuwapa nauli au kujitambulisha. Mgombea atakayethibitika anazunguka/ amezunguka ataondolewa bila kuchelewa katika orodha ya wagombea.

(b)     Kwa watendaji na viongozi wa Chama wa ngazi zote kuanzia sasa ni marufuku kuwatembeza wagombea ndani ya maeneo yao kwa nia ya kuwatambulisha kwa wapiga kura.  Mtendaji/kiongozi atakayebainika anakiuka agizo hili atachukuliwa hatua za kinidhamu mara moja. 

(c)      Kuanzia sasa ni marufuku kwa watendaji na viongozi wa Chama wa ngazi zote kuwaitia wagombea Wajumbe wa mikutano ya Uchaguzi kwa lengo lolote lile, kwani vikao vya aina hiyo havimo katika Katiba, na ni vikao haramu vinavyopalilia rushwa. 

NEC imetoa wito kwa wana-CCM popote walipo wapige vita rushwa na watoe taarifa ya vitendo vya rushwa katika Ofisi za Chama na TAKUKURU.  Kila mwana-CCM wa dhati awe askari wa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya adui rushwa kama ilivyo imani ya mwana CCM.
UCHAGUZI BILA RUSHWA UNAWEZEKANA,  KILA MWANACHAMA, TIMIZA WAJIBU WAKO.!
Imetolewa na:-
Nape M. Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA
ITIKADI NA UENEZI
15/05/2012

This entry was posted in

One Response so far.

  1. hongera halmashauri kuu ya chama cha mapinduzi kwa uamuzi huu utakao saidia kuondoa rushwa ndani ya chaguzi za chama,kwani rushwa inafanya vijana wengi kushindwa kupata uongozi ndani ya chama kwa sababu tu hawana pesa za kuhonga wajumbe husika wa uchaguzi,pia naomba uamuzi huu uwe wa vitendo na bila kuogopana ndani ya chama,itasaidia sana tatizo hili ambalo ni kero kubwa kwa wengi,vilevile nashauli zifanyike semina za ndani kwa wanachama wetu juu ya madhara makubwa ya tatizo hili.

Leave a Reply