Google PlusRSS FeedEmail

HOJA MTAMBUKA:KINANA, KILA LINALOIJENGA CCM KWA WAPINZANI NI KOSA, SONGA MBELE

NA BASHIR NKOROMO
WALIOBOBEA katika medani ya falsafa husema, adui yako siyo lazima awe yule anayekunyooshea silaha ili kudhuru mwili au maisha yako, bali hata asiyekutakia mafanikio mema na kupuuza harakati zako za kimaendeleo ni adui tena namba moja.

Kwa mujibu wa wanafalsafa hao, tofauti na adui wa kukudhuru mwili au maisha yako ambaye akikushikia silaha unamtambua mara moja, asiyekutakia mema na kupuuza harakati zako za kimaendeleo, inakubidi uwe mweledi sana kumtambua haraka.

Wanasema, moja ya dalili za adui wa aina hiyo, ni yule ambaye ukifanya jambo linalokupeleka kwenye mafanikio makubwa analiponda kuwa halifai, na ukifanya baya linalokudidimiza anakusifia kwamba hilo ndilo zuri na la maana kuendelea nalo.

Ushauri unaotolewa na wanafalsafa hao, ni kwamba, ukishamtambua mtu kuwa ni adui yako, ukimsikia anakusifu kuwa jambo fulani unalofanya ni nzuri achana nalo mara moja, lakini akiliponda kwa nguvu zake zote kuwa unalofanya halina manufaa na kwamba ni la hovyo sana, basi jambo hilo ni jema, endelea kulifanya, yaani songa nalo mbele.

Katika gazeti moja la Raia Mwema, ambalo nimetokea kuliamini sana kuwa ni moja ya magazeti mahiri nchini na bila shaka nitaendelea kuamini hivyo, katika toleo lake la Novemba  28, mwaka huu, Mwandishi mmoja Evarist Chahali ambaye ameandika uchambuzi wake akiwa Uskochi, amejaribu kuandika uchambuzi alioupa kichwa cha  'Kosa la Kwanza kwa Kinana'.

Katika mtiririko wa uchambuzi huo ameeleza mengi akimsadifu Kinana hadi na wanasiasa za Marekani. Lakini  kwa kuwa sina muda na nafasi ya kutosha ya kukuchosha msomaji kwa kuyarejea aliyoandika, afadhali nijadili naye kuhusu jambo moja tu alilojaribu kulifanya jamii ilione kuwa ni kosa la kwanza alilofanya Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana, wakati wa mkutano wa CCM, uliofanyika mjini Geita wiki iliyopita.

Chahali anajaribu kushawishi wasomaji wakubaliane nake kwamba hatua ya Kinana kukabidhi leseni kwa wachimbaji madini wadogo 21, kwenye machimbo ya Mugusu, wakati wa mkutano huo eti ilikuwa ni aina ya kuhodhi mamlaka ya Wizara ya Nishati na Madini inayoratibu na kusimamia shughuli za madini nchini ikiwemo uchimbaji.

Tena anaenda mbali zaidi kwamba, kwa Kinana kufanya hivyo, inaweza kutafsirika kuwa ni mwendelezo wa vitendo vya kifisadi kwenye sekta ya madini hapa nchini, akisema kwamba huenda waliokabidhiwa leseni zile siyo wamiliki halisi wa leseni hizo, kwamba ni mamluki waliozipokea leseni hizo wakiwa ni vivuli vya watu wengine.

Pangine, hili la uwezekano wa kwamba waliopewa leseni walikuwa vivuli vya wengine, nisilisemee sana, kwa kuwa inawezekana. Lakini ili kulithibitisha hilo ni lazima anayetuhumu hivyo ajiridhishe kwa kujiuliza kwamba inawezekanaje hao wachimbaji wadogo 21, wawe mazuzu kiasi cha kushangilia kuzipokea leseni hizo wakati wanajua siyo zao, hasa ikizingatiwa kwamba hao ni miongoni mwa wakazi wa Geita ambao kilio chao cha kila siku ni kupata leseni za uchimbaji mdogo kwenye eneo hilo la Mgusu?

Na kama pengine walilipwa ili kuzipokea, mamia ya watu waliokuwa kwenye mkutano ule nao walishawishika vipi hadi nao wakashangilia hatua hiyo badala ya kuzomea? Maana waliokuwa kwenye mkutano huo wanawajua wote waliopakabidhiwa leseni hizo kwa sababu wote ni wakazi wa Geita.

Mimi ni miongoni mwa mamia ya watu waliokuwa kwenye mkutano huo  wa hadhara wa CCM ambao Kinana akikabidhi leseni hizo.

Ni kwamba, Wizara ya Nishati na Madini ilikuwa imeshapitia taratibu zote za kutoa leseni hizo, na kilichofanyika pale ni tukio la kukabidhi leseni tu, kama vile Mkuu shule ya  Sekondari, Chuo cha Ufundi au Chuo Kikuu, ambavyo huandaa vyeti kwa ajili ya wahitimu kisha kazi ya kuwakabidhi wanaostahili ikafanywa na mgeni rasmi aliyealikwa kwenye mahafali.

Hivi Chahali na wengine wenye mtazamo kama yeye (kama wapo), kama mgeni rasmi akikabidhi hivyo vyeti kwa wahitimu waliostahili kwa kufuzu kwa vigezo, ndiyo inamaanisha kwamba amepora mamlaka ya shule au chuo husika?

Maana katika mkutano ule, ambao bila shaka asiye itakia mema CCM ulimkera, Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, kama Taasisi ya serikali inayotekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi kilichopewa na wanachi ridhaa ya kuunda serikali, walikuwepo kutokana na kuitwa na mwajiri wao CCM ili kueleza wanavyosimamia kwa manufaa ya umma sekta ya madini.

Ili waweze kueleza vizuri mbele ya wananchi, ilikuwa ni lazima waje na ushahidi wa kutosha kuwaridhisha wananchi hao na mwajiri mwenyewe (CCM) juu ya usimamizi huo katika rasilimali hiyo adhimu Tanzania.

Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho chenye mkataba na wananchi tangu uchaguzi mkuu uliopita, kilikuwa tayari kina malalamiko kwamba wakazi wa Geita wanapata dhiki kutokana na kutopewa fursa ya kuruhusiwa kufanya uchimbaji mdogo katika mgodi wa Mugusu.

Sasa kwenye mkutano akaja Naibu Waziri wa Nishati na madini anayeshughulikia madini, Steven Masele. Alifika kuitika wito wa CCM yaani mwajiri wa serikali iliyopo madarakani, Kinana, kisha akapandishwa jukwaani  akahojiwa mbele ya wananchi, Je bwana mmefikia wapi katika kutatua kero hii ya wachimbaji wadogo? Masele akajibu " Tunazo leseni 21 kwa ajili ya wachimbaji wadogo waliofaulu vigezo ambazo tunaweza kuwakabidhi wakati wowote.

Kinana akamuuliza Masele " Je, leseni hizo zimepitia utaratibu wote vizuri na zipo tayari kuweza kukabidhiwa kwa hao wachimbaji? Masele akajibu, "ndiyo".

Baada ya hapo Naibu Waziri akamuomba Kinana kuwakabidhi leseni zao wahusika. Kinana akafanya kazi hiyo ikakamilika bila malalamiko, maana ilifuatiwa na nderemo na vifijo kwa waliopewa leseni hizo na pia kwa wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Kimsingi mtiririko mzima wa kukabidhi hati hizo ulikuwa hivyo, lakini cha kushangaza ni kwamba mchambuzi wa makala hiyo, Chahali amejaribu, kutengeneza mawazo yananyowafanya baadhi ya wasomaji wake wadhanie leseni zile zilitolewa ghafla, papo hapo na CCM!

Bila shaka Chahali amebahatika kusoma na kuhitimu masomo yake, na bila shaka wakati wa mahafali alikabidhiwa cheti na mgeni rasmi, siyo Mkuu wa Chuo. Je, wakati anapokea cheti hicho alisita kwa kuhofia kwamba kwa mgeni rasmi kumkabidhi cheti hicho alikuwa anapora mamlaka ya mkuu wa chuo?

La msingi hapa ni kwamba,  hatua ya Katibu Mkuu wa CCM, Kinana kuwakabidhi leseni wachimbaji hao wadogo halikuwa na ukiukwaji wowote na lilikuwa jema kwa CCM, ndiyo sababu kalamu za wasioitakia mema CCM wanaotamani wakiamka wakute imeondoka madarakani zimekemea tena kwa ukurasa mzima kwamba lilikuwa tukio baya na kosa la kwanza kwa katibu Mkuu huyo.

Kwa mtazamo wangu na kwa kuzingatia ushauri wa wanafalsafa, Kinana usiungame kwamba ulilofanya ni kosa la kwanza, isipokuwa ni moja ya matukio bora ya kwanza uliyofanya katika ziara yako ya kwanza tangu uteuliwe kuwa Katibu Mkuu wa CCM mapema mwezi huu kule mjini Dodoma.

Songa mbele, huku ukijitahidi kutojaribu kufanya hata moja ambalo hao wasioitakia mema CCM (ambao kwa dalili zao unawajua) watakusifu. Na siku ukiteleza ukalifanya jambo ukasikia wamekusifu hadharani, lichunguze kwa makini na uliache mara moja, usiendelee nalo.

This entry was posted in

Leave a Reply