ZANZIBAR, Tanzania
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amewaongoza viongozi na mamia ya wananchi wa Zanzibar katika mazishi ya mwanasiasa na mwanadiplomasia mkongwe Balozi Issac Abraham Sepetu yaliyofanyika huko kijijini kwake Mbuzini, Wilaya ya Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi unguja.
Serikali katika salamu zake zilitolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed imesema kuwa Marehemu Balozi Sepetu atabaki katika nyoyo za wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla kutokana na mchango wake katika kulitumikia Taifa.
Waziri Aboud alimuelezea Balozi Sepetu ambaye katika uhai wake alishika nafasi mbali mbali katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa mtu aliyeitumika nchi yake kwa uadilifu na uaminifu mkubwa hivyo msiba huo si wa familia tu bali kwa wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania.
Alisema Serikali na wananchi wa Zanzibar wamepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa hayati Balozi Sepetu na kuwaomba wanafamilia kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezi.
Akitoa salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mazishi hayo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe alisema Rais Jakaya Mrisho wa Kikwete ameguswa sana na kifo cha Balozi Sepetu ambaye aliwahi kufanya nae kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje kwa miaka kumi.
Alisema kifo chake ni pigo kwa taifa na daima watanzania watamkumbuka sana Balozi Sepetu na kubaki katika nyoyo zao kutokana na utumishi wake bora kwa taifa.
Akisoma wasifu wa Balozi Sepetu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitega Uchumi-ZIPA nchini Khamis Salum alieleza kuwa maraeehmu Balozi Sepetu alizaliwa tarehe 16 Oktoba, 1943 huko Tabora alipata elimu yake ya msingi na sekondari katika skuli ya Mtakatifu Joseph mjini Unguja ambayo sasa inaitwa Tumekuja.
Mwaka 1966 alikwenda iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwa masomo hadi mwaka 1970 ambapo alihitimu shahada ya pili katika Uchumi na sayansi ya siasa. Aliporejea nyumbani aliteuliwa kushika nafasi ya Meneja Msaidizi Mkuu wa Shirika la Shirika la Biashara Zanzibar BIZANJE.
Kabla ya kwenda masomoni nchini Ujerumani marehemu alifanyakazi katika Idara ya Habari na Utangazaji Zanzibar na aliwahi kuwa Mhariri Msaidizi wa Gazeti la Kweupe ambalo llianzishwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeid Amani Karume.
Balozi wa Sepetu aliwahi kushika nyadhifa za Naibu wa Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri wa Habari na Utalii katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi wa Tanzania katika Shirikisho la nchi za Kisoshalisti la Kisovieti wakati huo na Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo wakati huo ikiitwa Zaire.
Katika Serikali ya Zanzibar aliwahi kuwa Kamishna wa Tume ya Mipango, Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mipango.Mwaka 2000 alichaguliwa mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki hadi mwaka 2005. Hadi anaaga dunia Balozi Sepetu alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya ZIPA.
Marehemu Balozi Sepetu ameacha wajane wawili, watoto na wajukuu.
Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi pamoja na wageni mbalibali kutoka Tanzania bara.
wakati huo huo mamia ya wakaazi wa mji wa Zanzibar walitoa heshma zao za mwisho kwa mwili wa marehemu Balozi Issac Abraham Sepetu mapema asubuhi huko katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo mjini Unguja
Mwili wa marehemu uliwasili kwa boti mapema asubuhi ukitokea Dar es Salaam ambako Balozi Sepetu mauti yalimkuta.
Baadae mwili ulipelekwa katika Kanisa la Roma la Minara Miwili lililopo Shangani mjini hapa kwa misa.