ZANZIBAR,Tanzania
UONGOZI wa Chama cha Mapinduzi (ccm) kupitia Umoja wa Vijana wa Chama hicho wa Jimbo la Kiembe Samaki umepongezwa kwa utaratibu wake uliojipangia wa kuendesha na kuimarisha michezo hasa ule wa kandanda ndani ya Jimbo hilo.
Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hapo nyumbani kwake Mazizini Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akikabidhi Jezi na mipira kwa timu za soka nane zilizoshiriki Mashindano ya Kombe la Dr. Sheni ambayo yalifanyika hivi karibuni katika Jimbo la Kiembe Samaki.
Balozi Seif ambae alikuwa akitekeleza ahadi aliyoitowa wakati akiyafunga mashindano hayo kwa kuipatia seti moja ya jezi na Mipira Miwili kila timu shiriki kati ya nane zilizomenyana kwenye mashindano hayo alisema Kiembe samaki inapaswa kurejea katika historia yake ya kutoa wachezaji wazuri.
Alisema eneo la Kiembe samaki limekuwa likitajikana kwa kuwa na wanasoka mahiri ambao wengi kati yao walifanikiwa kuchezea timu kubwa mashuhuri hapa Nchini ikiwemo ile ya Taifa ya Zanzibar na ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wanamichezo hao wa Jimbo la Kiembe samaki kwamba Serikali itajitahidi kuona kero zinazowakabili wana michezo hao hasa lile tatizo la uwanja wao linatafutiwa ufumbuzi.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Kiembe Samaki Waride Bakari Jabu, Katibu wa CCM Jimbo hilo Suleiman Haroub alimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa umahiri wake anaoendelea kuwa nao wa kuimarisha michezo hapa Nchini.
Naye Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Jimbo la Kiembe Samaki Ibrahim Mbarak Ramadhan alimueleza Balozi Seif kwamba licha ya jitihada zinazochukuliwa na uongozi wa Jimbo hilo wa kuimarisha michezo lakini bado suala la ubovu wa viwanja vya michezo limekuwa kero kubwa.
Ibrahim Mbarak alifahamisha kwamba ubovu wa uwanja wao ambao pia hutumika katika sherehe za siku kuu za Iddi umekuwa ukiwanyima furaha ya kuendeleza kwa michezo yao katika kiwango kinachokubalika Kimichezo.
“ Tunatamani uwanja wetu wenye urefu unaokubalika kivipimo siku moja unahimili tumutiwa kwa mazoezi au mashindano nyakati za usiku kama vilivyo viwanja vyengine vya wenzetu ambavyo viko nje ya Mji Mkuu “. Alitoa joto lake katibu huyo wa uvccm Jimbo la Kiembe samaki. PICHA ZA TUKIO HILO
Bofya Hapa