Rais Kikwete |
Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Salamu za Rambirambi Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Ndugu Abdulrahaman Kinana kufuatia kifo cha ghafla cha Diwani wa Kata ya Njombe Mjini na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Mkoa wa Njombe, Ndugu Lupyana Fute.
Ndugu Fute alifariki ghafla tarehe 19 Oktoba, 2013 nyumbani kwake Mtaa wa Mgendela katika Kata ya Njombe Mjini kutokana na shinikizo la damu.
“Nimepokea kwa mshtuko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha ghafla cha Diwani wa Kata ya Njombe Mjini na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama chetu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Lupyana Fute ambaye, enzi za uhai wake, nilimfahamu kama Kiongozi Mchapakazi na Mwanachama Mwaminifu na Mwadilifu wa CCM aliyekisaidia sana Chama Cha Mapinduzi katika utekelezaji wa majukumu yake”, amesema kwa masikitiko Rais Kikwete katika Salamu zake za Rambirambi.
Rais Kikwete amesema anaelewa fika kuwa kuondoka kwa ghafla kwa Mheshimiwa Fute kumeleta simanzi na majonzi makubwa siyo tu kwa Familia yake, bali pia kwa Wananchi aliokuwa akiwaongoza katika Wadhifa wake wa Udiwani, Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi katika Mkoa wa Njombe, na kwa kweli kwa Wanachama wengine wa CCM kote nchini ambao wataukosa mchango wa Mwanachama huyu muhimu.
“Kutokana na Msiba huu Mkubwa, ninakutumia wewe Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahaman Kinana Salamu zangu za Rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa Viongozi muhimu katika Chama chetu. Vilevile kupitia kwako naomba Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi zifike kwa Familia ya Marehemu Lupyana Fute kwa kumpoteza Kiongozi na Mhimili Madhubuti wa Familia”, amesema Rais Kikwete na kuongeza,
“Ninawahakikishia kuwa niko pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha Maombolezo ya Mpendwa wao, na namuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza Mahala Pema Peponi Roho ya Marehemu Lupyana Fute, Amina”.
Vilevile Rais Kikwete amemuomba Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahaman Kinana kumfikishia Salamu zake za Rambirambi kwa Wana-CCM kote nchini hususan wa Mkoa Mpya wa Njombe ambao Marehemu alikuwa akiwawakilisha katika Wadhifa wake wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM. Amewaomba wafuate mfano mzuri wa uchapakazi, uaminifu na uadilifu wa Marehemu katika utendaji wa kazi zao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22 Oktoba, 2013