Google PlusRSS FeedEmail

RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE AMEWAAPISHA WAJUMBE SITA WA TUME YA USULUHISHI NA UAMUZI

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo asubuhi  amewaapisha wajumbe sita wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.

Wajumbe walioapishwa ni Bw. Cornel Kananila Mtaki ambaye anakuwa Mwenyekiti  wa tume hiyo ambapo makamisha ni  Bibi Mary Cresent Massay, Bibi Salma Abdi Chande na Bw. Evod Paul Mushi.

Makamishna wenginei Bw. Sauli Herbet Kinemela na Bw. Yahya Kitambazi Msigwa.

Wajumbe wa tume hii wanashika nafasi ya tume ya awali ambayo ilimaliza muda wao mapema mwaka 2011, ambapo wajumbe wa tume iliyoapishwa leo waliteuliwa mwishoni mwa mwaka 2011.

Wakati huo huo Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na Viongozi wa Chama cha riadha nchini ambapo amewataka viongozi hao wafufue mchezo wa riadha hapa nchini.

“Kama kuna kitu mnataka serikali isaidie itawasaidia , lakini mchezo wa riadha kama michezo mingine,  inahitaji juhudi za vilabu vya michezo yenyewe, na serikali inachangia tu lakini jukumu kubwa ni lenu.”.  Rais amesema na kuwapa changamoto ya kuanza juhudi zao hizo  katika ngazi za chini,  ambapo ndipo wanapoweza kuvitambua vipaji vya watoto, kuvikuza na hatimaye kuviendeleza.

 Rais  amewakumbusha viongozi hao kuwa ahadi yake ya kusaidia michezo iko palepale, ambapo yuko tayari kugharamia wakufunzi au walimu wa michezo mbalimbali nchini kwa ajili ya kukuza michezo hiyo hapa nchini.

Miaka ya nyuma,  Tanzania ilikuwa inavunja rekodi mbalimbali duniani  katika riadha kutokana na wanariadha wake ambao walikua mahiri na wenye viwango vikubwa duniani, lakini katika miaka ya hivi karibuni  hali ni tofauti na juhudi za kuendeleza pale walipoishia hazijawahi kufanikiwa.

Kikao hicho  pia kimehudhuriwa na Waziri wa Habari, Vijana na Michezo. Dr. Fenela Mukangara na Katibu Mkuu wa Wizara  Bw. Sethi Kamuhanda.

Rais amewataka viongozi hao wa riadha nchini kuwa wabunifu zaidi,  kushirikisha wadau wengine wenye mapenzi na moyo na riadha , ili wapate kufikia malengo yao.                                                                             
                                                                            Mwisho.

Imetolewa na 
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi, 
Premi Kibanga, Ikulu DSM. 
18 June 2012.

This entry was posted in

Leave a Reply