Google PlusRSS FeedEmail

NAIBU KATIBU MKUU WA CCM ZANZIBAR VUAI ALI VUAI AMPASHA SEIF SHARIF



TAARIFA RASMI.



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesikitishwa na baadhi ya kauli zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad, wakati alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika jana (Juni Mosi, 2013), katika Viwanja vya Kibandamaiti, Mjini Unguja.



Katika mkurtano huo, Maalim Seif ametoa kauli zinazoweza kuleta mtafaruku wa maelewano kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi (Awamu ya Saba) Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein na Rais Mstaafu wa Zanzibar (Awamu ya Sita) Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume.



Miongoni mwa kauli nyingi alizozitoa kupitia mkutano huo, zinaonyesha waziwazi kwamba Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ni muumini na mtiifu kwa Rais Mstaafu Dkt. Amani A. Karume na kwamba hana chembe ya utiifu kwa Rais wa Zanzibar aliyopo madarakani Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, ilhali anatambua fika kuwa anawajibika kwake kutokana na kumteua kushika Wadhifa huo mkubwa.



Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kinamwambia kinaga ubaga Maalimu Seif kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha 39 (2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinasema kwamba …. “ndani ya siku saba mara baada ya kushika madaraka, Rais atateua Makamu wa Kwanza na Makamu wa Pili wa Rais”… Kwa mujibu wa matakwa ya Katiba, kazi hiyo Mhe. Dkt. Shein, tayari ameshaifanya tena kwa uadilifu mkubwa sana.



Aidha, Kifungu hicho cha 39 (5) pia kinasema kuwa … “Makamu wa Kwanza wa Rais atakuwa ni Mshauri Mkuu wa Rais katika kutekeleza kazi zake atakazopangiwa na Rais”. Vile vile, katika Ibara hiyo hiyo ya 39 (9) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inasema kuwa …”Makamu wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais, wakati wote watakapokuwa madarakani watawajibika kwa Rais”.



Kutokana na kauli alizozitoa Maalim Seif Shariff Hamad, katika mkutano wa hadhara, huko Kibandamaiti, kamwe hazionyeshi utii kwa Rais wa Zanzibar aliyopo Madarakani (Dkt. Shein), ambaye ndiye aliyemteua kushika nafasi hiyo ya Makamu wa Kwanza wa Rais na badala yake anaonyesha kuwa mtii na ushirikiano wa hali ya juu kwa Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Dkt. Amani Abeid Karume, jambo ambalo sio tu linalokwenda kinyume na matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, bali pia linaonyesha dharau kwa Rais aliyopo madarakani.



Kwa manti hiyo, Chama Cha Mapinduzi Zanzibar kinalaani kwa nguvu zote kauli za uchochezi, kejeli, fitna na dharau zilizotolewa na Katibu Mkuu huyo wa CUF dhidi ya Rais wake Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa vile hazina mustakbali mwema na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyo chini ya Mfumo wa Umoja wa Kitaifa (SUK).



Aidha, kitendo hicho kilichofanywa hadharani na Maalimu Seif ni dhahiri kinawafitinisha Viongozi wetu hao wa Kitaifa wa CCM na kwamba Chama Cha Mapinduzi hakiwezi kuvumilia hata kidogo kuona au kusikia kauli kama hizo, kwani wote hao wanatokana na CCM.


 
KUHUSU KAMATI YA MARIDHIANO.

Chama Cha Mapinduzi kimeshangazwa na kustaajabishwa sana pale kinaposikia kuwepo kwa Kamati ya Maridhiano yenye Wajumbe sawia kutoka Vyama vya CCM na CUF.


Kwa kupitia kwenu waandishi wa habari, CCM haijawahi kufanya kikao cha pamoja na CUF na kukubaliana kuunda Kamati kama hiyo na wala hakuna kikao chochote cha Kikatiba cha CCM kilichowahi kujadili na kuwateua baadhi ya wanachama wake, kuwa Wajumbe wa kile kinachoitwa Kamati ya Maridhiano.



Hivyo, Chama Cha Mapinduzi. Kinawataka wana CCM na wapenda amani na utulivu wote wa Taifa letu hili, kutohadaika na uwepo wa Kamati hiyo au kauli za wale wanaodai kuwa ni wajumbe wa kamati hiyo.


KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA.

Chama Cha Mapinduzi kinakitaka Chama Cha Wananchi (CUF) kisiwasemee Wazanzibari juu ya Mchakato wa Katiba unaoendelea nchini chini ya Tume Jaji Warioba.


CCM kinaamini kuwa mchakato huo una hatua kadhaa kama zifuatazo :-

• Hatua ya Mwanzo ni kukusanya na Kuchambua maoni ya wananchi kupitia mikutano ya wananchi, itakayoitishwa na Tume. Hatua hii ilifanyika mwezi Julai na Agosti, 2012, kwa Mikoa ya Kusini Unguja na Pemba. Awamu ya pili ya hatua hiyo, ilifanyika mwezi Oktoba na Novemba, 2012, kwa mikoa ya Kaskazini Unguja na Pemba. Awamu ya Mwisho ilifanyika mwezi Disemba, katika Mkoa wa Mjini Magharibi.

HATUA YA PILI YA MCHAKATO.

Ni kutathmini, kuchambua maoni ya wananchi na hatimaye kuandaa Rasimu ya Katiba.

 
• HATUA YA TATU

Kusimamia na Kuunda Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na ya kitaasisi. Kazi hii ilifanywa na Tume mwezi Machi, 2013.


• HATUA YA NNE

Ni kuwasilisha rasimu ya Katiba mbele ya mabaraza ya Wilaya na ya Kitaasisi, ili wajumbe wa Mabaraza hayo, waweze kutoa maoni yao juu ya Rasimu hiyo ya katiba kupitia mikutano itakayoitishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Uzinduzi wa Rasimu hiyo unatarajiwa kufanyika kesho (Juni 03, 2013), katika Ukumbi wa Karemjee, Mjini Dar es Salaam.

 
Kwa mujibu wa Kifungu cha 22 (1) cha Sheria Nam. 8 ya mwaka 2011 ya Mabadiliko ya Katiba, bunge hilo Maalum litakuwa na wajumbe wafuatao :-



a) Wabunge wote wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

b) Wabunge wote wa Wawakilishi wa Zanzibar.

c) Wajumbe 166 watakaoteuliwa kutoka Makundi yafuatayo :-

i) Asasi zisizokuwa za Kiserikali

ii) Asasi za kidini

iii) Vyama vya Siasa vilivyopata usajili wa kudumu

iv) Asasi za Elimu ya Juu

v) Makundi yenye Mahitaji Maalum ndani ya Jamii

vi) Vyama vya wafanyakazi

vii) Jumuiya ya Wakulima

viii) Jumuiya ya Wafugaji na

ix) Kikundi chochote cha watu wenye malengo yanayofanana.


HATUA YA MWISHO

Hatua ya mwisho ya mchakato wa Katiba, kwa mujibu wa Kifungu cha 31 (1) cha Sheria hiyo, itakuwa ni Kura ya maoni, itakayoandaliwa, kuendeshwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar. Matokeo ya kura ya maoni yataamuliwa kwa msingi wa kuungwa mkono kwa asilimia inayozidi 50 ya jumla ya kura zote zilizopigwa kutoka T/Bara na asilimia kama hiyo kutoka Zanzibar.

Kwa hali hiyo, Chama Cha Mapinduzi kinasisitiza haja kwa wana CCM na wananchi hasa wazalendo kutokubali kusikiliza porojo zisizokuwa na msingi zinazosambazwa na wapinzani kila pembe ya Zanzibar siku hadi siku.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI.





02 JUNI, 2013.

This entry was posted in

Leave a Reply