Google PlusRSS FeedEmail

TASWIRA YA USHIRIKI WA TANZANIA KATIKA MIKUTANO INAYOENDELEA KWENYE UMOJA WA MATAIFA


Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya  Takwimu , Dkt. Albina  Chuwa  akiwasilisha hoja  na mchango wa Afrika  wakati wa majadiliano ya ajenda  kuhusu  Teknolojia ya  Habari na Mawasiliano (ICT) katika  Mkutano wa 45 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa unaoendelea hapa Makao  Makuu ya Umoja wa Mataifa.
 
Na Mwandishi Maalum, New York
Wajumbe wanaoiwakilisha  Tanzania katika Mkutano wa 45 wa  Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa  na  Mkutano wa wazi wa  Tisa wa Kikosi Kazi   kuhusu   mapendekezo ya  ajenda  za malengo mpya ya maendeleo endelevu baada ya  2015 ( SDGs), wamendelea  kutetea maslahi  ya  Tanzania kwa kushiriki na kuchangia majadiliano ya mada mbalimbali  zinazohusiana na  mikutano hiyo.

 Akichangia   katika   mada  iliyohusu Technolojia ya  Habari na Mawasiliano (ICT) ambayo ilikuwa kati ya  Mada kumi na  moja, zilizojadiliwa katika siku ya  pili ya Mkutano  wa 45 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa,   Mkurugenzi Mkuu wa  Ofisi ya Taifa ya  Takwimu,  Dkt.  Albina Chuwa  amesema,  Tanzania na  Afrika kwa ujumla  mwaka  hadi mwaka  imeendelea kupiga hatua katika eneo hilo  licha ya changamoto mbalimbali.

Amezitaja baadhi ya  changamoto hizo kuwa ni  kutokuwapo kwa uratibu kati ya wazalishaji wa takwimu za ICT na watumiaji na  kati ya wazalishaji  na watoaji wa data ambao ni chanzo  muhimu  cha taarifa.

Na kwa sababu hiyo anasema,  tatizo hili  kama halitarekebishwa linaweza kusababisha uchapishaji  usio sahihi wa takwimu  kuhusu ICT , jambo ambalo  linaweza kupelekea utoaji  wa maamuzi  ya kisera wenye  makosa.

“Uboreshaji na  Uratibu  kati ya wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa takwimu,  utaepusha kujirudia kwa  makosa yakiwamo ya  matumizi ya raslimali  fedha na watu,  raslimali ambazo ni haba katika Afrika. Akasema  Mkurugenzi Mkuu ambaye pia  ndiye aliyewasilisha hoja za Afrika katika mada hiyo ya ICT.

Aidha  akasema  kipengele  cha  takwimu za ICT kinapashwa  kuingiza katika mikakati ya kitaifa kwaajili ya maendeleo ya  takwimu na katika mipango ya kazi ya  Kikanda.

Akielezea zaidi mchango wa ICT katika  eneo zima la  ukusanyaji wa Takwimu na umuhimu wake katika  utekelezaji wa malengo mbalimbali ya maendeleo Barani Afrika, Dkt. Albina Chuwa  anasema ukusanywaji wa takwimu katika ngazi  za kitaifa lazima uimarishwe kwa kuweka utaratibu wa uratibu kati ya taasisi husika pamoja na Ofisi za Taifa za Takwimu.

Kuhusu uwezeshaji,  Mkurugenzi Mkuu  amesema,  Afrika inahitaji kuimarisha uwezo wake wa  kutafuta rasilimali  ndani ya Afrika , ili hatimaye  Afrika ijijengee uwezo wa kuboresha ukusanyaji, uchambuzi na usambazaji wa viashiria vya msingi vya ICT  katika Afrika.

Aidha   kutokana na ongezeko la matumizi ya ICT katika Afrika,  Afrika imeutaka Umoja wa Mataifa, kupitia  Kamisheni yake ya Takwimu,  kurekebisha taarifa  ilizonazo ili ziweze kutoka picha halisi ya  maendeleo ya ukuaji wa ICT   katika Afrika  ikiwa ni pamoja na hatua ambazo zimefikiwa na Bara hilo katika eneo la ICT.

Katika hatua nyingine, Dkt. Albina Chuwa akichangia katika  ajenda iliyohusu utekelezaji wa mfumo wa   mazingira ya   uhasibu wa kiuchumi  ( SEEA) alipendekeza kwamba   nchi za Afrika , Tanzania ikiwamo,  zitahitaji  kuwezeshwa kimafunzo na kiutaalamu ili  zijenge uwezo wa kuutumia mfumo huo.

Akasema Tanzania ingependa kuona  wataalamu walioandaa mfumo huo wanakuja na  mkakati wa utoaji mafunzo na  uwezeshaji kwa  nchi zinazoendelea  ikiwamo Tanzania na hasa ikizingatiwa  umuhimu wa Takwimu katika utekelezaji wa malengo mbalimbali ya maendeleo baada  ya 2015.


 Hajjat Amina Mrisho Said,  Kamishna wa Sensa,  na  Bw. Wilfred Mwingira,  Meneja wa  Shughuli za Takwimu wakifuatilia  majadiliano ya  Mkutano wa  45 wa Kamisheni ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa,  Mkutano huu  unawakutanisha  wataalamu wa takwimu kutoka nchi 24 ambazo ni wajumbe wa Kamisheni pamoja na wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa.  Mkutano  huu  unafanyika katika  kipindi ambacho tayari kuna  majadiliano ya wazi  yanayoendelea ya kikosi kazi  kinachoandaa ajenda  mpya za maendeleo endelevu baada ya 2015.   Nafasi na  umuhimu wa suala la Takwimu katika utekelezani wa malengo ya maendeleo  ni jambo ambalo  limekuwa likijitokeza mara kwa mara katika majadiliano  hayo.

 Mjumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tisa wa majadiliano kuhusu ajenda mpya za maendeleo endelevu baada ya 2015, Dkt. Lorah Madete   akijiandaa kutoa mchango wa Tanzania katika  mkutano wa pamoja kati ya wajumbe wa kikosi  kazi   k uhusu ajenda mpya za  SDGs baada ya 2015 na  Kikundi cha Wataalam ambao wamekuwa wakijadiliana na kuangalia namna gani au ni kwa vipi malengo hayo mapya ya maendeleo endelevu  baada ya 2015 yatafadhiliwa au kuwezeshwa kwa maana  ya rasilimali fedha

This entry was posted in

Leave a Reply