Google PlusRSS FeedEmail

WAANDISHI WANAWAKE WANAFANYA KAZI KATIKA MAZINGIRA MAGUMU-UTAFITI

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova,  ( kati kati) akizungumza wakati wa majadiliano kuhusu Teknolojia ya habari na mawasiliano na mchango wa  vyombo huru vya habari katika  kuwawezesha wanawake na watoto wa kike,  katika majadiliano hayo,  wazungumzaji waliokaa meza kuu ambao ni  kutoka  kushoto,   Bi. Elisa Munoz,  Mkurugenzi  Mtendaji wa  IWMF, Muwakilishi wa Kudumu wa Austria Balozi Martin Sjdik, Bw. Peter Launsky-Tieffenthal  Katibu Mkuu  Msaidizi  na mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa , Anne Bennett, Mkurugenzi Mtendaji wa Hirondelle ( USA) na Pamela S. Fall,  anayeripoti katika  kituo cha  CBS na Rais wa  chama cha Waadishi wa habari  Umoja wa  Mataifa walijadili kwa kina umuhimu wa teknolojia ya habari na mawasiliano kama nyezo muhimu ya uwezeshaji wa wanawake na watoto  wa kike, lakini pia kama  nyezo muhimu katika kuwapatia habari na taarifa mbalimbali, habari zinazoandaliwa na vyombo huru na ambavyo waandishi wake wenyewe na weledi wa matumizi ya ICT. 
Na Mwandishi Maalum, New York
Utafiti  wa pamoja  uliofanywa na Taasisi mbili za kimataifa,  zijulikanazo kama  The International News Safety ( INSI) na The International Women’s Media Foundation ( IWMF)  umebainisha kwamba,  waandishi wa  habari wanawake, wanakumbana na vurugu za aina mbalimbali  ikiwa ni pamoja na  unyanyaswaji  wa kijinsia.


 Ripoti ya utafiti  huo yenye kichwa  kisemacho “ vurugu na unyanyasaji dhidi ya wanawake katika vyombo vya habari; picha halisi. inaeleza kwamba sehemu kubwa   ya udhalilishaji huo unafanyika katika   vyombo vya  habari ambako wanafanyia kazi.


Taarifa ya  uzinduzi wa ripoti hiyo  yenye  kurasa 40  imetolewa na  Mkurugenzi Mtendaji wa  IWMF Bi. Elisa Lees Munoz, wakati wa  majadiliano ya mada  kuhusu Teknolojia ya  Habari na Mawasiliano na  mchango wa  vyombo  huru vya habari  katika uwezeshwaji wa wanawake na watoto wa kike.


Majadiliano hayo  yalifanyika  siku ya  jumanne,    sambamba na  Mkutano wa 58 wa Kamisheni   kuhusu Hali ya  Wanawake ( CSW)  unaoendelea hapa  Umoja wa Mataifa na  yaliandaliwa  kwa pamoja kati ya  Shirika la Umoja wa Mataifa la  Elimu, Sayansi na Utamaduni ( UNESCO ) na  Uwakilishi  wa Kudumu wa Austria katika Umoja wa Mataifa.


Kwa  mujibu wa  Bi, Munoz ripoti hiyo ni matokeo ya   utafiti uliofanywa taasisi hizo mbili kuanzia  mwishoni mwa mwaka jana na mwanzoni mwa mwaka huu. Kwa kuwahoji waandishi wa habari  wanawake 1,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani.


Bi Munoz anasema utafiti huo  umefanyika kwa ufadhili wa UNESCO na  Austria   na unaotoa picha ya kwanza ya aina yake na  ya kina kuhusu hatari inayowakabili wanawake wengi wanaofanya kazi katika vyombo vya habari duniani  kote.


Akielezea  matokeo zaidi ya utafiti huo, Mkurugenzi  Mtendaji wa  IWMF anasema,   karibu theluthi mbili ya wahojiwa walikiri kupokea aina moja ama nyingine ya vitisho kutokana na kazi yao, udhalilishwaji wa kijinsia,  vikiwamo pia vitendo ya kukaripiwa au kutukanwa  pasipo sababu au hata kuitwa majina ya ajabu ajabu.


Aidha  kwa mujibu wa utafiti huo     wengi wa wahojiwa hao walieleza kwamba hawakuwahi kutoa taarifa  mahali popote dhidi ya ukatili  na udhalilishwaji wanaofanyiwa  licha ya kwamba  waliathirika kisaikolojia.


“ Tunapozungumzia usalama wa waandishi wa habari,  mara  nyingi tunafikiri ni usalama wa waandishi wanaoripoti katika  maeneo hatari kama vile kwenye   vita,  migogoro au majanga asilia. Lakini ni  kwa namna gani tunafikiri kwamba  hata  vyumba vya habari vinaweza kuwa mahali hatari” anaeleza   Munoz.


Na kuongeza Utafiti huu unaonyesha kwamba waandishi wanawake mara nyingi wamo katika mazingira hatarishi  katika ofisi zao wenyewe wanakofanyia kazi, wanashambuliwa na wafanyakazi wenzao, na wanaangushwa na watu ambao wanapashwa  kuwaamini na kuwasaidia.


Utafiti huo unaonyesha pia udhalilishwaji wa waandishi  wanawake haufanywi na wakuu wao wa kazi peke yao au wafanyakazi wenzao,  bali hata  na watu wa kada mbalimbali wakiwamo wale ambao waandishi hao hutumwa kwenda kuwafanyia mahojiano au kutafuta habari .


Wazungumzaji wengine katika majadiliano hayo  walikuwa ni   Mkrugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bokova,  Bw. Peter Launsky-Tieffenthal ambaye ni Katibu Mkuu  Msaidizi  na mkuu wa Idara ya  Mawasiliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa , Muwakilishi wa kudumu wa Austria,  Balozi Martin Sjdik, Anne Bennett, Mkurugenzi Mtendaji wa Hirondelle ( USA) na Pamela S. Fall,  anayeripoti katika  kituo cha  CBS na Rais wa  chama cha Waadishi wa habari  Umoja wa  Mataifa

 Baashi ya washiri wa majadiliano kuhusu  ICT ambayo yaliandaliwa kwa pamoja na  UNESCO na Uwakilishi wa Kudumu wa Austria na kufanyika sambamba na  mkutano wa 58 wa Kamisheni   kuhusu  Hali ya Wanawake. katika majadiliano hayo, Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya International Women's  Media Foundation, (IWMF mwenye suti nyekundu, alitoa taarifa kuhusu uzinduzi utakaofanywa wa  ripoti ya utafiti kuhusu mazingira hatarishi wanayofanyia kazi waandishi wa habari wanawake.  Ripoti  hiyo yenye kurasa 40  inahusu utafiti   uliofanywa kwa kuwashirikisha waandishi wa habari wanawake  1,000 kutoka duniani  kote.
Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bibi.Anna T. Maembe, akifutilia majadiliano ambayo yameingia siku ya pili ya ajenda kuu ya Mkutano wa 58 wa Kamisheni kuhusu Hali ya Wanawake, ajenda hiyo ni mafanikio na changamoto za utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia, ( MDGs) kwa wanawake na watoto wa kike. Mkutano wa 58 wa CSW ulifunguliwa siku ya jumatatu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.

This entry was posted in

Leave a Reply