* Wanaosema inawezekana wanawadangaya wananchi
* Asema yenyewe inafungua funsa tu
* Wanaokwanza Kilimo Kwanza ni wezi, waadhibiwe
KATIBU Mkuu wa CCM, amewataka Watanzania kuacha kujidanganya au kudanganywa na mwanasiasa yeyote kwamba kuna serikali itakayoweza kutoa ajira kwa kila mtu na kwamba kuamini hivyo ni kupumbazwa kifikra..
Alisema, badala yake serikali zote ikiwemo ya Tanzania inayosimamiwa na CCM, kazi yake ni kuandaa na kuweka mazingira na fursa bora zinazowezesha wananchi kufanya kazi mbalimbali za kuweza kuinia uchumi wao na wa taifa kwa jumla.
Kinana alisema hayo kwa nyakati tofauti, akizungumza kwenye mkikuatano ya hadhara, katika wilaya mpya ya Kakonko, akiwa katika ziara mkoani Kigoma, ambayo ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya miaka 36 ya CCM zinazofikia kilele chake, Februari 3, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.
Alisema, kutokana na kutambua hilo, serikali ya Chama Cha Mapinduzi, imekuwa ikifanya jitihada za kuweka mazingira bora ya amani na utulivu hapa nchini ili kila mtu aweze kufanya shughuli zake bila bughudha wala kulazimika kukimbia eneo lake kwenda lingine kwa hofu ya kupoteza maisha.
Kinana alisema, pamoja na kuimarisha amani, Serikali imekuwa ikibuni fursa mbalimbali kuwezesha wananchi kujiajiri hasa katika sekta binafsi, ikiwemo katika viwanda na kilimo huku akisisitiza kwamba kwa kutambua kwamba kilimo ndicho kinachotoa ajira kwa watu wengi kwa zaidi ya asilimia 75, nguvu kubwa ya serikali imeelekezwa kwenye sekta hiyo.
"Tunatambua na kuamini kwamba asilimia kubwa ya waliojiajiri wapo kwenye sekta ya kilimo, ndiyo sababu serikali yenu ya CCM, imeupa umuhimu mkubwa mpango wa Kilimo kwanza ili sekta hii iweze kuwa ya mafanikio makubwa na hivyo kuweza kuinua maisha ya watu na taifa kwa jumla", alisema Kinana.
Kinana ambaye wilayani Kakonko alihutubia mikutano mbalimbali ya ndani na ya hadhara, alisema, serikali imekuwa ikiimarisha mpango wa Kilimokwanza kwa kuhakikisha wakulima wanalima kilimo cha kisasa na chenye tija, kwa kuwapatia maarifa, zana na pembejeo.
Hata hivyo Kinana alisema, wakati serikali imo katika jitihada hizo, wapo baadhi ya watu walipoewa jukumu la kusimamia usambazaji wa pembejeo wamekuwa kikwazo kikubwa kwa kwenda kinyume na inavyotakiwa na hivyo kufifisha matarajio.
"Inashangaza kwamba kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao kampuni zao zimepewa jukumu la kusambaza pembejeo kama mbolea kwa wakulima hapa Kakonko, lakini wanafanya hujuma kwa kuchelewesha mbolea na wanapoifikisha inakuwa si kwa kiwango kinachotakiwa", alisema Kinana.
"Kwa kweli hawa wanapswa kuitwa wezi, kwa sababu hawakiuki kwa makosa bali kwa makusudi kwa ajili ya ubinafsi wa kutaka kujinufaisha wao jambo ambalo lazima serikali ya CCM ichukue hatua za haraka kuwadhibiti ikiwemo kuwachukulia hatua za uhakika za kisheria wahusika", alisema.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Kasanda wilayani Kakonko,
Diwani wa Kata hiyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo ambayo ndiyo kwa sasa inasimamia shughuli za wilaya hiyo mpya ya Kakonko, Juma Maganga alimwambia Kinana kwamba, baadhi ya wafanyabiashara waliopewa jukumu la kusambaza pembejeo za kilimo hawatimizi wajibu wao kwa wakulima.
Alisema, baadhi wamekuwa wakipeleka kwa wakulima mbolea ya kukuzia kabla ya ile ya kupandia ambayo ndiyo inatakiwa kutangulia kwanza, na mmoja wa wafanyabiashara hao alipeka kwa wakulima magunia 20 tu ya mbolea badala ya 180 yaliyokuwa yanahitajika.
Pamoja na mikutano ya hadhara, Kinana amekagua shughuli za maendeleo, ikiwemo uenzi wa nyumba za zahanati katika kata ya Kasanda, ujenbzi wa daraja la Umoja katika mpaka wa Tanzania na Burundi kwenye kijiji cha Nyabibuye, Kakonko ambacho kinapakana na mkoa wa Changuzo ulioko Burundi.
Daraja hilo linalotarajiwa kukamilika Machi mwaka huu, linalengwa kuchangamsha biashara zitakazofanywa baina ya warundi na Watanzania kwenye soko jipya na la kisasa linalojengwa na wizara ya Kilimo na chakula katika kijiji cha Nyabibuye.
Kinana pia ameshiriki ujenzi wa nyumba mbili za walimu unaoendelea katika shule ya sekondari ya Nyamtukuza iliyopo kata hiyo, ambapo alishirikina na wananchi, walimu na wanafunzi kusomba mawe kwa ajili ya ujenzi huo
Wakati Kinana anafanya ziara katika wilaya za Kakonko na Kibondo, wajumbe wengine wa sekretarieti aliowasili nao mkuani Kigoma kwa ajili ya sherehe hizo za miaka 36 ya CCM wapo katika wilaya za Kasulu na Kigoma vijijini kuhamasisha maendeleo na kugagua utekelezaji wa ilani ya CCM.