Google PlusRSS FeedEmail

VIONGOZI WAWILI WA CCM, WILAYA YA BAHI WAFARIKI DUNIA


NA BASHIR NKOROMO
Ikiwa ni siku moja baada ya Katibu wa  CCM Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Sikujua Athuman Semwendo (45 ) kufariki dunia, Katibu wa Jumuiya ya Wanawake UWT, wilaya hiyo Tabu Maimbali (57) naye amefariki Dunia.

Katibu wa UWT Mkoa wa Dodoma Kaundima Kasase amemweleza mwandishi wa mtandao huu, kwamba Tabu alifariki jana jioni katika kituo cha afya cha Bahi  baada ya kujisikia vibaya na kuamua kwenda kwenye kituo hicho kupatiwa matibabu ndipo alipolazwa.

Alisema taarifa za awali zinasema kuwa marehemu alipatwa na”Low Blood Pressure” shinikizo la damu la kushuka.

Alisema  Tabu alifariki saa 10 jioni, wakati zikifanyika juhudi za kumhamishia katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Alisema mwili wa marehemu ulitarajiwa kusafirishwa leo kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli za mazishi, marehemu ameacha Mume na watoto watano.

Siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita, Katibu wa CCM wa Wilaya hiyo Sikujua Semwendo alifariki dunia katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma ambako alikuwa amelazwa .

Inaelezwa kwamba Sikujua alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa pumu jambo ambalo iliwalazimu madaktari katika hospitali hiyo kumwekea vifaa maalumu vya kupumulia lakini hata hivyo alifariki dunia.

Marehemu Sikujua alitarajiwa kuzikwa siku ya Jumamosi iliyopita Mkoani Mbeya .

This entry was posted in

Leave a Reply