Google PlusRSS FeedEmail

WASIRA: KILIMO KWANZA KUUFIKISHA UCHUMI 'MIFUKONI' MWA WANANCHI


Waziri Wasira
NA BASHIR NKOROMO, DAR ES SALAAM,
Uhalisia wa kukua kwa uchumi hadi mifukoni mwa wananchi walio wengi una matumaini ya kufikiwa kutokana na utekelezwaji  madhubuti wa kuinua Kilimo kupitia mpango wa Kilimo Kwanza unaofanywa serikali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Sera na Uratibu, Steven Wasira alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha 'Tuongee Asubuhi' cha kituo cha televisheni cha Star Tv, leo, Januari 15, 2013.

Katika kipindi hicho, kilichokuwa na mada ya 'Uhalisia na Kukua kwa Uchumi' pamoja na Wasira wazungumzaji wengine walikuwa, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Mtaalam wa Uchumi kutoka Chuo cha SAUTI cha Mwanza, Odas Bilame.

Wasira alisema, kwa sasa wananchi wengi hawaoni uhalisia wanapoambiwa kwamba uchumi wa nchi unakuwa, kwa sababu, hali ya kukuwa kwa uchumi kwa sasa hakujawagusa waajiriwa katika sekta ya kilimo ambao ndio wengi kiasi
cha asilimia 80.

Alisema, katika kipindi cha kati ya mwaka juzi na mwaka jana uchumi wa Tanzania ulionyesha kuwa umekuwa kwa kati
ya asilimia 6.5 na 6.7, lakini kukua huku kuliwagusa zaidi watumishi waliopo katika sekta nyingine kama za viwanda na
watumishi wa umma.

"Katika hali hii ambayo watumishi wa sekta zote wanategemea lazima wapate chakula na mazao mengine kutoka kwa
wakulima, ambao hawajanufaika vya kutosha na mafanikio ya kukua wa uchumi huu, ni lazima, athari za kutoonekana
ukuaji uchumi katika jamii zitakuwepo", alisema, Wasira.

Alisema, kutokana na kutambua kwamba ni lazima sekta ya Kilimo iboreshwe vya kutosha ndipo ukuaji wa uchumi utadhihirika kwa uhakika miongoni mwa wengi, Serikali imeelekeza nguvu zake kuhakikisha mpango wa Kilimo Kwanza unazaa matunda.

Alisema, katika jitihada za kufikia lengo hilo, Serikali imetenga sh. bilioni 300 kwa ajili ya kuwekeza kwenye utafiti katika kilimo, ambapo katika uwekezaji huo, sasa wapo wataalam wengi na maofisa ugani vijijini kwa ajili ya kuwezesha wakulima kufanya kilimo bora na cha kisasa.

Wasira alisema, pia kiwanda cha mbolea cha Minjingu kimejengwa ili kuongeza upatikanaji wa mbolea ili kuhakikisha kwamba kila mkulima anapata mbolea ya kutosha na kuongeza kuwa  pamoja na kiwanda hicho Serikali inao mpango wa kujenga vingine vya mbolea ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa pembejeo hiyo.

Alisema, wakati jitihada zimewekwa kwenye uinuaji sekta ya kilimo, ujenzi na uboreshaji miundombinu ya usafiri ikiwemo barabara na reli, utafungua milango ya mazao kutoka vijijini kwenda maeneo mbalimbali nchini hata nje ya nchi kwa urahisi, hatua ambayo itachochea kukua kwa kasi zaidi kwa uchumi.

Akielezea historia ya Uchumi wa Tanzania, Wasira alisema, awali hali ya uchumi ilikuwa ikienda vizuri, lakini ilianza kuathiriwa na uhaba wa mafuta uliojitokeza miaka ya 1977 lakini ukaendelea kuathiriwa zaidi na vita vya Kagera, mwaka 1978 na hadi sasa zimeendelea kuwepo changangamoto za kidunia ambapo Tanzania kama moja ya nchi zilizomo haiwezi kuzikwepa.

Kwa upande wake Profesa Lipumba, alikiri kwamba Kilimo Kwanza ni 'muarobaini' wa kukua kwa uchumi wa nchi, lakini akaonya kwamba ni lazima juhudi za makusudi zifanyike kuhakikisha kuwa uhalisia wa kukua wa uchumi ni kuigusa mifuko ya wananchi.

Pamoja na kukiri umuhimu wa mpango wa kilimo kwanza, Profesa Lipumba aliponda kwamba, licha ya mikakati mizuri  kuwepo lakini mingi ipo katika makatarasi tu, haitekelezwi kwa vitendo.

"Sasa kama dhamira ipo, umefika wakati wa watekelezaji kuacha maneno na badala yake kufanya kazi kwa vitendo zaidi", alisema Lipumba.

Kwa upande wa nafasi ya wasomi wanavyoisadifu hali ya kukua kwa uchumi Tanzania, Odax alisema, wasomi wanakubalina kwamba juhudi zikiwekezwa kwenye kilimo uchumi utakuwa.

This entry was posted in

Leave a Reply