Google PlusRSS FeedEmail

NJAMA ZA KUNDI LA WAASI LA M23 KUJIPANGA UPYA ZAFICHUKA

Na Mwandishi Maalum, NEW YORK

Martin Kobler akizungumza
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa,  limeambiwa,   kuna taarifa za  uhakika na zisizo na  shaka  kuwa  kundi la waasi la M23 limeanza  kujiunda na kujipanga upya.

Hayo yameelezwa siku ya jana, Mwakilishi wa Katibu Mkuu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mkuu wa Misheni ya Kulinda Amani  katika DRC, ( MONUSCO),
Martin Kobler

Alikuwa  akiwasilisha   mbele ya Baraza Kuu la  Usalama la Umoja wa Mataifa, taarifa ya  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  kuhusu  Misheni ya  Kulinda  Amani  ya Umoja wa Mataifa  katika DRC ( MONUSCO).


 “Tunazo taarifa za uhakika kabisa kwamba kundi hili la M23 baada ya kusambaratishwa vibaya mwezi Novemba mwaka jana, sasa limeanza kujiunda na kujipanga upya” akasema Bw. Kobler na kuongeza, “ Ninapenda kutumia nafasi hii, kuitaka Serikali ya DRC kuanza kutekeleza makubaliano  ya Nairobi. 


Na kwa nchi za Uganda na Rwanda kutoruhusu ardhi yao kutumiwa na kundi la M23 iwe ni  kujipanga upya au kwa mafunzo ya aina yoyote ”.

Mbali ya  Mkuu wa MONUSCO kutoa taarifa yake kwa  Baraza  hilo, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu katika eneo la Maziwa Makuu, Bi. Mary Robinson naye aliwasilisha taarifa yake.


Mkuu huyo wa Misheni ya  MONUSCO alieleza bayana kwamba  makundi ya waasi katika  Jamhuri ya  Kidemokrasi ya Kongo bado ni tishio kubwa katika mchakato mzima wa utafutaji wa Amani ya kudumu katika DRC na hususani katika eneo la Mashariki ya nchi hiyo.


“Uwepo wa Brigedi Maalum ( FIB) na matumizi ya ndege zisizoendeshwa na  binadamu ( UAVs), makundi yote ya waasi yanajua wazi kwamba, sasa tuna nia na uwezo wa  kutumia  nguvu kubwa   wakati wowote”. Akasisitiza   Mkuu huyo wa MONUSCO.


Katika  taarifa yake kwa Baraza  Kuu la Usalama, Bw. Kobler ,alielezea  kwa kina hali ya usalama  ilivyo nchini DRC na  kazi kubwa inayofanywa na  MONUSCO katika kuyakabili makundi ya waasi na  vilevile kutoa ulinzi kwa raia.


 Bw. Kobler alibainisha zaidi kwa kusema kuwa,“ Katika wiki zijazo, tutakuwa tumekamilisha   mapitio ya mkao wa kijeshi  katika eneo lote la   Mashariki ya Kongo. Baada ya  kukamilisha kazi hiyo tutakuwa na  urahisi wa kwenda mahali popote  na  wakati wowote  tunapohitajika, kukabiliana na tishio la aina  yoyote na kutoa ulinzi  kwa raia “ 
Naye  Bi. Mary Robinson, Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu katika eneo la Maziwa Makuu, akizungumza kwa njia ya  video tele-conferencing kutokea Kishansa DRC, ameliambia Baraza Kuu la  Usalama, kwamba wakati umefika sasa kwa nchi zile zilizotia saini Mpango Mpana wa Umoja wa Mataifa kuhusu Siasa,  Usalama na Maendeleo katika DRC na Maziwa Makuu  kuanza kutekeleza maamuzi  magumu.


Akasema  juhudi za  kutafuta Amani na usalama katika  DRC zipo katika  kipindi  muhimu hivi sasa na kutoa wito kwa viongozi waliosaini mpango huo kuanza kutelekeza ahadi zao ili hatimaye Amani iweze kupatikana.


Bi.  Robinson ambaye  kesho ( Jumanne) atahudhuria mkutano wa Wakuu wa Nchi za Maziwa Makuu ( ICGLR)utakaofanyika nchini  Rwanda alieleza pia  kwamba,  mazingira  ya utulivu yaliyokuwapo baada ya kusambaratishwa  kundi la M23 yamepotea na  kwamba eneo hilo sasa lipo katika  kipindi cha kurejea kwa machafuko.


 Akasema  utulivu huo umetoweka hasa  baada ya  kutokea kwa mashambulizi yaliyofanywa na kundi la waasi la  Alliend Democratic Forces ( ADF) katika eneo la Mashariki ya  DRC.

 
Aidha kuendelea kwa hali  ya machafuko katika  Jamhuri ya  Afrika ya Kati na  kuibuka kwa mapigano katika  Sudan ya Kusini, pia kumechangia kuwepo mdororo huo wa kiusalama mashariki ya DRC.


Na kwa sababu hiyo anasema,   utekelezaji wa mpango mpana wa kisiasa bado unabaki kuwa  suluhu pekee ya  upatikanaji wa  Amani ya kudumu, usalama, ushirikiano na maendeleo katika   eneo la Maziwa Makuu.

This entry was posted in

Leave a Reply