Add caption |
WAZIRI wa Nchi ofisi ya Rais anayeshuhulikia Utawala Bora, Kaptein mstaafu, George Mkuchika amesema migogoro ya ardhi, mauaji ya maalbino na vikongwe, wanachi kujichukulia sheria mikononi, rushwa pamoja na ujangili zinadaiwa kuwa moja ya sababu zinazochangia kuporomoka kwa Tanzania katika viwango vya utawala bora duniani.
Mkuchika aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kikao cha 30 cha kamati ya ushauri wa mkoa wa Kilimanjaro (RCC) kikao ambacho ni cha kwanza kwa mwaka 2014 na maalum kwa ajili ya kujadili vipauumbele vya Bajeti ya Mkoa huo kwa mwaka 2014/2015.
Kaptein Mkuchika alisema kutokana na taarifa zilizotolewa hivi karibuni, Tanzania inashika nafasi ya pili kwa utawala bora nyuma ya Rwanda kwa nchi za ukanda wa Afrika mashariki nyuma ya Rwanda, 17 katika ukanda wa Afrika na 102 kati ya nchi 176 duniani ambapo kwa mujibu wa taarifa hizo Tanzania imeshuka kiwango katika ukanda wa Afrika katika kipindi cha miaka miwili.
Alisema katika taarifa hizo, Tanzania ilikuwa ikishika nafasi ya 10 miaka miwili iliyopita na kuongeza kuwa kuporomoka huko kunatokana na kukithiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu, mauaji ya albino na vikongwe, mapigano ya wakulima na wafugaji, Ujangili, ambapo zaidi ya watu kumi walikufa mkoani Manyara.
“tukiangalia kiundani Matukio haya yamesababisha kwa kiasi kikubwa Tanzania kuporomoka katika viwango vya utawala bora, miaka miwili iliyopita, tulikuwa wa 10 katika bara la Afrika, Afrika mashariki tunashika nafasi ya 2, duniani tuko nafasi ya 102 kati ya nchi 176, kukithiri kwa matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu, mauaji ya albino na vikongwe, mapigano ya wakulima na wafugaji, Ujangili, zaidi ya watu kumi walikufa mkoani Manyara,” alisema Mkuchika.
Kuhusu swala la Rushwa, Mkuchika alisema tatizo hilo haliwezi kumalizwa endapo wananchi wenyewe hawatabadili tabia yao kwani uzoefu unaonesha kuwa asilimia kubwa ya Rushwa ndogo hutokana na Wananchi wenyewe.
Alisema katika swala la Rushwa, kamati za ushauri za mikoa na mabaraza ya Halmashauri zina nafasi kubwa kufanikisha vita na mapambano dhidi ya vitendo hivyo kutokana na kuhusika kwao katika maamuzi mengi yanayohusu maendeleo ya mikoa na Halmashauri zao.
“kweli kwa kiasi kikubwa kamati ya ushauri ya mkoa, mabaraza ya madiwani zina nafasi kubwa ya kupunguza tatizo la rushwa katika Halmashauri na mikoa yao, endapo watu hawa watabadilika hasa katika maamuzi wanayoyachukua katika shughuli na vikao vyao,” alisema
Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama aliwataka watendaji katika halmashauri zote za wilaya hiyo kutekeleza agizo la kutenga mgao wa asilimia 15 kwa ajili ya makundi maalum ambayo ni asilimia 5 kwa ajili ya vijana asilimia 5 ya wanawake na asilimia5 kwa ajili ya vita dhidi ya mapambano ya Ukimwi ambapo alisema mkoa haitasita kuichukulia hatua Halmashauri itakayoshindwa kutekjeleza agizo hilo.
“kila halmashauri inatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya makundi maalumu ambapo , asilimia 5 kwa vijana, tano kwa wanawake na asilimia 5 kwa ajili ya mapambano dhidi ya vita ya Ukimwi, na halmashauri itakayoshindwa kutekeleza itachukuliwa hatua kali,” alisema.