GEITA, TANZANIA
Baada ya Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Aggrey Mwanri, kuagiza waliohusika na upotevu wa sh. milioni 16.6, za Halmashauri ya Kijiji cha Katoro mkoani Geita, wakamatwe haraka na kufikishwa mahakamani, viongozi watatu wa kijiji hicho, akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji, Joel Mazemule (CHADEMA), wamekamatwa na walitarajiwa kufikishwa mahakamni leo kuhusiana na upotevu wa fedha hizo.
Mwanri alitoa agizo hilo wakati wa ziara ya Sekretarieti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa, iliyongozwa na Katibu Mkuu wa Chama, Abdulrahman Kinana, baada ya wananchi kuelezwa kuwa, viongozi hao wametafuna kiasi hicho cha fedha lakini hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yao.
Kamanda wa polisi Mkoani Geita, Leonard Paulo, katika taarifa yake kwa waandishi wa habari jana, aliwataja watuhumiwa wengine waliokamatwa pamoja na Mazemule (42) kuwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Katoro, Fundi Makanza(44) na kuwa mwingine ni Mjumbe wa serikali ya kijiji hicho kupitia CHADEMA, Charles Malegi (34).
Kamanda huyo alisema “Ni kweli tunawashikilia hawa viongozi watatu toka jana kwa tuhuma za ubadhilifu wa sh. Milioni 116.6 ambazo ni mali ya umma.”
Alieleza kwamba, polisi limefuatilia vielelezo vyote ikiwemo nakala halisi zilizotolewa na Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya wilaya ya Geita, Alexander Lumelezi na kujiridhisha, ndio maana wakawakamata.
Alisema, fedha hizo zinazodaiwa kutafunwa na watuhumiwa hao, zilitokana na ukusanyaji ushuru, toka katika vyanzo mbalimbali vikiwemo mashamba, visima na maduka yaliyopo kijijini hapo.
Alifafanua kuwa, kati ya mwaka 2010/2011 kiasi kilichokusanywa na watuhumiwa hao kilikuwa sh. mil 21.3 lakini sh. Milioni l6.6 zilipotea na hadi sasa hazijulikani zilipokwenda.
Kamanda Paul alisema, watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo kujibu tuhuma zinazowakabili.