Nape Nnauye-Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi |
--> Inataka kuwaokoa wabunge wa Chadema katika sakata hilo.
--> Yasema suala la tuhuma za rushwa kwa wabunge lisigeuzwe kuwa la kisiasa.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimelaani juhudi zinazofanywa na baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kupotosha na kuuficha ukweli juu ya tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge.
Akizungumza na waandishi a habari leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye alisema, zipo juhudi za baadhi ya wanasiasa na vyama vya siasa kujaribu kulifanya suala la tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wabunge kuwa la kisiasa kwa malengo yao.
"Mfano mzuri wa juhudi hizi ni kitendo cha Tundu Lissu, ambaye ni mbunge wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kkambi ya upinzani Bungeni cha kutoa aliyoiita orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kufanya biashara na TANESCO na kwamba ndio watuhumiwa wa rushwa inayozungumziwa", Alisema Nape na kuongeza;
"Cha kushangaza orodha yake ilikuwa na wabunge wa CCM peke yake wakati wote tunajua kuwa yapo majina ya baadhi ya wabunge wa vyama vingine hasa Chadema, yanayotajwa katika orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa hii".
Nape alisema juhudi hizo za Lissu na wenzake zinalengo la kuuficha ukweli na kujaribu kuwalinda watuhumiwa wa uhalifu wanaotokana na Chadema.
"Tunamtaka Lissu na wengine wanaofanya juhudi hizo kuacha mara moja, na badala yake tuvipe nafasi vyombo vinavyohusika vichunguze na matokeo ya uchunguzi huo yatangazwe hadharani ili tuwajue wabunge waliotusaliti", alisena Nape.
Alisema CCM inalaani vitendo vya rushwa hasa vinapohusishwa na viongozi ambao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kwamba rushwa ya namna hiyo inavuruga sana uchumi wa nchi, hivyo wanaohusika nayo haitoshi kuwaita wala rushwa tu bali ni zaidi ya wahujumu uchumi.
"Wakikithibitika ni muhimu hatua kali zichukuliwe kulikomesha kabisa hili na iwe fundisho kwa wengine", alisema Nape.
Nape alisema CCM inawapongeza watendaji wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini wakiongozwa na Waziri wao Prof. Sospeter Muhongo, Manaibu wake, Massele na Simbachawene na Katibu Mkuu, Maswi kwa uzalendo, ujasiri na umahiri wao mkubwa waliouonyesha kwa muda mfupi waliokaa kwenye wizara hiyo.
"Tunaamini uzalendo walioonyesha katika kusimamia wizara hii,utaigwa na watumishi wengine wa umma katika kuhakikisha matumizi mazuri ya rasilimali za nchi zinalindwa ili kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania yanatimia. Tunaunga mkono jitihada zao", alisema Nape.
Alisema, pia CCM inalipongeza bunge kwa kuendelea kusimamia serikali na rasilimali za nchi katika kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa ya maendeleo.
"Tunawaomba waheshimiwa wabunge wazidi kutanguliza masilahi ya taifa mbele na uzalendo mkubwa katika shughuli zao za kila siku", alimalizia.