Google PlusRSS FeedEmail

WANANCHI WAMEHIMIZWA KUTEMBELEA TOVUTI YA SEKRETARIETI YA AJIRA


Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Bw. Xavier Daudi amewataka
wahitimu na wale wote wenye kutafuta fursa za ajira Serikalini kujijengea utamaduni wa kutembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira mara kwa mara kwani kila nafasi za ajira zinapojitokeza huwekwa katika tovuti hiyo ili kutoa fursa kwa wadau walioko nje na ndani ya nchi kuweza kuziona kwa urahisi.

Amesema hayo leo, wakati akiongea na mwandishi wa habari ofisini kwake aliyetaka kujua fursa za ajira zilizoko na taratibu za mchakato wa ajira tangu kutolewa kwa tangazo hadi kupangiwa kituo cha kazi.

Daudi amesema, kwa mfano mwananchi yeyote akitembelea katika tovuti ya Sekretarieti ya Ajira hivi sasa ataona tangazo la kuitwa kazini kwa waombaji kazi waliofaulu katika usaili uliofanyika mwezi Juni, 2012 ambao wanatakiwa kuripoti kwa Waajiri; Wakala wa Vipimo, pamoja na kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii. 

Mbali na hilo, pia watakuta tangazo la kuitwa kwenye usaili kwa wale waliokidhi vigezo kulingana na nafasi walizokuwa wameomba kama zilivyokuwa zimetangazwa kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Chuo cha Mipango Dodoma, Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo na taasisi nyinginezo.

Aliongeza kuwa katika Tovuti hiyo watakuta pia tangazo la nafasi za kazi 194 zikiwemo nafasi za Wakurugenzi, Wakufunzi Waandamizi wa Vyuo, Wakufunzi Wasaidizi, Wahandisi, Mafundi Sanifu, Wakaguzi wa ndani wa hesabu, Makatibu Mahsusi, Walinzi, Wapishi na kada nyinginezo.
Aidha, amesisitiza ni muhimu kwa waombaji kuzingatia masharti ya tangazo pindi wanapotuma maombi yao kwa njia ya posta ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata fursa ya ajira serikalini maana mchakato wa ajira hufuata Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu 

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira alimaliza mahojiano yake kwa kuitaja tovuti ya Sekretarieti ya Ajira kuwa ni www.ajira.go.tz kwa wale wasioifahamu ili waweze kuifahamu.

This entry was posted in

Leave a Reply