DAR ES SALAAM,
Chama Cha Mapinduzi-CCM-kimesema kina uhakika wa kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujayo wa mwaka 2015 kutokana na kwamba bado kipo imara na kinakubalika na Watanzania wengi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndugu NAPE NNAUYE wakati akizungumza na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Tawi la Ofisi Ndogo Makao Makuu na baadhi ya wanachama wa Tawi hilo mara baada ya kufungua Ofisi Mpya ya Tawi la Ofisi Ndogo.
Kwa imani hiyo amesema hakuna sababu ya Wana-CCM kukata tamaa kwani wamezunguka Mikoani na kujionea hali halisi ya jinsi wananchi wanavyoendelea kukiamini Chama tawala ambacho ni Chama cha Wakulima na Wanyonge.
Kuhusu migongano ya Dini Katibu huyo wa NEC, Itikadi na Uenezi amesisitiza kuwa migongano hiyo itamalizwa na Chama kwa kushirikiana na viongozi na wananchi kwani CCM ndicho Chama pekee chenye kudumisha amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Mapema akisoma risala ya wanachama wa Tawi la CCM la Ofisi Ndogo ya Makao Makuu lililopo katika Kata ya Jangwani, Katibu wa Tawi Ndugu ROSE THOMAS amesifu hatua mbalimbali zinazochukuliwa na chama katika kurejesha imani ya CCM kwa wananchi.
Tawi hilo la Ofisi Ndogo lina Mashina Sita na lina wanachama 308.