NA BASHIR NKOROMO, DSM
Katika kuadhimisha siku ya kupinga ukeketaji Duniani, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kushirikiana na UNFPA, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Shirika la Kidini la TIP wamesema juhudi za pamoja zinahitajika kitaifa katika kupambana na mila ya ukeketaji.
Mkutano huo na waandishi wa habari ulioandaliwa na UNFPA katika ukumbi wa shirika hilo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kupinga ukeketaji Duniani ambayo huadhimishwa na Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kila ifikapo tarehe 6 ya mwezi Februari.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Kupinga ukeketaji Dunia 2013 ni: “Pamoja Tuwajibike; Kutokomeza Ukeketaji Nchini”. Ujumbe wa kauli mbiu unahimiza wadau wote kuwa na juhudi za pamoja kupinga ukeketaji ambo uliojikita katika mila na tamaduni za makabila ili kulinda haki na maendeleo ya wanawake na watoto.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Meshack Ndaskoi alieleza kuwa vitendo vya ukeketaji ni ukatili dhidi ya wanawake, wasichana na watoto wa kike na hivyo ni kinyume na sheria za nchi.
Ilielezwa kuwa mnamo mwaka 1996 asilimia 18 ya wanawake walikuwa wamekeketwa. Ikilinganishwa an asilimia 14.5 ya wanawake ambao walikeketwa kwa mwaka 2004, na mwaka 2010 idadi ya wanawake waliokuwa wamekeketwa ilibakia kuwa asilimia 14.6. Aidha, mikoa minane ilionesha kuwa na idadi kubwa ya mila ya ukeketaji. Mikoa hiyo ni pamoja na singida, Mara, Iringa, Manyara, Dar es salaam, Tabora, Ruvuma na Mwanza.
" Ni wazi kuwa tamaduni na mila tunazorithishwa ni nguzo ya utambulisho wa jamii zetu. Desturi na taratibu za matukio haya muhimu ambazo zinatumika kupevusha kutoka rika mbalimbali thamani yake ni kuwa kipimo cha kufikia umri wa kuitwa baba au mama", alisema Mkurugenzi huyo na kuongeza "Katika utaratibu huu tusingelitarajia kuwepo kwa madhara na ukatili wa aina yoyote. Katika hili Wizara inahimiza kuendeleza mila zenye manufaa kwa jamii, na kutaka wananchi waelimishwe zaidi kutambua mila zenye madhara na kushirikishwa katika kupata mbinu mbadala ya kuzitokomeza".
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la UNFPA yeye alisema kuwa kati ya wanawake milioni 100 hadi 140 wamekeketwa duniani wakiwemo milioni 92 katika Bara la Afrika. Mila ya ukeketaji ina madhara mengi kwa watoto wa kike na wasichana ikiwa ni pamoja na: kutokwa damu nyingi na matatizo ya mkojo, maambukizi, na matatizo wakati wa kujifungua, na chanzo cha fistula kwa wanawake wanaojifungua. Shirika la UNFPA linatoa mwito kuepuka usiri katika mila hii maana inamadhara kwa wanawake.
Naye Mwakilishi wa Kituo cha Haki za Binadamu Bi Imelida L. Urio alisisitiza kuwa ukeketaji ni ukatili dhidi ya binadamu hususan wanawake. Kwa kutambua hilo, Wajumbe wa Baraza la Umoja wa Kitaifa walipitisha mkataba wa nyongeza (2010) kutoa nguvu zaidi kwa nchi wanachama kupinga ukeketaji.
Ukeketi unapungua ingawa kuna mapungufu ya kisheria mabyo yatahitaji wadau kutoa mapendekezo yao ili Serikali iweze kuyazingatia katika sheria zake. Ilielezwa kuwa marekebisho ya kisheria yatawezesha kumlinda pia mwanamke dhidi ya ukeketaji. Sheria ya Mtoto ya 2009 inamtaja tu mtoto na hivyo wanawake wanaweza kukosa ulinzi wa kisheria.
Aidha, mashirika yasiyo ya kiserikali yamebainisha kuwa Sheria ya Mtoto 2009 haikueleza wazi ni jinsi gani mtoto aliyekimbia kukeketwa anaweza kupewa ulinzi. Maana mtoto anaweza kwenda mahakamani akaeleza kuwa anapinga kukeketwa na akalindwa kisheria. Kutokana na upungufu huu watoto wamekuwa wakikimbilia kwa viongozi wa madhehebu ya dini, polisi, Viongozi wa serikali za mtaa, makambi ya watoto, shule; na kote huko msaada wanaopewa haujitoshelezi kisheria. Mapungufu haya yatahitaji Serikali kukutana na wadau ili kuyajadili na kuyazingatia kwa manufaa ya haki za mtoto wa kike, wasichana na wanawake kwa ujumla. Hata hivyo Bibi Urio amekubali kwamba katika baadhi ya maeneo kuna watuhumiwa wa makosa ya ukeketaji mabao wanafikishwa mahakamni na kupewa adhabu stahiki.
Vilevile, Mwakilishi wa Tanzania Internalfaith Partnership (TIP) Bwana Justin Nyamoga aliwaasa wananchi kuwa ukeketaji ni ukatili maana unahusisha umwagani wa damu, maumivu na madhara ya kimwili kiakili na kisaikolojia. Hivyo taasisi za dini zinaahidi kushirikianana Serikali kuzuia na kutokomeza ukeketaji kwa kuwaelimisha waumini na wananchi kwa ujumla. Amebainisha kuwa angelipenda kuona Tanzania inachukua hatua ili kupunguza ukeketaji na hatimaye kuwa na Tanzania ambayo haina ukatili wa kijinsia hususan kuondokana kwenye orodha za nchi zenye ukeketaji duniani.