- Awaambia kazi ndo kwanza imeanza.
- Azoa vigogo kibao wa Chadema.
- Adai miaka 20 inatosha kuwakomaza.
- Awafananisha na nguruwe anayekula watoto wake mwenyewe.
- Awakumbusha upinzani si kupinga kila kitu.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa anayeshughulikia Itikadi na Uenezi Ndg. Nape Nnauye amewataka vyama vya upinzani na hasa Chadema kuacha kulialia kila siku badala yake wajipange kutoa upinzani wa kweli badala ya maigizo wanayoyafanya.
Ndg. Nape ameyasema hayo jana kwenye mkutano mkubwa wa hadhara kwenye viwanja vya mwembe yanga Temeke wakati akihutubia maelfu ya wanachi na mashabiki wa chama hicho kwenye mkutano huo.
Mkutano huo umeandaliwa na CCM mkoa wa Dar es salaam kwa lengo la kujibu mapigo ya Chadema waliofanya mkutano wao siku ya jumapili.
Nape alisema, " watani zangu acheni kujiliza kila siku, mnaishia kulialia tu. Mmekuja mwembe yanga nikadhani mna jambo la maana,kumbe kulialia tu! Yaani miaka ishirini ya vyama vingi bado mnajiliza tu? Mtakua lini?"
Nape akawndelea kusema kuwa uteuzi wa kamati kuu ya CCM ni ishara kuwa kazi imeanza,hivyo kujiliza kwao hakuta irudisha nyuma CCM.
" Tumekamilisha uchaguzi na upangaji wa safu ndani ya chama. Safu hii ina kazi kubwa mbili, kwanza kusukuma utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ili kuboresha maisha ya watanzania na kazi ya pili ni kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo 2014 na 2015"! Alisisitiza Nape
Akasema Chadema wameshindwa kukomaa mpaka sasa hata baada ya miaka 20 ya mfumo wa vyama vingi kwasababu wana tabia ya nguruwe ya kula watoto wake yenyewe.
" hawa watani kinachowamaliza ni kuwa na tabia ya nguruwe, nguruwe akishazaa watoto, akishikwa njaa hula watoto wake mwenyewe, sasa wao kila kukicha wanakula watoto wao wenyewe watakomaa lini?"alihoji Nape.
Nape anasema kwasababu ya kutokomaa kwa upinzani nchini ndo maana wamejenga tabia ya kupinga kila kitu hata yale yenye manufaa kwa wananchi.
"Mtashangaa kuwa wenzetu hupinga kila kitu cha serikali mpaka bajeti ambazo pesa zikipitishwa ndio zinajenga miundo mbinu kama barabara, zinaleta madawa, zinaajiri waalimu, zinalipa mishahara na hata posho wanazolipwa zinatokana na bajeti ya serikali, kwasababu ya tabia ya nguruwe kula hata watoto wake ilimradi ana njaa, basi wao hupinga kila kitu" alisema Nape.
"Angalieni bunge la bajeti mwezi wa nne mpaka wa saba, mtagundua hakuna mpinzani atakubali bajeti ya serikali, ambayo pesa ikipitishwa inakwenda kwenye majimbo yao pia. Bajeti iliyopita ni mpinzani mmoja tu nadhani alikubali bajeti ipite." Alieleza Nape.
Aidha Nape alisema kwenye kikao cha NEC kilichomalizika mjini Dodoma hivi karibuni pamoja na mambo mengine walijadili changamoto kubwa ya ajira nchini hasa kwa vijana na kuahidi kuwa swala hilo atalizungumzia kwa kina kwenye mkutano wa hadhara utakaofanyika Goba leo jioni.