Google PlusRSS FeedEmail

OFISA TABIBU WA BUNDA MATATANI KWA KUMTOA MIMBA MHUDUMU WA BAA

BUNDA, Tanzania
POLISI wilayani Bunda, wamesema kuwa watamfikisha mahakamani wakati wowote afisa tabibu mmoja wa halmashauri ya wilaya ya Bunda, anayetumiwa kumtoa mimba mhudumu mmoja wa baa ambaye sasa hali yake ni mbaya sana.

Afisa tabibu huyo Michael Musimu, ambaye amekuwa akifanya kazi katika kituo cha afya Manyamanya, kilichoko mjini Bunda, anashikiliwa na polisi akituhumiwa kumtoa mimba, mhudumu mmoja wa baa ijulikanayo kwa jina la Savana, iliyoko mjini hapa.

Polisi wamemtaja mhudumu huyo kuwa ni Salome Saimon Bugunda, ambaye sasa hali yake ni mbaya sana na amepelekwa katika hospitali ya rufaa Bugando iliyoko jijini Mwanza.

Imedaiwa kuwa tukio hilo liketokea juzi na kwamba baada ya Musimu, kumtoa mimba mhudumu huyo, hali yake ilibadilika na kumpeleka katika kituo cha afya Manyamanya, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya zaidi na ndipo akakimbizwa katika hospitali ya DDH Bunda ambako pia alipewa rufaa ya kwenda Bugando.

Aidha, imeelezwa kuwa mhudumu huyo, ameumizwa vibaya kwani sehemu ya utumbo wake umetolka nje.

Kukamatwa kwa afisa tabibu huyo kumetokana na mwanamke huyo kumtaja bayana kwa kuwaambia ndugu zake ambao walitoa taarifa polisi.

“Kukamatwa kwa afisa tabibu huyo kumetokana na huyo mwanamke kumtaja kwa kuwaambia ndugu zake kwamba aliyemtoa mimba hiyo ni Musimu, ambaye ndiye aliyempeleka DDH na kumtelekeza huko” kilisema chanzo kimoja cha habari ambacho akikutaka kutaja jina lake.

Licha ya polisi wilayani hapa kuthibisha kuwepo kwa tukio hilo na kumshikilia mtuhumiwa huyo, lakini kamanda wa polisi mkoani Mara, kamishina msaidizi wa polisi, Absalum Mwakyoma, amesema kuwa bado hajapatiwa taarifa kamili juu ya tukio hilo na kuahidi kulifuatilia.

This entry was posted in

Leave a Reply