Google PlusRSS FeedEmail

KIONGOZI ADAIWA KUINGIA MITINI TEMEKE, ASAKWA NA WAPIGAKURA WAKE

NA MWANDISHI WETU
VIONGOZI wa Jumuia ya Wazazi katika Kata za Temeke, Dar es Salaam, wametoa madai mazito kwa Mjumbe wao wa Baraza Kuu la Jumuia hiyo Taifa, Nicholaus Msemo, kwamba 'ameingia mitini' tangu walipomchagua kushika wadhifa huo katika uchaguzi mkuu wa Jumuia za CCM uliopita.

Wamedai kwamba tangu kuchaguliwa kwake hawajamuona kushiriki katika shughuli mbalimbali za Jumuia hiyo ikiwemo kufanya ziara walau za kuwashukuru wapigakura hao ambao ni Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuia hiyo mkoa wa Dar es Salaam.

Malalamiko hayo juu ya Msemo kudaiwa kuingia mitini, yalitolewa mwanzoni mwa wiki hii, kwa Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi mkoa wa Dar es Salaam, Angela Kizigha, katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi mmoja, ulioko Mbagala Kuu, wilayani Temeke na kuhudhuriwa na viongozi ngazi za kata zote za wilaya hiyo ambao ni Wenyeviti, Makatibu na Makatibu wa  Elimu, Mazingura na Uchumi.

Mkutano huo uliitishwa na Kizigha kwa lengo la kuwashukuru viongozi hao, kwa kumchagua kuwa Mweneyekiti wao katika uchaguzi mkuu wa Jumuia hiyo uliofanyika Mwaka jana, ambapo katika shukurani hizo, aligawa sare za Jumuia hiyo kwa wajumbe wote 60 waliohudhuria na pia kutoa sh. milioni 1.2 kwa ajili ya kuanzisha Chama Cha Akiba na Mikopo (SACCOS) kwa viongozi hao.

"Mwenyekiti, kwanza sisi wenyeviti na viongozi wengine katika kata za Temeke, tunakupongeza kwa uamuzi wako wa kutenga mda kuja kutushukuru, lakini tunaomba pia utuambie aliko Ndugu Msemo. Huyu tangu tulipomchagua akapita tena kwa mbinde hatujawahi kumuona kabisa", alisema  Mweneyekiti wa Jumuia ya Wazazi Kata ya Makangarawe Haruna Mtulya, wakati akizungumza kwa niaba ya wenzake katika mkutano huo.

Walidai kwamba mbali na kutojitokeza kuwashuku, tangu walipomchagua, Msemo amekuwa akiwapiga chenga, badala ya kuwa nao karibu kwa lengo la kuwapa ushirikiana katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wanachama na wananchi wa kawaida ambazo zimekuwa zikijitokeza katika kata zao.

Akijibu, Angela ambaye pia ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashairiki, alisema, anatambua kwamba katika Jumuia hiyo wapo baadhi ya viongozi ambao baada ya kuchaguliwa wamejiona kwamba wameshamaliza kazi, na hivyo hawajishughulishi tena, katika kufuatilia kero za wanachama na wananchi kwa jumla, na kibaya zaidi wengine hawahudhurii hata kikao vya kikatiba.

"Sitawajibu kuhusu hili la Msemo kwa kuwa siyo ajenda iliyonileta, hapa nimekuja kuwashukuru na kutatua baadhi ya kero nilizoahidi kwamba tutasaidiana kuzifanyia kazi kama kuanzisha Saccos na kugawa sare maalum za Jumuia yetu, hili nimefanya, lakini kwa kweli tunao viongozi wa aina hii na baadhi yao tunakusudia kuwaandikia barua za kujieleza kwa nini wasivuliwe uongozi kama hawataki kuutumikia", alisema Angela.

Habari zilizopatikana, zimeeleza kwamba, Kikao cha Baraza  Kuu la Jumuia ya Wazazi mkoa wa Dar es Salaam, kilichofanyika juzi, kimeazimia kumwandikia barua Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuia hiyo mkoa wa Dar es Salaam, Mustafa Yakub kutokana na kudaiwa kutoshiriki kikamilivu katika shughuli za jumuia ikiwemo kukwepa vikao rasmi.

Akizungumza kwa simu, Msemo akikana tuhuma dhidi yake, akidai kwamba amekuwa akishiriki shughuli mbalimbali ikiwemo kufadhili mikutano ya Jumuia hiyo, huku akisisitiza kwamba, kuwashukuru wapigakura siyo lazima ni jambo la kufanywa kwa hiari.

"Hayo ni majungu na fitina za kisiasa tu, mimi nimekuwa nikishiriki shughuli nyingi sana,japokuwa nimewahi kukosekana baadhi ya vikao, lakini sasa kukosekana kikao kimoja tu ndiyo ionekane sishirikiani kabisa na wenzangu? Na kuhusu hili la kuwashukuru wapigakura, hili siyo lazima ni la hiari", alisema Msemo.

Baada ya habari hii kuchapwa leo katika gazeti la UHURU, Mlalamikiwa Ndugu Msemo ameelezea kutoridhishwa na madai hayo dhidi yake. Kwa kuwa kwenye gazeti hapati zaidi fursa ya kutoa maoni yake kwa marefu na mapana, Tumeichapa stori hiyo hapa kumpa fursa hiyo ili tumsikilie.  Mbali na Msemo, wengine pia mnakaribishwa kutoa maoni kuhusu stori hii.


Mtayarishaji Mkuu
CCM Blog
0712 48008

This entry was posted in

Leave a Reply