Google PlusRSS FeedEmail

MWENYEKITI WA ZAMANI WA CCM MKOA WA MWANZA AUAWA NA WANANCHI KWA KIPIGO

MWANZA, Tanzania 
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Chama Mapinduzi (CCM) mkoani hapa na Diwani wa kata ya Kisesa wilayani Magu kwa sasa, Clement Mabina (pichani), ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa kipigo, kufuatia ugomvi wa shamba.

Habari zilizopatikana mjini hapa, na kuthibitishwa na polisi pia halmashauri ya wilaya ya Magu, zimedai kwamba, Mabina ameuwa leo saa mbili asubuhi, katika eneo la mlima wa Kanyama, Kisesa wilayani humo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Mabina ambaye alikuwa Diwani wa Kata ya Kisesa (CCM) aliuawa kwa kushambuliwa kwa mawe na mapang, baada ya kutokea kutoelewana na wananchi wa eneo hilo la mlima ambapo alikwenda kupanda miti kwa madai kuwa lilikuwa shamba lake.

Mkuu wa polisi wa wilaya ya Magu (OCD) aliyejitambulisha kwa jina moja la Mkapa, alikiri kutokea kwa mauaji hayo na kudai kwamba awali ilisikika milio ya bunduki kwenye eneo la Kanyama kabla ya kumtuma Mkuu wa Upelelezi wa wilaya hiyo (OC CID) kwenda katika eneo la tukio, hivyo taarifa kamili itatolewa na polisi mkoani Mwanza.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Desdery Kiswaga wakati akielekea kwenye eneo la tukio hilo leo mchana, aliliambia Uhuru kuwa alipokea taarifa za kifo cha Mabina kwa masikitiko makubwa baada ya kusikia kauawa na wananchi wenye hasira kali wakati wakigombea shamba la mlima huo.

Taarifa zaidi kutoka katika eneo la Kanyama zimedai kuwa Mwenyekiti huyo wa CCM awamu iliyopita,leo asubuhi alipofika kwenye eneo la mlima huo analolimiliki ambalo linadaiwa kuwa na mgogo baina yake na baadhi ya wananchi wa Kanyama, wananchi walifika na kumhoji kwa nini anapanda miti.

Hali hiyo ilizua mabishano makali na kutoelewana na wananchi hao ambao baadhi walikuwa na mapanga na kuzidi kuongezeka huku wakimzingira.

Kutokana na hali hiyo, Mabina alifyatua risasi hewani kuwatawanya lakini wananchi hao walianza kumshambulia kwa mawe na ndipo alipojihami kwa kufyatua risasi nyingine ambazo kwa bahati mbaya, moja wapo ya risasi ilimpiga mtoto mmoja aliyekuwa kwenye tukio hilo na kusabaisha kifo chake.

Wananchi hao walizidi kumshambulia kwa mawe na kumjeruhi kichwani kabla ya kumuangusha chini na kumkata kwa mapanga na kusababisha kifo chake papo hapo.

Hadi tukienda mitamboni jana mchana, habari kutoka ndani ya jeshi la polisi mkoani Mwanza zilisema kwamba, Kamanda mpya wa mkoa huo Varentin Mlowola, alikuwa katika eneo la tukio akiongoza timu ya askari kuwasaka wananchi hao waliojichukulia sheria mkononi.

Marehemu Mabina hadi anakumbwa na mauti hayo, alikuwa Diwani wa Kata ya Kisesa. Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Magu na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Mwanza kwa kipindi cha miak mitano, kabla ya kushindwa na Dkt Anthon Diallo katika uchaguzi mkuu wa Chama mwaka jana.

This entry was posted in

Leave a Reply