UFAFANUZI WA MAMBO MBALIMBALI YALIYOPOTOSHWA NA MHE. ZITTO ZUBERI KABWE – NAIBU KATIBU MKUU WA CHADEMA KATIKA HOTUBA YAKE ALIYOITOA KWA WATANZANIA WAISHIO NCHINI MAREKANI
1. KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA MPYA
Katika hotuba yake anadai kwamba mchakato wa Katiba Mpya unaoendelea hivi sasa unatokana na shinikizo la CHADEMA, Asasi za kiraia na viongozi wa dini.
UFAFANUZI
Huo ni upotoshaji mkubwa na wa wazi kabisa unaolenga kufuta historia sahihi ya mchakato wa uandikaji au upatikanaji wa Katiba Mpya unaoendelea hivi sasa.
Ni jambo lililo dhahiri kabisa kwamba mchakato wa Katiba Mpya ni utekelezaji wa hotuba ya Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyoitoa katika salamu za kuaga mwaka 2010 kukaribisha mwaka 2011 na baadaye katika sherehe za Chama Cha Mapinduzi kutimiza miaka 34 Mjini Dodoma. Hili ndilo chimbuko halisi la hoja ya Katiba Mpya.
Akitoa maamuzi hayo alisema Katiba iliyopo sasa ni nzuri, imetuvusha salama miaka hamsini iliyopita, tukiwa wamoja, imetujengea umoja wa Kitaifa. Lakini katika kipindi hicho hicho kumetokea mabadiliko mengi duniani na hapa nchini ya kisayansi, kiteknolojia, kitamaduni, kisiasa n.k. Hakuna shaka kwamba sasa tunahitaji Katiba Mpya itakayotuvusha miaka mingine 50 ijayo. Jambo hili Zitto Kabwe kalinukuu kwenye hotuba yake anaposema kuwa:-
“Tanzania tunayoitaka kwa miaka mingine hamsini ….” Mantiki hii ya miaka mingine 50 inatokana na hotuba ya Mhe. Dr. Jakaya M. Kikwete sio yeye.
2. KUHUSU UBADHIRIFU SERIKALINI
Katika hotuba yake amedai kuwa CHADEMA ndio viongozi waliobeba dhamana ya mpito huu, kutoka Serikali ya kibadhirifu isiyojali watu mpaka Taifa lenye demokrasia iliyokomaa na lenye maendeleo na ustawi wa watu wake. (Developmental Democratic State).
UFAFANUZI
Kwanza CHADEMA haina “dhamana” ya uongozi wa nchi, mwenye dhamana ya uongozi wa nchi ni Chama Cha Mapinduzi ambacho kina Rais ambaye ni Mkuu wa nchi, Mkuu wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. CHADEMA wanachokitafuta ni Mob leadership ambayo ni fujo “Anarchy or law lessness” kitu ambacho huwezi kukidhibiti hata ukishika madaraka (mfano ni Libya, Mali, Algeria n.k.).
Mob leadership ni fujo kwa sababu ina watu ambao hawana sera ya pamoja hawana wajibu wa kisheria, hawana maslahi ya kijamii na kidini, wanadai haki bila wajibu.
Dhamana ya kuwafikisha watu katika Serikali ya kidemokrasia imo mikononi mwa Serikali iliyopo madarakani. Matamshi yanayotolewa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA yanaonyesha dhahiri kuwa hawathamini demokrasia ya nchi, umoja wa kitaifa wala amani na utulivu.
Mfano:-
(i) Tamko la Mhe. Joshua Nassari la kumzuia Rais, Mkuu wa Nchi, asikanyage Mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania.
(ii) Tamko la Mhe. Kabwe la kudai kuwa Wazanzibar wameporwa mafuta na gesi.
(iii) Hata kwenye uchaguzi mdogo wa Mbeya vijijini mwaka 2009 CHADEMA ilitamka kwamba Mhe. Ali Hassan Mwinyi Rais Mstaafu asikanyage Mbeya.
(iv) Tamko la Mhe. Wenje kuwa Mwanza inajitosheleza kuwa nchi kwa rasilimali zake na hivyo kupendekeza serikali za majimbo ili Mwanza ijiendeshe yenyewe.
Matamko haya hayawezi kutamkwa na kiongozi mmoja wa CHADEMA bila ridhaa ya Chama ama sivyo wangekuwa wanachukuliwa hatua na Chama chao.
Kwa kuwa matamshi haya ni uhaini, uchochezi na ufashisti (ANARCHY). Kauli hizi zinaweza kupelekea machafuko katika nchi, mgawanyiko, ubaguzi, fujo na umwagaji damu, mambo ambayo yatamwathiri kila raia wa Tanzania bila kujali Chama chake cha kisiasa.
Kwa hiyo, Chama Cha Mapinduzi ambacho kina dhamana ya uongozi wa nchi hii kinalaani matamshi hayo na kinawataka viongozi wa vyama vya siasa waache kutoa matamshi ya hovyo na hatari kwa mstakabali wa Taifa letu. Chama Cha Mapinduzi kinaitaka Serikali kufuatilia matamshi haya kwa kina na itoe taarifa kwa wananchi.
3. KUHUSU WATANZANIA KUTAKA UONGOZI MPYA
Katika utangulizi wa hotuba yake amedai kuwa “watanzania kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu wameamka na kutaka mabadiliko ya kisiasa na hasa kutaka kabisa uongozi mpya wa nchi kutoka Chama kingine tofauti na Chama kinachoongoza hivi sasa.”
UFAFANUZI
Chama kinachoongoza hivi sasa ni Chama Cha Mapinduzi “CCM” unapozungumza kauli kama hii lazima uangalie na hali halisi ya Chama chenyewe kama Taasisi.
Kwanza, Chama Cha Mapinduzi kina wanachama hai wengi ambao ni watanzania kuliko CHADEMA.
Pili, Chama Cha Mapinduzi kina mashabiki na wapenzi wastaarabu ambao ni watanzania wengi kuliko CHADEMA.
Tatu, Chama Cha Mapinduzi katika mfumo wake hakijapata ombwe la uongozi, kina uongozi katika ngazi za Shina, Tawi, Kata, Jimbo, Wilaya, Mkoa na Taifa na hao wote ni watanzania. Na kama kuna Chama chenye heshima ya kuwasemea watanzania wote kila kona ni CCM sio Chama kingine chochote.
Nne, katika uchaguzi wa ndani ya Chama wa mwaka 2012, watanzania wameendelea kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi ndani ya CCM. Mpaka sasa Mashina yamekwishafanya uchaguzi kwa asilimia 97.56. Hao walioshiriki uchaguzi huo wa mashina ni watanzania.
Tano, katika chaguzi ndogo za Kata, Vijiji, Mitaa na Vitongoji CCM imeendelea kuongoza na wanaopiga kura nao ni wantanzania.
Sita, Chama Cha Mapinduzi tangu 2007 kimefanikiwa kufungua matawi yake nje ya nchi maeneo mbalimbali mfano India, Uingereza na Marekani. Hao ni watanzania waishio katika ulimwengu wa kwanza na wanaamini kuwa CCM bado ni imara na hata Mhe. Rais alipoalikwa juzi kuhudhuria mkutano wa G8 alikutana na wanachama wa CCM Tawi la Marekani. Kitendo cha Mhe. Rais ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa kualikwa G8 ni heshima kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi na Taifa kwa kuwa kigezo cha kumwalika kilikuwa ni demokrasia, utawala bora, amani na utulivu nchini vigezo ambavyo vinavutia wawekezaji kutoka nje.
Kwa hiyo, hoja ya Mhe. Zitto ni Batili (futile) kwa sababu anatazama kwa macho ya ubinafsi kwa lengo la kugombea Urais mwaka 2015.
Uongozi mpya kabisa wa nchi ni upi? Kwa kuwa uongozi wa nchi yoyote huru na ya kidemokrasia unapatikana kwa utaratibu wa uchaguzi wa kawaida unaozingatia Katiba na Sheria za nchi katika mazingira ya uhuru na uwazi na vyama vyote vinashiriki. Afafanue maana ya uongozi mpya kabisa na namna utakavyopatikana huku akijua kabisa kwamba vyama vyote vya siasa vitakuwa na haki ya kushiriki uchaguzi. Lazima utapata uongozi mchanganyiko kama ilivyo hivi sasa katika mfumo huu wa vyama vingi.
4. KUHUSU SERA YA MADINI YA 2009 NA SHERIA YA MADINI YA 2010
Katika hotuba yake amedai kuwa Tanzania haina sera ya Gesi asili na kwamba, sheria ya madini ya mwaka 2010 imetokana na shinikizo la CHADEMA na Asasi za kiraia.
UFAFANUZI
Chama Cha Mapinduzi katika ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo inapatikana katika website ya CCM www.ccm.or.tz katika ibara ya 55 ya ilani imeeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya madini kwa kipindi cha 2005/2010, ambayo ni pamoja na kukamilika kwa sera ya madini ya 2009 na kupitishwa kwa sheria ya madini ya mwaka 2010.
Mhe. Kabwe mwaka 2009 alikuwa wapi kutoa mchango wake?
Hoja hii ni ya CCM yeye na Chama chake wameidandia kwa malengo ya kibinafsi na sio maslahi ya nchi.
5. SUALA LA URAIA WA NCHI MBILI (DUAL CITIZENSHIP)
Mhe. Zitto anadai kwamba suala la uraia wa nchi mbili ni sera ya CHADEMA.
UFAFANUZI
Suala la uraia wa nchi mbili limekuwa ni sera ya Chama Cha Mapinduzi na limesimamiwa na Serikali yake, hususan Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe.
Katika hotuba ya bajeti ya 2011/2012 iliyotolewa na Mhe. Bernard Membe Bungeni katika Bunge la Nne kikao cha 31 cha tarehe 22 Julai, 2011 alisema:-
“Ni dhamira ya Wizara yangu kuona suala la uraia wa nchi mbili linazinduliwa sanjari na Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Watanzania mnapaswa kujua jinsi Zitto Kabwe anavyoiba hoja kwa manufaa binafsi alipowadanganya watanzania waishio nchini Marekani na dunia kwa ujumla akisema:-
“CHADEMA inataka suala hili lifikie mwisho kwenye mjadala wa Katiba.”
Huo ni uwongo mkubwa na uzushi, kwa kuwa dhamira hiyo ni ya Serikali ya CCM na ilishawasilishwa na Waziri mwenye dhamana Bungeni na yeye akiwepo.
6. HALI YA UCHUMI WA NCHI
Amedai kuwa uchumi unaokuwa hivi sasa sio uchumi wa watanzania bali ni uchumi wa watu wachache kwenye sekta chache kama madini, mawasiliano na ujenzi; hivyo kupelekea watanzania wengi zaidi ya 15m kuishi chini ya Tshs. 500 kwa siku, kutokuwa na uhakika wa kula na kukabiliwa na mfumuko wa bei.
UFAFANUZI
Kwanza, takwimu zake sio za kitafiti kwani hazionyeshi chanzo. Pili hazina ulinganisho wa hali ya maisha ya wananchi wa nchi zinazotuzunguka ili uchungu alionao moyoni uonekane waziwazi kama ni kweli au ni uzushi.
Mhe. Kabwe amepotosha kwa makusudi ya kulinda maslahi binafsi ya Urais wa 2015 kwa kuwa haiingii akilini kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama takwimu hizo yeye hajazisoma.
Kwa mujibu wa kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2010 kilichotolewa na Wizara ya Fedha kukuwa kwa sekta ya kilimo kumeongezeka kwa 4.2% mwaka 2010 tofauti na asilimia 3.2% mwaka 2009. Lakini katika taarifa yake anadai kuwa uchumi wa vijijini ambako ndiko kwenye kilimo umekuwa kwa asilimia moja tu (flat lining).
Katika uchambuzi wake wa hali ngumu ya uchumi na mfumuko wa bei kama angelinganisha na nchi jirani angegundua kuwa mfumuko wa bei kwa Tanzania upo chini zaidi kwa asilimia 19 ukilinganisha na nchi zinazotuzunguka ambao mfumuko ni mkubwa zaidi mfano Ethiopia ni 30%.
Katika hali halisi ya maisha ya watanzania wa vijijini chakula chao hakitokani na pesa, wanakula vitu vingi ambavyo haviingii kwenye takwimu za uchumi mfano, kuku, mayai, maziwa, mihogo, viazi vitamu, nyama n.k. Hivyo vinaliwa bila kuingia kwenye mzunguko wa soko ndio maana hakuna mtanzania anayekufa njaa. Lakini nchi jirani wanakufa njaa na wanakimbia nchi zao kwa njaa. Mfumuko wa bei ni tatizo la Dunia nzima sio Tanzania peke yake.
Huyu ni mgombea Urais wa aina gani ambaye si mkweli kwa nchi yake, hasomi takwimu na anaropoka mambo ya ndani ya nchi hovyo hovyo duniani.
7. SUALA LA FURSA YA ELIMU
Katika hotuba yake ameeleza kuwa “leo mtoto wa maskini Tanzania hapati elimu anayopata mtoto wa mwenye uwezo.” Na kwamba Tanzania ijiandae kupokea bomu litakaloletwa na kundi kubwa la vijana wasio na elimu wala ujuzi.”
UFAFANUZI
Huo ni uwongo na uzushi unaolenga kutetea maslahi binafsi. Kwa kuwa katika uchambuzi wake amejikita kwenye shule binafsi na sio shule za serikali ambazo zipo katika vijiji vyote Tanzania, vinatoa elimu huru, sawa na bila ubaguzi.
Serikali ya Tanzania imetoa fursa ya Elimu kwa kila mtoto wa Tanzania tangu awali. Mpaka imefikia wakati hata mabinti wa kazi za ndani (house girls) hawapatikani wote wapo mashuleni.
Kuthibitisha hilo mnamo tarehe 20/9/2010 Tanzania ilipata tuzo ya utekelezaji mzuri wa miradi ya Elimu katika ngazi za awali, elimu ya msingi na sekondari kutoka umoja wa mataifa. Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokea Tuzo hizo Mjini New York.
Hivi huyu Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA anakuwa wapi asiyaone haya mpaka kwenda kuwadanganya watanzania waishio Marekani huko huko ilikotolewa Tuzo?
Serikali ya CCM imejenga Vyuo vya kutosha vinavyozalisha wasomi wa kutosha na hata bomu tunalojiandaa kulikabili ni la vijana wasomi ambao hawana ajira na sio vijana wasio na elimu kama anavyodai yeye.
IMETOLEWA NA TAWI LA CCM MAKAO MAKUU
DODOMA
28/05/2012